Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akitoa hotuba katika uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika katika zahanati ya Nduguti leo asubuhi. |
Diwani wa kata ya Nduguti Mhe. Loth Dia akizungumza katika uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika katika zahanati ya Nduguti leo asubuhi. |
“Jamii iliyopata chanjo ni jamii yenye Afya, Timiza wajibu
wako” Ni kauli mbiu iliyobeba kampeni ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi
kwa wasichana wenye umri wa Miaka 14 iliyozinduliwa rasmi leo Wilayani Mkalama.
Uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na wananchi, viongozi
mbalimbali wa dini na jamii, wanafunzi wa sekondari na wataalam mbalimbali
kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama
Mhe. Mhandisi Jackson Masaka.
Katika uzinduzi huo Mhe. Masaka aliwasisitiza wananchi
kuwapeleka watoto wao wa kike wenye umri wa miaka 14 ili wakapate kinga ya
saratani hiyo ambayo kila mwaka husababisha vifo vya wanawake 4216 hapa nchini.
“hii ina maana kila siku wastani wa wanawake 11 hufariki
dunia hapa nchini kutokana na saratani hii takwimu ambayo ni kubwa sana hivyo
wananchi tuhakikishe tunawapa mabinti zetu chanjo hii ili kushusha na
kutokomeza kabisa ugonjwa huu kwa
akinamama” Aliongeza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka alisisitiza kuwa wananchi wakipata chanjo
itawapunguzia gharama za matibabu kwa sababu suala hilo hivi sasa limekuwa
mzigo mkubwa sana kwa mwananchi wa kawaida.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe.
Loth Dia aliwataka wananchi wa Wilaya ya Mkalama kuondoa dhana potofu kuwa
chanjo huongeza zaidi maradhi na kuwataka kujitokeza kwa wingi katika vituo vya
kutolea chanjo hiyo.
“Siku za nyuma wanawake wengi walipoteza maisha kwa sababu
hakukuwa na chanjo ya Ugonjwa huu hivyo tunaishukuru serikali kwa kuokoa maisha
ya kizazi kilichopo kutokana na ugonjwa huu wa saratani ya Mlango wa kizazi na
wananchi tuiunge Mkono kwa kuhakikisha watoto wetu wanajitokeza kwa wingi
kwenda kupatiwa chanjo hii” Alisema Mhe. Dia.
Kwa mwaka 2018 Wilaya ya Mkalama imelenga kutoa chanjo kwa
wasichana 2783 ambao walizaliwa mwaka 2004.
No comments:
Post a Comment