Monday 14 May 2018

Singida haitakuwa ya mwisho tena- Nchimbi

PICHA TATU CHINI: MAANDAMANO YA AMANI YA WANAFUNZI HUKU WAKIWASILISHA KAULI MBIU MBALIMBALI KUHUSU ELIMU.






Afisa Mawasiliano na Mahusiano wa Shirika la Twaweza bw. Greyson Mgoy akimueleza kazi za shirika hilo Mgeni rasmi wa maadhimisho ya juma la elimu Mhe. Daktari Rehema Nchimbi 

Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula akizungumza machache wakati wa maadhimisho ya Juma la Elimu yaliyofunguliwa kitaifa leo Wilayani Mkalama.

Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye pia ndiye alikuwa Mgeni rasmi wa maadhimisho ya juma la Elimu Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akitoa hotuba wakati wa maadhimisho ya Juma la Elimu yaliyofunguliwa kitaifa leo Wilayani Mkalama.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga muda fupi baada ya kuwasili katika ofisi za halmashauri hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akiteta jambo naWaziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI)  Mhe. Selemani Jafo muda mfupi baada ya Mhe. Jafo kuwasili katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Wilaya ya Mkalama leo imeingia katika moja ya rekodi za Kitaifa baada ya kufungua rasmi maadhimisho ya juma la Elimu kwa mwaka huu.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya kitaifa mwaka huu alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi ambapo pamoja na mambo mengine alitumia hotuba yake kusisitiza Mtandao wa Elimu kutangaza mambo mazuri yanayofanywa na serikali katika sekta hiyo.

“Kauli mbiu yenu ya uwajibikaji wa pamoja katika kuinua elimu nchini inapaswa kutekelezwa kwa vitendo na jamii yote ya Mkalama kwa sababu sioni sababu ya wazazi wa wanafunzi wa Mkalama kushindwa kuchangia chakula cha watoto wao shuleni wakati nina ushahidi kuwa wazazi hawa ni wakulima wazuri” Aliongeza  Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi aliwataka wananchi watumie vizuri mbegu za pamba na korosho walizopewa na serikali bila malipo yoyote kuhakikisha wanapata mavuno mengi yatakayowasaidia kuchangia elimu.

“Kuanzia sasa ninaagiza shule zote za sekondari hapa Singida ni lazima ziwe na mabwawa ya kufuga samaki ambapo mbali na kupata chakula kupitia mabwawa hayo pia kitakuwa ni chanzo kizuri cha mapato kwa kila shule kwa sababu soko la samaki ni kubwa sana hasa Mkoa jirani wa Dodoma, mtapata, hili sio ombi ni lazima! Alisisitiza Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi aliwaagiza wakurugenzi wote wa Halmashauri zilizopo Mkoani Singida kuhakikisha wanampa taarifa za utekelezaji wa agizo hilo kila ifikapo mwisho wa Mwezi  na taarifa hizo  apatiwe moja kwa moja katika ofisi yake.

“Tunawashukuru sana TenMet kwa kutuandalia juma hili na tunawaahidi haya mema yote mliyotupa tutayarudisha kwa mema pia na kwa mchango Mkubwa ambao serikali ya awamu ya tano imetoa katika Elimu ya Mkalama hatuwezi kubaki nyuma tena na safari hii tunataka kama tukiwa wa mwisho basi tuwe wa mwisho kwa ufaulu wa asilimia 90” Alimalizia Mhe. Nchimbi.

Wakati huo huo  Wilaya ya Mkalama ilipata ugeni wa ziara ya muda mfupi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo ambaye alifika kwa ajili ya kukagua thamani ya fedha kulingana na ubora wa jengo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ambapo aliridhika na kazi iliyofanyika  kwa awamu ya kwanza na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Gofrey Sanga kuhakikisha viwango hivyo vya ubora vinazingatiwa katika ujenzi wa awamu ya pili ya Ofisi ya hiyo.

“Mkalama ni moja ya Wilaya change hivyo inahitaji kupewa kipaumbele katika miradi mbalimbali na nikuhakikishie Mhe. Mkuu wa Mkoa, Wizara yangu itahakikisha Mkoa wa Singida kwa ujumla unasonga mbele” Aliongeza Mhe. Jafo.

Mhe. Jafo pia alisema kuwa mbali na kujenga vituo viwili vya Afya vya Kisasa ambavyo ni Kinyambuli na Mkalama, Kwa Mkoa wa Singida serikali ya awamu ya tano imetenga fedha za ujenzi wa hospitali mbili za Wilaya ambazo zitajengwa katika Wilaya ya Mkalama na Singida vijijini.

“Naomba nitumie fursa hii kukutamkia wazi Mkuu wa Mkoa na wananchi wote wa Singida vijijini kwa ujumla kuwa hospitali ya Wilaya Singida Vijijini itajengwa Ilongelo na sitaki mtu yoyote ahangaike kuja ofisini kwangu kujadili juu ya hilo, mimi nimeshalimaliza kwa sababu nachoangalia mimi ni kupeleka hospitali sehemu ambayo nina uhakika wananchi wengi zaidi watapata huduma na sio kundi la watu wachache wanaojaribu kuangalia maslahi yao kisiasa” Alimalizia Mhe. Jafo.





No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA