Tuesday 19 February 2019

Makamu wa Rais azindua Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya Mkalama

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akisikiliza maelezo ya Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Iguguno (hayupo pichani)  kuhusu muundo na matumizi ya bweni lililojengwa katika shule ya sekondari ya Iguguno wakati wa ziara yake Wilayani Mkalama mapema leo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Mkalama Mhe. Lameck Itungi muda mfupi baada ya kufika katika shule ya sekondari ya Iguguno wakati wa ziara yake Wilayani Mkalama mapema leo.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso akiwasalimia wananchi wa Iguguno mapema leo alipokuwa  kwenye ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan iliyoanzia hapo Iguguno na kuishia Makao Makuu ya Wilaya hiyo yaliyopo Nduguti.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso akikusanya fedha kutoka kwa viongozi mbalimbali kwa ajili ya kumkabidhi mwanafunzi Lailat Ramadhani (19) anayesoma kidato cha kwanza shule ya sekondari Iguguno ikiwa ni ishara ya kuunga mkono jitihada zake za masomo  alizozionesha licha ya kuwa na changamoto ya kuwa na umbo dogo kuliko wanafunzi wote shuleni hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika viwanja vya shule ya sekondari Iguguno mapema leo wakati wa ziara yake aliyoifanya Wilayani Mkalama.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika daraja la Mto Sibiti mapema leo wakati wa ziara yake aliyoifanya Wilayani Mkalama.

Pichani ni muonekano wa daraja la Sibiti kwa hivi sasa ambapo Meneja wa TANROAD mkoa wa Singida Mhandisi Matari Masige amemuahidi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa ifikapo Machi 15 daraja hilo litakuwa limekamilika kwa asilimia 100 na litakuwa tayari kuzinduliwa.

Meneja wa TANROAD mkoa wa Singida Mhandisi Matari Masige akimpa maelekezo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan juu ya namna daraja la Mto Sibiti lilivyojengwa wakati wa ziara yake aliyoifanya leo Wilayani Mkalama.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi (kushoto) akimuelekeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusu mpango wa ujenzi wa vivuko vya kupitishia mifugo vitakavyoweka kando ya daraja la mto Sibiti mapema leo baada ya kiongozi huyo kuzuru darajani hapo.

Naibu waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa (kulia) akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Rais wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania  juu ya mambo yaliyofanywa na Wizara yake Wilayani Mkalama mapema leo katika daraja la Mto Sibiti.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika eneo la Mto Sibiti mapema leo wakati wa ziara yake Wilayani Mkalama.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mkoa na Taifa ambapo kutoka kushoto ni Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa na kutoka kulia ni Meneja wa TANROAD mkoa wa Singida Mhandisi Matari Masige na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (katikati) akimpa maelezo Makamu wa Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania wakati wakielekea kukata utepe na kuzindua rasmi Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Kushoto kwa Mkuu wa Wilaya ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga  na kulia kwa Makamu wa Rais ni Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Paskazia  Tibalinda.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga (kulia) akitoa maelezo juu ya gharama na muda uliotumika kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri hiyo mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan muda mfupi kabla hajakata utepe kuashiria uzinduzi wa ofisi hiyo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwaongoza viongozi mbalimbali kukata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mapema leo wakati wa ziara yake Wilayani hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) na Mkuu wa Mkoa  wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi (kushoto)  wakifungua kitambaa cha kibao cha uzinduzi wa Ofisi ya Halmashauri kama ishara ya uzinduzi rasmi wa Ofisi hiyo mapema leo wakati wa ziara yake Wilayani Mkalama.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipiga makofi muda mfupi baada ya kufungua kitambaa cha kibao cha uzinduzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama tukio alilolifanya leo wakati wa ziara yake Wilayani hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwenye viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mapema leo mchana wakati wa ziara yake wilayani hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati wakielekea jukwaani tayari kabisa kwa ajili ya kuzungumza na wananchi waliojitokeza kwenye viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akizungumza machache muda mfupi kabla ya kumkabribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aweze kutoa hotuba yake kwa wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwenye viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama





Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mkalama wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya leo Wilayani hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakati akihitimisha ziara yake Wilayani hapo leo.

Wanafunzi wa kidato cha tano wa Shule ya sekondari Iguguno wakionesha picha za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli (kushoto) na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan muda mfupi baada ya Makamu huyo wa Rais kuwasili katika viwanja vya Shule hiyo mapema leo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na mwanafunzi Laylat Ramadhani (19) muda mfupi kabla hajamkabidhi kiasi cha fedha kitakachomsaidia katika masomo yake ikiwa ni ishara ya kutambua juhudi zilizooneshwa na mwanafunzi huyo licha ya kukabiliwa na changamoto ya kuwa na umbile dogo kuliko wanafunzi wote shuleni hapo.



Muda mfupi uliopita Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewahutubia wananchi wa Wilaya ya Mkalama katika Mkutano uliofanyika kwenye moja ya viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mhe. Samia ambaye aliambatana katika ziara yake aliambatana na mawaziri watatu, alianza ziara hiyo kwa kukagua miundombinu ya shule ya sekondari Iguguno kabla ya kwenda kuangalia hatua ya ujenzi wa daraja la mto Sibiti na alihitimisha ziara hiyo muda mfupi uliopita kwa kuzindua Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na kuzungumza na wananchi.

Akizungumza kabla ya hotuba ya Mhe. Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa alisema kuwa dhamira ya serikali kwa sasa ni kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Mkalama hawapati changamoto yoyote kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara na ndio maana kwa kushirikiana na Wakala wa barabara wa Taifa (TANROADS) itahakikisha kila upande unaunganishwa kwa kiwango cha lami.

“Hivi karibuni tutaenda kujenga daraja la chuma pale kijiji cha Msingi na wakati wowote fedha ikipatikana kipaumbele chetu kitakuwa ni kuweka lami barabara inayotoka Iguguno hadi daraja la Sibiti huku tukiunganisha pia barabara ya lami kutoka kijiji cha Gumanga hadi Msingi” Alisisitiza Mhe. Kwandikwa.

Kwa upande wake Naibu waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso alisema kuwa mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 10 zimeshatumika kwa miradi ya maji ya Wilaya ya Mkalama ikiwa ni pamoja na mradi wa maji wa Kikhonda, Ipuli, Iguguno, Nyahaa na Nduguti ambapo alisisitiza kuwa fedha za miradi hiyo yote zilishalipwa na wananchi wameanza kupata huduma ya maji kwa miradi iliyokamilika.

“Lakini Mhe. Makamu wa Rais ni lazima niseme ukweli kuwa mradi wa maji wa Nyahaa umejaa ufisadi mkubwa sana kwa sababu serikali imelipa zaidi ya shilingi milioni 900 lakini mradi huo haujakamilika mpaka sasa ingawa mkandarasi alishalipwa hela zote na cha kusikitisha zaidi mhandisi aliyekuwa anasimamia mradi huo amehamishiwa Gairo” Alitoa angalizo Mhe. Aweso

Kufuatia hali hiyo Mhe. Aweso alimuomba Makamu wa Rais kumuagiza katibu Mkuu wa Wizara ya Maji amuandikie barua ya wito mhandisi huyo ili afike kwenye kikao cha majumuisho ya Ziara keshokutwa na kutoa majibu ya kina kuhusu suala hilo ombi ambalo Mhe. Makamu wa Rais alilikubali.

Katika hotuba yake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwapongeza viongozi wote wa Wilaya ya Mkalama kwa kukamilisha ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ambapo aliwataka kuendelea kufanya hivyo katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya na miradi mingine ya serikali.

“Lakini lazima niseme ukweli kuwa kitendo cha kusimamishwa pale Ibaga kimeonesha wazi kuwa kuna ukosefu wa ushirikiano baina ya wananchi kwa sababu inaonekana kuna baadhi ya watu wanapangwa kusimama barabarani na mabango kwenye misafara ya viongozi jambo ambalo si zuri na linachafua taswira nzuri mliyoijenga wananchi wa Mkalama” Alisisitiza Mhe. Samia.

Mhe. Samia alihitimisha hotuba yake kwa kuwasihi wananchi wa Mkalama kutunza mazingira hasa katika kipindi hiki cha Masika ili vyanzo vya maji vilivyopo visikauke na kusababisha ukame wakati wa Kiangazi.

“Mwisho ninawaomba Wananchi wa Mkalama na Mkoa wa Singida kwa ujumla, tujihadhari sana na ugonjwa wa Ukimwi kwa sababu japo sijapata takwimu ya Wilaya lakini takwimu ya Mkoa si nzuri hata kidogo hivyo tujilinde dhidi ya Ugonjwa huu hatari ndugu zangu” Alimalizia Mhe. Samia.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA