Thursday, 12 July 2018

Uwanja wa kisasa kujengwa Mkalama

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa katika sehemu ya watu mashuhuri ''VIP''

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa kwa muonekano wa juu

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa kwa muonekano wa mbele

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa kwa muonekano wa pembeni




Habari Njema na kubwa kwako Mwananchi wa Wilaya ya Mkalama na Tanzania kwa ujumla  ni kwamba Wilaya ya Mkalama imeanza mchakato wa Ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu utakapokuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 45,000.

Uwanja huo bora kabisa na wa kisasa unaotarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.6 unajengwa katika kijiji cha Maziliga na tayari eneo hilo limeshasafishwa huku hatua ya kulisawazisha au kufanya ‘’levelling’’ kama inayojulikana kitaalam ikitarajiwa kufanyika Wiki ijayo.

Mbali na Mpira wa Miguu, uwanja huo utakuwa na viwanja vya ndani vya michezo ya Mpira wa Kikapu, Mpira wa ikono, Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu na sehemu ya Mashindano ya riadha.

Ujenzi huo unaoratibiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Mkalama chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Mhandisi Lameck Itungi  unatarajiwa kukamilika Julai 2019 ambapo zaidi ya matofali 5000 kati ya 27,000 yanayohitajika kwa ajili ya ujenzi wa Ukuta wa Uwanja huo yameshafyatuliwa.

Kwa Mujibu wa Mhe. Itungi jumla ya mali zinazokadiriwa kuwa na  thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 800 zimeahidiwa kutolewa  na  wadau mbalimbali ambapo kiasi kingine cha Fedha kinatarajiwa kukusanywa katika Harambee itakayofanyika septemba 9 mwaka huu.

“Mgeni rasmi katika harambee hiyo anatarajiwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson hivyo nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama na Watanzania kwa ujumla mjitokeze kuunga Mkono jitihada hizi za dhati kwa ajili ya kuendeleza sekta ya Michezo Mkalama na Tanzania kwa ujumla” Alisihi Mhe. Itungi.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA