Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mheshimiwa Nape Nnauye ( Aliyesimama) akizungumza na wadau wa sekta za wizara yake kwa mkoa wa Singida katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida katika kikao kilichofanyika jana jioni.
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo mheshimiwa
Nape Moses Nnauye jana alikutana na
wadau wa sekta za wizara yake katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa
ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Singida.
Katika kikao hicho Nape alizungumzia kila sekta inayohusiana
na wizara yake kwa kina ambapo kwa upande wa sekta ya habari msisitizo mkubwa
ulikuwa ni halmashauri ambazo hazina maafisa habari zitenge bajeti na kuajiri wataalam hao ili
kutengeneza daraja kati ya vyombo vya habari na serikali.
Pia mheshimiwa Nape aliagiza na kusisitiza wakurugenzi wa
halmashauri zote, wakuu wa idara na viongozi mbalimbali wa Wilaya wawaruhusu
maafisa habari kuingia kwenye vikao vyote vya maamuzi ili waweze kuwa na taarifa sahihi na za kutosha pindi
wanapokutana na vyombo vya habari.
“Tanzania ina magazeti 15 yanayotoka kila siku na magazeti
haya habari zake kubwa ni zile zinazohusiana na serikali, maafisa habari
wasipoingia kwenye vikao vya maamuzi watawakimbia waandishi wa habari na
waandishi wa habari wasipopata habari wanaenda kuandika habari za uongo au
zisizo na ubora” Aliongeza Nape.
Akisisitiza juu ya hilo alisema kuna kipindi Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kilikuwa kina sifa mbaya sana kwa jamii hivyo akawaomba
viongozi wakuu wa chama awe anaingia kwenye vikao vyote vya maamuzi hata vile
ambavyo vitashirikisha watu watatu tu.
“Baada ya kuanza kuingia kwenye vikao vya chama, kwanza mi
nikawa ndo msemaji mkuu wa chama na nikaanza kutoa taarifa sahihi kwa waandishi
wa habari katika kila kilichokuwa kinaendelea ndani ya chama,na hatimaye
heshima na hadhi ya chama ikarejea” Alisema Nape.
Kwa upande wa Michezo alisisitiza kufanyika kwa mchakato
wa kutafuta viongozi imara katika ngazi za Wilaya na mikoa ili kuepuka viongozi
wanaowekwa na viongozi wakuu wa taifa kwa ajili ya kuwapigia kura tu kwenye
vikao vya kamati kuu.
“Kuna sehemu nilienda nikauliza nyie kiongozi wenu nani,
wakasema kuna bwana mmoja alikuja hapa akatupa pesa tukampigia kura akaondoka
zake, Hiyo ni hatari sana na jambo hili ni lazima likomeshwe” Alisisitiza Nape.
Kwa upande wa Sanaa na utamaduni, Mheshimiwa Nape
alisisitiza kujengwa kwa vituo vya maonesho ya kumbukumbu katika kila mkoa ili
kurahisisha shughuli za utalii na kukuza uchumi wa mkoa husika.
“Hapa Singida kuna vivutio vingi sana vya utalii lakini
hakuna sehemu maalum ambayo hata mtu akitaka kufahamu historia mbalimbali ya
watu na vitu vya kale vilivyopo, ni lazima tuweke vituo ambavyo tutakusanya
vivutio vyote vya mkoa na kuviweka sehemu moja” Alimalizia Nape.
|
Wakati mwingine tunauza sura hata sisi... ilitakiwa unichukue nikupige picha na Mh. Waziri kaka....
ReplyDelete