PICHA 10 CHINI: Ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka aliyoifanya leo kwa kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya Nanenane kanda ya kati yanayofanyika jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka leo
alikuwa mgeni rasmi katika manesho ya 22 ya sikukuu ya Wakulima na Wafugaji
(nanenane) kanda ya kati ambapo alitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika
viwanja vya maonesho hayo jijini Dodoma.
Ziara hiyo ya Mhe. Masaka ilianzia katika banda la Ofisi
ya Rais-TAMISEMI ambapo aliishauri wizara hiyo kufanya matumizi mbadala ya
jengo lao walilolijenga kwa ajili ya maonesho ya Nane nane badala ya kuliacha wazi
huku likisubiri siku ambayo maadhimisho ya kitaifa yatafanyikia jijini Dodoma.
“Kuna taasisi mbalimbali zinapenda kushiriki maonesho haya
lakini zimekosa maeneo ya kuweka bidhaa zao, mnaweza kuwapa jengo hilo au
mnaweza hata kufikiria kuweka maonesho ya utamaduni ili wananchi waweze
kufahamu kwa kina tamaduni za kitanzania kwa sababu kuliacha bila matumizi
yoyote kama mnavyofanya hivi sasa ni kupoteza fedha za serikali ilizowekeza
wakati wa kulijenga” Alisisitiza Mhe. Masaka.
Baada ya kutoka katika banda la TAMISEMI Mhe. Masaka
alielekea katika banda la wataalam wa ufugaji wa kisasa wa kuku wanaojulikana
kama ‘’Silverland’’ ambapo akiwa hapo aliwashauri wataalam hao kuhakikisha
elimu inayohusu ufugaji wa kuku ifike mpaka kwa wafugaji wadogo badala ya
kuishia kwenye maonesho ya Nanenane.
Mhe. Masaka ambaye katika ziara hiyo aliongozana na
viongozi wengine waandamizi wa Mkoa wa Dodoma na Wizara ya Kilimo alifika pia katika banda la Mamlaka ya Maendeleo ya
biashara (TANTRADE) ambapo akiwa hapo
aliisisitiza mamlaka hiyo kuhakikisha inatoa matangazo kwa wakulima juu ya
masoko ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha.
“Sasa hivi wakulima wanalima lakini wengi hawajui masoko
ya mazao wanayolima yako wapi matokeo yake wanajikuta wanalima kilimo kisicho
na tija hivyo ninawashauri mtengeneze utaratibu mzuri wa kuwajulisha wakulima
kuhusu aina ya mazao yanayohitajika sokoni na mahali yanapohitajika mazao hayo’’
Aliongeza Mhe. Masaka.
Mbali na mabanda hayo Mhe. Masaka pia alitembelea Mamlaka
ya Uhamiaji, benki ya CRDB, halmashauri za wilaya za Mkalama na Chamwino,
AGRICOM na Polymachinery, Sido na Benki kuu ya Tanzania (BOT).
No comments:
Post a Comment