Friday, 7 September 2018

Pikipiki hizi zisitumike kwenye michepuko-DC

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akizungumza na maafisa elimu kata wa Wilaya hiyo (hawapo pichani) muda mfupi kabla ya kuwakabidhi pikipiki zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la EQUIP-T.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga (kulia) akitoa maelezo ya awali muda mfupi kabla ya kumkaribisha mkuu wa Wilaya ya Mkalama (katikati) aweze kukabidhi pikipiki zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la EQUIP-T.

Maafisa elimu kata wa Wilaya ya Mkalama wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka (hayupo pichani) muda mfupi kabla hawajakabidhiwa  pikipiki zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la EQUIP-T.

Hizi ndio pikipiki walizokabidhiwa maafisa elimu kata leo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka amekabidhi jumla ya pikipiki 17 zilizotolewana shirika lilisilo la kiserikali linalojulikana kama “EQUIP-T”  ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na shirika hilo kama sehemu ya kuwapa hamasa maafisa elimu kata wilayani hapa.


Hafla hiyo fupi ilifanyika mapema leo asubuhi kwenye viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambapo Mhe. Masaka aliwataka maafisa elimu hao kuhakikisha wanatumia vyombo hivyo vya usafiri kuinua kiwango cha elimu wilayani Mkalama.

“Pikipiki hizi sio za matumizi binafsi na msizitumie kwenda kwenye michepuko yenu kwa sababu tunahitaji kuona pikipiki hizi zinapunguza idadi ya mimba shuleni na zinaongeza kiwango cha ufaulu” Alisisitiza Mhe. Masaka.

Kwa upande wake mwakilishi wa maafisa  elimu kata hao ambaye pia ni Afisa elimu kata wa kata ya Msingi, Bw. Elisante Mbazi aliishukuru serikali na shirika la EQUIP-T kwa vitendea kazi hivyo ambapo kwa niaba ya maafisa elimu kata wenzake, aliahidi kutumia pikipiki hizo kuongeza kiwango cha ufaulu na kuboresha elimu kwa ujumla wilayani Mkalama.

“Tulikuwa tunapata changamoto ya kuzifikia baadhi ya shule kwa ajili ya ufuatiliaji lakini sasa kupitia pikipiki hizi za kisasa, changamoto hiyo imeisha” Alimalizia Mbazi.
Pikipiki hizo zilizokabidhiwa leo zilikuwa na viambatanishi vyake vyote vya msingi ikiwemo kofia ngumu na  ‘’gloves’’ za kuvaa mikononi wakati wa kuendesha.

Wednesday, 5 September 2018

Makamu wa Rais kuinufaisha Mkalama

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa ofisini kwake Ikulu jijini Dar-salaam (picha kwa hisani ya mtandao)



Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) na Mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo (IFAD) inatarajia kuipa fursa ya kipekee wilaya ya Mkalama baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza uhakika na Usalama wa Chakula katika maeneo kame ya Tanzania (LDFS).

Mradi huo unaoendelea katika nchi 12 barani Afrika zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara unatarajiwa kutekelezwa katika vijiji vya Mpambala, Nyahaa, Lugongo na Mkiko vilivyopo katika kata ya Mpambala.

Kupitia mradi huo wananchi wa Mpambala watapata fursa ya kushiriki moja kwa moja kupitia kamati za uwakilishi za vijiji zitakazoshirikisha jinsia zote ambapo zitakuwa na kazi ya kupanga na kusimamia maliasili zilizopo kati ya vijiji kwa kukubaliana katika upangaji na matumizi yanayozingatia usawa na kuandaa miongozo.

Mradi huo unaotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao  pia utaipa serikali fursa ya kutambua teknolojia na maeneo yanayofaa kwa uvunaji wa mvua na  maeneo ya vyanzo vya maji ambapo teknolojia hiyo itasaidia kupunguza upotevu wa maji na kuongeza uzalishaji hasa kipindi cha kiangazi kwa wananchi wa kata ya mpambala.

