Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akizungumza na wajumbe wa Umoja wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (ALAT) ngazi ya Mkoa wa Singida mapema leo asubuhi. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akijitambulisha mbele ya wajumbe wa Umoja wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (ALAT) ngazi ya Mkoa wa Singida mapema leo asubuhi. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Daktari Rehema Nchimbi
amelaani kitendo cha Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu kushambuliwa
kwa risasi na watu wasiofahamika akiwa kwenye gari yake kilichotokea hivi
karibuni akiwa kwenye gari nyumbani kwake Dodoma.
Mhe. Nchimbi amelaani tukio hilo muda mchache kabla ya
kufungua kikao cha Umoja wa mamlaka ya serikali za mitaa (ALAT) ngazi
ya Mkoa wa Singida huku ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzungumza hadharani
kuhusiana na tukio hilo tangu kutokea kwake.
“Bila kujali itikadi za kisiasa, dini au kabila, suala
lililomtokea Mhe. Tundu Lissu linapaswa kulaaniwa na kila Mtu hasa sisi wa Mkoa
wa Singida kwa sababu ni Mbunge anayeutumikia Mkoa wetu na ni mwananchi
mwenzetu wa Mkoa wa Singida” Alisema Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi amesema kuwa ni vizuri Wananchi wote wa Mkoa
wa Singida na Tanzania kwa ujumla wawe na subira na Imani dhidi ya vyombo vya
Ulinzi na Usalama ambavyo bado vinaendelea kulifuatilia na kuchunguza tukio hilo kwa ukaribu.
“Si jambo jema kumnyooshea kidole mtu, kundi la watu au
taasisi fulani kuhusiana na tukio hili kwa sababu vyombo vyetu vya ulinzi na
usalama vipo makini sana na baada ya kumaliza kazi yao vitatoa majibu sahihi
yaliyotokana na uchunguzi wao hivyo kwa sasa tuwe na subira na tuungane
kumuombea ndugu yetu Mhe. Lissu aweze kupona na kurejea katika majukumu yake ya
kuwahudumia Watanzania” Alisisitiza Mhe. Nchimbi.
Katika kikao hicho Mhe. Nchimbi amewataka viongozi wote wa
halmashauri za Mkoa wa Singida kuwa na fikra na uongozi wa kimkakati ili kuhakikisha
wanawahudumia wananchi wote kutokana na rasilimali zilizopo bila kujali
zinatosha au la.
“Kama utakuwa na ‘strategic thinking’ maana yake utakuwa
na uwezo wa kujua namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wako
kulingana na rasilimali ulionazo na kamwe huwezi kuwa na kisingizio kuwa
miundombinu haijitoshelezi” Alisema Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi amesema baada ya kuwa na fikra za kimkakati
ni lazima viongozi wote wa Wilya husika wawe na uongozi wa kimkakati ambao
utampa nafasi kila kiongozi kwa nafasi yake kutoa mchango wake katika kutatua
changamoto za wananchi.
“Sio unaenda Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya na kumueleza
tatizo lako anasema mimi ni ‘DC’ kwa hiyo kama ni ‘DC’ ‘so what’, ni lazima katika kila changamoto
ya mwananchi mchango wa kila kiongozi uonekane” Alisisitiza Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi alihitimisha hotuba yake fupi kwa kuwataka
viongozi wanaounda umoja huo Mkoani Singida kuhakikisha wanaifanya Singida kuwa
Mkoa wa Viwanda kwa kuwavuta wawekezaji wengi zaidi kuchangamkia fursa nyingi
zilizopo Mkoani hapa.
“Kuna ngozi nyingi sana inatoka mkoani Singida, hebu
jaribuni kuangalia namna gani tunaweza kuanzisha kiwanda cha ngozi hapa na pia
naomba nyie mshiriki katika Kilimo cha mazao mbalimbali yanayostawi vizuri
Mkoani Singida huku mkisisitiza na wananchi nao kufanya hivyo na hatimaye
tuongeze uzalishaji wa mazao yanayoupa sifa kubwa mkoa wa Singida” Alimalizia
Mhe. Nchimbi.
Muangalie Mhe. Nchimbi akizungumza wakati wa kikao cha leo kwa kubonyeza hapa
No comments:
Post a Comment