Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akizungumza kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti ili aweze kufungua baraza la madiwani lililofanyika leo. |
Baadhi ya madiwani wakipitia nyaraka mbalimbali wakati wa baraza la madiwani lililofanyika leo. |
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. Loth Dia akisoma taarifa ya kamati yake ya Fedha, Mipango na Utawala wakati wa baraza la madiwani lililofanyika mapema leo. |
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega akizungumza machache muda mfupi kabla ya kufunga baraza la madiwani lililofanyika leo. |
Mwenyekiti wa kamati ya Uchumi na Mazingira Mhe. Mohamed Juma akisoma taarifa fupi ya kamati yake wakati wa baraza la madiwani lililofanyika leo. |
Baada ya jitihada za muda mrefu zilizofanywa na viongozi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, hatimaye serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzani kupitia bajeti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2018/2019 imeidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 1.5
kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya.
Habari hiyo njema imetolewa na kuthibitishwa na Mbunge wa
jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula wakati wa kikao cha baraza la robo ya pili la
madiwani lililofanyika mapema leo katika
Ofisi ya Halmashauri hiyo.
“Upatikanaji wa hospitali itakuwa ni ukombozi mkubwa sana
kwa wananchi wa Mkalama ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma muhimu na
za msingi za matibabu” Alisema Mhe.
Kiula.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
Mhandisi Godfrey Sanga amesema hospitali hiyo itajengwa kwa mtindo wa ghorofa
na tayari eneo itakapojengwa hospitali hiyo limeshatengwa na miundombinu ya
barabara kuelekea kwenye hospitali hiyo tayari imeshawekwa.
Akizungumzia jambo hilo kabla ya kufunga baraza la leo,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega amempongeza
mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula kwa ushirikiano mkubwa alioutoa katika
kipindi chote cha ufuatiliaji wa kuhakikisha fedha hizo zinatengwa.
“Pia ingawa wanasema beki hasifiwi, nitumie fursa hii
kukupongeza sana Mkurugenzi Mtendaji kwa utendaji wako mzuri uliosaidia jambo
hili kufanyika kwa sababu pamoja na sifa nzuri zinazokuja kwetu wanasiasa bado
ukweli unabaki kuwa nyie watendaji ndio wafanikishaji wa haya mambo kwa kiasi
kikubwa sana” Alimalizia Mhe. Mkwega.
Uidhinishwaji wa fedha za ujenzi wa hospitali ya Wilaya
inakuwa ni muendelezo wa habari njema katika sekta ya Afya Wilayani Mkalama baada ya siku kadhaa zilizopita kupokea vifaa
tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300 na serikali kutoa zaidi ya
shilingi milioni 400 za Uboreshaji wa kituo cha Afya cha Kinyambuli ambao upo
katika hatua za mwisho kukamilika.
MASWALI
NA MAJIBU YA BARAZA LA MADIWANI LILILOFANYIKA LEO MEI 08, 2018.
Swali
la 1. Mhe. Amri Gyunda (kata ya Msingi): Ni
lini Mbwa wanaozurula mitaani Wilayani Mkalama watawekewa utaratibu mzuri ili
wasiendelee kuleta madhara kwa wananchi?
Jibu:
Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Mbwa wote wanapaswa kuwekwa
katika mazingira mazuri na kufungwa na wamiliki wao lakini kutokana na hoja
yako Mhe. Amri, tutaanza kuwachukulia hatua wamiliki wote wanaoacha mbwa wao
wazurule ovyo mitaani.
Swali
la 2. Mhe.
Eunick Kalaila (Viti maalum Kinyangiri): Ni lini huduma ya baraza la
ardhi la Wilaya itaanza kutolewa Wilayani Mkalama?
Jibu: Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Taratibu
zimefanyika na wahusika walifika hapa Wilayani kwa ajili ya kukagua jengo
lililopendekezwa kufanyia baraza hilo hivyo tunachosubiri hivi sasa ni mrejesho
wa ukaguzi wao kama wameridhika na jengo hilo au la.
Swali
la 3. Mhe.
Bilal Msengi (kata ya Tumuli): Ni
lini jina la jimbo la Iramba Mashariki litabadilishwa na kuitwa jimbo la
Mkalama?
Jibu: Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Suala
la kubadilisha majina ya majimbo lipo chini ya Tume ya Uchaguzi lakini tayari
tulishawaandikia na tunachosubiri hivi sasa ni majibu kutoka kwao.
Jibu
la Nyongeza- Mhe. James Mkwega (Mwenyekiti wa Hw)- Waheshimiwa
madiwani mimi nadhani jina Iramba Mashariki lingebaki kuwa hivyo kwa sababu
tukibadilisha jina tutapoteza asili yetu na ikumbukwe jina hili linamaanisha sisi
ni watu wa Iramba.
Swali
la Nyongeza. Mhe.
Bilal Msengi (kata ya Tumuli: Kuna mpango gani wa kutenga
maeneo maalum kwa ajili ya watu jamii ya wahadzabe ili waweze kufanya shughuli
zao za maendeleo?
Jibu: Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Ni
kweli jamii ya wahadzabe ni watu maalum sana na ni moja ya alama inayotutangaza
vizuri nje ya hapa lakini kutokana na mpango wa kukabiliana na uharibifu wa
Mazingira, mipango inafanyika ili kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya wahadzabe
kufanya shughuli zao.
Jibu
la Nyongeza- Mhe. Allan Kiula (MB)- Madiwani wote tunapaswa kuwa
wasimamizi wa matumizi bora ya ardhi na maeneo hivyo ni wajibu wetukukaa na
kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kila kata inakuwa na mpango wa matumizi
bora ya Ardhi.
Swali
la 4. Mhe.
Omary Nzia (kata ya Miganga): Ni kwa nini Maafisa watendaji
wa wa vijiji wanalipwa nusu ya malipo wanayostahili wakati wa kustaafu?
Jibu:
Khashim Lugome (Afisa Utumishi) – Hakuna afisa Mtendaji
anayelipwa nusu ya mafao yake kwa sababu wote wanalipwa kutokana na mchango
waliochangia na pia wamekidhi vigezo vya msingi kwa kuchangia miezi 180 ya
utumishi mfululizo.
Kama mtumishi yoyote aliajiriwa na Halmashauri na kulipwa
mshahara wake wote na Halmashauri bila kukatwa makato yoyote kisha akaajiriwa na
kwa mkataba wa kudumu na serikali ni wazi hatopata mafao ya kipindi alichokuwa
na mkataba wa muda kwa sababu hakuwa akikatwa.
Swali
la 5. Mhe.
Abiba Omary (kata ya Kinampundu viti maalum): Eneo
lililotengwa hapo awali kwa ajili ya matumizi ya kujenga uwanja wa mpira wa
miguu limebadilishwa matumizi na kuwa eneo la Soko, je lipo eneo lililotengwa
kwa ajili ya Uwanja?
Jibu: Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Ndio
lipo eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu katika
kijiji cha Maziliga.
Binafsi sioni sababu ya jina la iramba mshariki kubadilishwa Ni jina lenye utambulisho mzuri...pia Ni nembo yetu sisi wanyiramba wote.
ReplyDeletePia ni vema mkurugenzi,ashirikiane vema na tanesco au REA ili kufikisha umeme katika vijiji na kuhimiza kila kaya kujinga na matumiz ya nishati hiyo.