Wananchi wa vijiji vya kata ya Mpambala pia watapatiwa mafunzo ya shamba darasa kuhusu kilimo hifadhi na mbinu bora za kilimo rafiki kwa mazingira, uboreshaji na urutubishaji wa udongo, mbinu za kilimo misitu, kilimo cha makinga maji, kilimo cha mzunguko na usimamizi shirikishi wa kudhibiti wadudu na magonjwa ya mazao.

Mafunzo hayo yataenda sambamba na kuwasaidia wakulima hao upatikanaji wa mbinu bora za kilimo na pembejeo  katika mashamba darasa yatakayoanzishwa.

Mbali na Mkalama wilaya nyingine zinazotekelezwa mradi huu hapa nchini ni Kondoa (Dodoma), Nzega (Tabora), Magu (Mwanza) na Micheweni (Kaskazini Pemba).

Wednesday, 8 August 2018

Mkalama yang'ara Nanenane Kanda ya kati

Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde (kulia) akimkabidhi cheti cha Ushindi Afisa Mifugo wa Wilaya ya Mkalama Bw. Elias Mbwambo baada ya Wilaya hiyo kuibuka mshindi wa kwanza kwa halmashauri za wilaya zilizopo Mkoani Singida kwenye kilele cha maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji (NANENANE)  Nzuguni jijini Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akimpongeza Afisa Mifugo wa Wilaya ya Mkalama Bw. Elias Mbwambo baada ya Wilaya hiyo kuibuka mshindi wa kwanza kwa halmashauri za wilaya zilizopo Mkoani Singida kwenye kilele cha maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji (NANENANE) hapa Nzuguni jijini Dodoma.

Wawakilishi wa wakulima wa Wilaya ya Mkalama wakijumuika na viongozi wa Idara za Kilimo na Mifugo za Wilaya hiyo kufurahia ushindi baada ya Wilaya hiyo kuibuka mshindi wa kwanza kwa halmashauri za wilaya zilizopo Mkoani Singida kwenye kilele cha maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji (NANENANE) Nzuguni jijini Dodoma.




“RUDI MKALAMA, KUMENOGA!”   Hiyo ndio kauli inayoweza kutumika hivi sasa baada ya Wilaya ya Mkalama kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwa Halmashauri za Mkoa wa Singida kwenye maonesho ya 22 ya sikukuu ya wakulima na Wafugaji (NANENANE)  yaliyohitimishwa leo hii na Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde.

Ushindi huo  unatokana na Wilaya hiyo kujidhatiti kikamilifu katika sekta za Kilimo na Mifugo ambapo waliweza kuonesha kwa vitendo kwa kuotesha mimea mbalimbali inayolimwa Wilayani Mkalama kupitia mashamba yao yaliyopo hapa kwenye viwanja vya Nzuguni.

Mbali na mimea hiyo iliyostawi vizuri, Mkalama pia wameweza kuonesha ustadi wa kufuga samaki na kuku ambapo wataalam wa mifugo na uvuvi waliweza kuonesha namna bora kabisa ya kufuga kuku wa kienyeji na aina mbalimbali za samaki kupitia bwawa lililopo nyuma ya banda lao  la Maonesho.

Katika hali inayoonesha kujipanga zaidi kwa Uongozi wa Wilaya ya Mkalama katika maonesho yajayo, Wilaya hiyo imeshatengeneza mabanda ya kufugia Ng’ombe na Mbuzi hivyo kwa wageni watakaotembelea banda hilo kwenye maonesho ya mwaka 2019  watapata fursa ya kujifunza namna bora ya kufuga ng’ombe na mbuzi.

Mkalama Guntooooooo!



Monday, 6 August 2018

Ni lazima taarifa za masoko ziwafikie wakulima- Masaka

PICHA 10 CHINI: Ziara  ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka aliyoifanya leo kwa kutembelea  mabanda mbalimbali ya maonesho ya Nanenane kanda ya kati yanayofanyika jijini Dodoma.











Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka leo alikuwa mgeni rasmi katika manesho ya 22 ya sikukuu ya Wakulima na Wafugaji (nanenane) kanda ya kati ambapo alitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika viwanja vya maonesho hayo jijini Dodoma.

Ziara hiyo ya Mhe. Masaka ilianzia katika banda la Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambapo aliishauri wizara hiyo kufanya matumizi mbadala ya jengo lao walilolijenga kwa ajili ya  maonesho ya Nane nane badala ya kuliacha wazi huku likisubiri siku ambayo maadhimisho ya kitaifa yatafanyikia jijini Dodoma.

“Kuna taasisi mbalimbali zinapenda kushiriki maonesho haya lakini zimekosa maeneo ya kuweka bidhaa zao, mnaweza kuwapa jengo hilo au mnaweza hata kufikiria kuweka maonesho ya utamaduni ili wananchi waweze kufahamu kwa kina tamaduni za kitanzania kwa sababu kuliacha bila matumizi yoyote kama mnavyofanya hivi sasa ni kupoteza fedha za serikali ilizowekeza wakati wa kulijenga” Alisisitiza Mhe. Masaka.

Baada ya kutoka katika banda la TAMISEMI Mhe. Masaka alielekea katika banda la wataalam wa ufugaji wa kisasa wa kuku wanaojulikana kama ‘’Silverland’’ ambapo akiwa hapo aliwashauri wataalam hao kuhakikisha elimu inayohusu ufugaji wa kuku ifike mpaka kwa wafugaji wadogo badala ya kuishia kwenye maonesho ya Nanenane.

Mhe. Masaka ambaye katika ziara hiyo aliongozana na viongozi wengine waandamizi wa Mkoa wa Dodoma na Wizara ya Kilimo alifika pia  katika banda la Mamlaka ya Maendeleo ya biashara (TANTRADE)  ambapo akiwa hapo aliisisitiza mamlaka hiyo kuhakikisha inatoa matangazo kwa wakulima juu ya masoko ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha.

“Sasa hivi wakulima wanalima lakini wengi hawajui masoko ya mazao wanayolima yako wapi matokeo yake wanajikuta wanalima kilimo kisicho na tija hivyo ninawashauri mtengeneze utaratibu mzuri wa kuwajulisha wakulima kuhusu aina ya mazao yanayohitajika sokoni na mahali yanapohitajika mazao hayo’’ Aliongeza Mhe. Masaka.

Mbali na mabanda hayo Mhe. Masaka pia alitembelea Mamlaka ya Uhamiaji, benki ya CRDB, halmashauri za wilaya za Mkalama na Chamwino, AGRICOM na Polymachinery, Sido na Benki kuu ya Tanzania (BOT).



Saturday, 4 August 2018

Miaka minne ijayo Singida na Dodoma tutaongoza korosho- Nchimbi

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akitoa hotuba jioni ya leo wakati akifungua rasmi maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na wafugaji maarufu kama nanenane kanda ya kati  jijini Dodoma.




‘’Nyie wote mlioshiriki katika maadhimisho haya ya Sikukuu ya Wakulima na wafugaji mnatakiwa kuhakikisha yale mliyojifunza yanaonekana kupitia kwa wananchi wenu huko mlipotoka’’

Ni moja ya kauli zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi wakati wa hotuba yake muda mfupi kabla hajafungua rasmi maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji kanda ya kati maarufu kama Nane nane yanayoendelea hapa jijini Dodoma.

Katika hotuba yake Mhe. Nchimbi alibainisha kuwa mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi trilioni 13.8 kwa ajili ya Kilimo na Mifugo hivyo aliwataka wadau wa sekta hizo kutumia fursa hiyo vizuri na kuhakikisha sekta za kilimo na mifugo zinakuwa chachu ya kuhakikisha azma ya Tanzania kuelekea kwenye uchumi wa viwanda inatimia.

“Leo wakati natembea kwenye mabanda mbalimbali nimekutana na mkulima ambaye katika maelezo yake amenieleza kupitia boga moja nililomkuta nalo badala ya kuliuza shilingi elfu 10 ana uwezo wa kulitumia  kuingiza zaidi ya shilingi laki moja kwa kutengeneza juice, maandazi na keki” Alisema Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi alisema kuwa hivi sasa zao la korosho  limekuwa ni zao mkakati katika mikoa ya Dodoma na Singida  ambapo viongozi wa mikoa hiyo wanataka kuhakikisha ndani ya miaka minne ijayo mikoa hiyo itakuwa vinara wa mazao hayo.

“Kwa bahati mbaya katika maeneo yaliyozoeleka kulima mazao hayo tafiti zinaonesha wanavuna mazao hayo mara moja tu kwa msimu lakini huku kwetu hasa mkoani Singida imeshathibitika zao la korosho kuweza kuvunwa mara mbili kwa mwaka” Aliongezea Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi amewataka Wakulima kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuendelea kuongeza kipato kupitia sekta hiyo kwa mwaka mzima badala ya hivi sasa ambapo wakulima wengi baada ya kuuza mavuno yao hushinda vijiweni huku wakisubiri msimu wa masika.


Thursday, 12 July 2018

Uwanja wa kisasa kujengwa Mkalama

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa katika sehemu ya watu mashuhuri ''VIP''

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa kwa muonekano wa juu

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa kwa muonekano wa mbele

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa kwa muonekano wa pembeni




Habari Njema na kubwa kwako Mwananchi wa Wilaya ya Mkalama na Tanzania kwa ujumla  ni kwamba Wilaya ya Mkalama imeanza mchakato wa Ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu utakapokuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 45,000.

Uwanja huo bora kabisa na wa kisasa unaotarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.6 unajengwa katika kijiji cha Maziliga na tayari eneo hilo limeshasafishwa huku hatua ya kulisawazisha au kufanya ‘’levelling’’ kama inayojulikana kitaalam ikitarajiwa kufanyika Wiki ijayo.

Mbali na Mpira wa Miguu, uwanja huo utakuwa na viwanja vya ndani vya michezo ya Mpira wa Kikapu, Mpira wa ikono, Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu na sehemu ya Mashindano ya riadha.

Ujenzi huo unaoratibiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Mkalama chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Mhandisi Lameck Itungi  unatarajiwa kukamilika Julai 2019 ambapo zaidi ya matofali 5000 kati ya 27,000 yanayohitajika kwa ajili ya ujenzi wa Ukuta wa Uwanja huo yameshafyatuliwa.

Kwa Mujibu wa Mhe. Itungi jumla ya mali zinazokadiriwa kuwa na  thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 800 zimeahidiwa kutolewa  na  wadau mbalimbali ambapo kiasi kingine cha Fedha kinatarajiwa kukusanywa katika Harambee itakayofanyika septemba 9 mwaka huu.

“Mgeni rasmi katika harambee hiyo anatarajiwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson hivyo nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama na Watanzania kwa ujumla mjitokeze kuunga Mkono jitihada hizi za dhati kwa ajili ya kuendeleza sekta ya Michezo Mkalama na Tanzania kwa ujumla” Alisihi Mhe. Itungi.

Tuesday, 5 June 2018

Wajasiriamali Mkalama wanufaika

PICHA 10 CHINI:  WAWAKILISHI WA VIKUNDI 10 VYA UJASIRIAMALI  WILAYANI MKALAMA WAKIPOKEA HUNDI ZA MIKOPO YA RIBA NAFUU  KUTOKA KWA MKUU WA WILAYA YA MKALAMA MHE. MHANDISI JACKSON MASAKA JIONI YA LEO.















Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka jioni la leo amevikabidhi vikundi 10 vya ujasiriamali hundi zenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 37.8  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo wa bajeti wa Serikali unayoitaka kila Halmashauri kutoa asilimia 10 ya fedha zake kuviwezesha vikundi vya wanawake na vijana mikopo ya riba nafuu.

Fedha hizo zimekabidhiwa kwenye vikundi 10, saba vya vijana na vitatu vya wanawake ambapo baada ya kukabidhi hundi hizo Mhe. Masaka alivitaka vikundi hivyo kuhakikisha vinatumia fedha hizo kufanyia shughuli za maendeleo ili viweze kupata faida na kurejesha fedha walizopewa ili watoe fursa ya vikundi vingine kukopeshwa kwa haraka.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga alisema kuwa fedha Halmashauri hiyo itaendelea kutoa fedha zaidi  kwa vikundi kulingana na ongezeko la mapato yake ya ndani.

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA