Tuesday 19 February 2019

Makamu wa Rais azindua Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya Mkalama

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akisikiliza maelezo ya Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Iguguno (hayupo pichani)  kuhusu muundo na matumizi ya bweni lililojengwa katika shule ya sekondari ya Iguguno wakati wa ziara yake Wilayani Mkalama mapema leo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Mkalama Mhe. Lameck Itungi muda mfupi baada ya kufika katika shule ya sekondari ya Iguguno wakati wa ziara yake Wilayani Mkalama mapema leo.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso akiwasalimia wananchi wa Iguguno mapema leo alipokuwa  kwenye ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan iliyoanzia hapo Iguguno na kuishia Makao Makuu ya Wilaya hiyo yaliyopo Nduguti.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso akikusanya fedha kutoka kwa viongozi mbalimbali kwa ajili ya kumkabidhi mwanafunzi Lailat Ramadhani (19) anayesoma kidato cha kwanza shule ya sekondari Iguguno ikiwa ni ishara ya kuunga mkono jitihada zake za masomo  alizozionesha licha ya kuwa na changamoto ya kuwa na umbo dogo kuliko wanafunzi wote shuleni hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika viwanja vya shule ya sekondari Iguguno mapema leo wakati wa ziara yake aliyoifanya Wilayani Mkalama.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika daraja la Mto Sibiti mapema leo wakati wa ziara yake aliyoifanya Wilayani Mkalama.

Pichani ni muonekano wa daraja la Sibiti kwa hivi sasa ambapo Meneja wa TANROAD mkoa wa Singida Mhandisi Matari Masige amemuahidi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa ifikapo Machi 15 daraja hilo litakuwa limekamilika kwa asilimia 100 na litakuwa tayari kuzinduliwa.

Meneja wa TANROAD mkoa wa Singida Mhandisi Matari Masige akimpa maelekezo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan juu ya namna daraja la Mto Sibiti lilivyojengwa wakati wa ziara yake aliyoifanya leo Wilayani Mkalama.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi (kushoto) akimuelekeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusu mpango wa ujenzi wa vivuko vya kupitishia mifugo vitakavyoweka kando ya daraja la mto Sibiti mapema leo baada ya kiongozi huyo kuzuru darajani hapo.

Naibu waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa (kulia) akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Rais wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania  juu ya mambo yaliyofanywa na Wizara yake Wilayani Mkalama mapema leo katika daraja la Mto Sibiti.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika eneo la Mto Sibiti mapema leo wakati wa ziara yake Wilayani Mkalama.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mkoa na Taifa ambapo kutoka kushoto ni Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa na kutoka kulia ni Meneja wa TANROAD mkoa wa Singida Mhandisi Matari Masige na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (katikati) akimpa maelezo Makamu wa Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania wakati wakielekea kukata utepe na kuzindua rasmi Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Kushoto kwa Mkuu wa Wilaya ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga  na kulia kwa Makamu wa Rais ni Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Paskazia  Tibalinda.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga (kulia) akitoa maelezo juu ya gharama na muda uliotumika kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri hiyo mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan muda mfupi kabla hajakata utepe kuashiria uzinduzi wa ofisi hiyo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwaongoza viongozi mbalimbali kukata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mapema leo wakati wa ziara yake Wilayani hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) na Mkuu wa Mkoa  wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi (kushoto)  wakifungua kitambaa cha kibao cha uzinduzi wa Ofisi ya Halmashauri kama ishara ya uzinduzi rasmi wa Ofisi hiyo mapema leo wakati wa ziara yake Wilayani Mkalama.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipiga makofi muda mfupi baada ya kufungua kitambaa cha kibao cha uzinduzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama tukio alilolifanya leo wakati wa ziara yake Wilayani hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwenye viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mapema leo mchana wakati wa ziara yake wilayani hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati wakielekea jukwaani tayari kabisa kwa ajili ya kuzungumza na wananchi waliojitokeza kwenye viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akizungumza machache muda mfupi kabla ya kumkabribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aweze kutoa hotuba yake kwa wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwenye viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama





Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mkalama wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya leo Wilayani hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakati akihitimisha ziara yake Wilayani hapo leo.

Wanafunzi wa kidato cha tano wa Shule ya sekondari Iguguno wakionesha picha za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli (kushoto) na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan muda mfupi baada ya Makamu huyo wa Rais kuwasili katika viwanja vya Shule hiyo mapema leo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na mwanafunzi Laylat Ramadhani (19) muda mfupi kabla hajamkabidhi kiasi cha fedha kitakachomsaidia katika masomo yake ikiwa ni ishara ya kutambua juhudi zilizooneshwa na mwanafunzi huyo licha ya kukabiliwa na changamoto ya kuwa na umbile dogo kuliko wanafunzi wote shuleni hapo.



Muda mfupi uliopita Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewahutubia wananchi wa Wilaya ya Mkalama katika Mkutano uliofanyika kwenye moja ya viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mhe. Samia ambaye aliambatana katika ziara yake aliambatana na mawaziri watatu, alianza ziara hiyo kwa kukagua miundombinu ya shule ya sekondari Iguguno kabla ya kwenda kuangalia hatua ya ujenzi wa daraja la mto Sibiti na alihitimisha ziara hiyo muda mfupi uliopita kwa kuzindua Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na kuzungumza na wananchi.

Akizungumza kabla ya hotuba ya Mhe. Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa alisema kuwa dhamira ya serikali kwa sasa ni kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Mkalama hawapati changamoto yoyote kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara na ndio maana kwa kushirikiana na Wakala wa barabara wa Taifa (TANROADS) itahakikisha kila upande unaunganishwa kwa kiwango cha lami.

“Hivi karibuni tutaenda kujenga daraja la chuma pale kijiji cha Msingi na wakati wowote fedha ikipatikana kipaumbele chetu kitakuwa ni kuweka lami barabara inayotoka Iguguno hadi daraja la Sibiti huku tukiunganisha pia barabara ya lami kutoka kijiji cha Gumanga hadi Msingi” Alisisitiza Mhe. Kwandikwa.

Kwa upande wake Naibu waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso alisema kuwa mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 10 zimeshatumika kwa miradi ya maji ya Wilaya ya Mkalama ikiwa ni pamoja na mradi wa maji wa Kikhonda, Ipuli, Iguguno, Nyahaa na Nduguti ambapo alisisitiza kuwa fedha za miradi hiyo yote zilishalipwa na wananchi wameanza kupata huduma ya maji kwa miradi iliyokamilika.

“Lakini Mhe. Makamu wa Rais ni lazima niseme ukweli kuwa mradi wa maji wa Nyahaa umejaa ufisadi mkubwa sana kwa sababu serikali imelipa zaidi ya shilingi milioni 900 lakini mradi huo haujakamilika mpaka sasa ingawa mkandarasi alishalipwa hela zote na cha kusikitisha zaidi mhandisi aliyekuwa anasimamia mradi huo amehamishiwa Gairo” Alitoa angalizo Mhe. Aweso

Kufuatia hali hiyo Mhe. Aweso alimuomba Makamu wa Rais kumuagiza katibu Mkuu wa Wizara ya Maji amuandikie barua ya wito mhandisi huyo ili afike kwenye kikao cha majumuisho ya Ziara keshokutwa na kutoa majibu ya kina kuhusu suala hilo ombi ambalo Mhe. Makamu wa Rais alilikubali.

Katika hotuba yake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwapongeza viongozi wote wa Wilaya ya Mkalama kwa kukamilisha ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ambapo aliwataka kuendelea kufanya hivyo katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya na miradi mingine ya serikali.

“Lakini lazima niseme ukweli kuwa kitendo cha kusimamishwa pale Ibaga kimeonesha wazi kuwa kuna ukosefu wa ushirikiano baina ya wananchi kwa sababu inaonekana kuna baadhi ya watu wanapangwa kusimama barabarani na mabango kwenye misafara ya viongozi jambo ambalo si zuri na linachafua taswira nzuri mliyoijenga wananchi wa Mkalama” Alisisitiza Mhe. Samia.

Mhe. Samia alihitimisha hotuba yake kwa kuwasihi wananchi wa Mkalama kutunza mazingira hasa katika kipindi hiki cha Masika ili vyanzo vya maji vilivyopo visikauke na kusababisha ukame wakati wa Kiangazi.

“Mwisho ninawaomba Wananchi wa Mkalama na Mkoa wa Singida kwa ujumla, tujihadhari sana na ugonjwa wa Ukimwi kwa sababu japo sijapata takwimu ya Wilaya lakini takwimu ya Mkoa si nzuri hata kidogo hivyo tujilinde dhidi ya Ugonjwa huu hatari ndugu zangu” Alimalizia Mhe. Samia.

Friday 23 November 2018

Kampeni hii ifanyike katika kata zote-DC

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akihutubia umati wa watu waliojitokeza kwenye sherehe za uzinduzi wa kampeni ya Furaha yangu zilizofanyika katika kijiji cha Nkalakala leo.

Muuguzi wa zahanati ya Nduguti Bi. Josephine Makanyaga akitoa maelezo juu ya namna zoezi la damu salama linavyotekelezwa mbele ya mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka (kushoto) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Furaha yangu"uliofanyika katika kijiji cha Nkalakala leo.

Kikundi cha Ngoma kutoka kijiji cha Nkalakala  kikitumbuiza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya "Furaha yangu" leo katika kijiji cha Nkalakala.



“Ninaagiza kampeni hii ifanyike katika kata nyingine zote 16 zilizobakia za Wilaya yaMkalama”

Hilo ni agizo lililotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upimaji wa hiyari wa  virusi vya ukimwi iliyopewa jina la “Furaha Yangu” uliofanyika leo katika kijiji cha Nkalakala ambapo zaidi ya watu 250 walijitokeza kupima.

Katika hotuba yake Mhe. Masaka alimshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwa kuzindua kampeni hiyo kitaifa yenye lengo la kuhamasisha wananchi hasa wanaume kujitokeza kwa wingi katika vituo vya afya kupima kwa hiyari virusi vya ukimwi.

“Kwa Wilaya ya Mkalama suala la kupima afya sio jipya kwetu kwa sababu nimeshuhudia watu wengi sana wakijitokeza kupima afya zao kipindi cha mkesha wa Mwenge na sherehe nyingine huku vipimo mbalimbali vikifanyika ikiwemo shinikizo la damu, Malaria na HIV/VVU” aliongeza Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka aliwasisitiza wananchi wote wa Mkalama kuchukua tahadhari kwa kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya Ukimwi ili kuweza kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo ambayo kwa mkoa wa Singida imeonekana kukua kwa asilimia 0.3 kutoka asilimia 3.3 ya mwaka 2011/2012 hadi asilimia 3.6 ya mwaka 2016/2017.

“Lakini pia ninaomba wananchi msipuuze pindi mnapobanwa na vikohozi visivyoisha kwa sababu huenda ikawa ni dalili ya ugonjwa wa Kifua kikuu kwa hiyo usijikaushe ewe dada na kaka nendeni mkapime na bahati nzuri Wilaya yetu imepata wahisani wa kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi na TB  na kampeni hizi ni msaada mkubwa kwa afya zetu” Aliongeza Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka alihitimisha hotuba yake kwa kuwahimiza wananchi wote kuwashawishi vijana na watoto wao wasome kwa bidii masomo ya sayansi ili waweze kupata nafasi za kusomea uuguzi, ukunga, maabara, udaktari na kozi nyingine za afya kwa sababu wasipofanya hivyo watakuwa na majengo mazuri ya zahanati, vituo vya afya na hospitali lakini hakutakuwa na wataalam wa kuendesha vituo hivyo.

Kampeni ya “Furaha Yangu” ilizinduliwa kitaifa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa mnamo tarehe 16 mwezi juni mwaka huu makao makuu ya nchi jijini Dodoma.


Tuesday 30 October 2018

Ujenzi hospitali ya Wilaya uanze wiki ijayo- Ndugulile

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Daktari Faustine Ndugulile akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kinyambuli mapema leo alipotembelea kituo cha Afya cha Kinyambuli.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Daktari Faustine Ndugulile (katikati)  akitoa agizo la kuanza kwa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Mkalama wakat wa ziara yake aliyoifanya wilayani hapa leo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Daktari Faustine Ndugulile akihitaji ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya ujenzi kutoka kwa Mhandisi wa ujenzi wa wilaya ya Mkalama  Bi. Paskazia Tibalinda (wa pili kutoka kulia) wakati wa ziara yake leo wilayani hapa.

Viongozi mbalimbali wa serikali wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameendelea na ziara za kikazi ndani ya wilaya ya Mkalama ambapo leo ilikuwa ni zamu ya Naibu waziri wa Wizara ya Afya , Maendeleo ya jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Daktari Faustine Ndugulile.

Mhe. Ndugulile aliipongeza wilaya ya Mkalama kwa jitihada za dhati za kuhakikisha wanapanda katika vigezo vya ubora wa utoaji wa huduma za afya au  “Star rating”  kama inavyojulikana kitaalam ambapo mwaka 2016  vituo vyote vilikuwa chini ya nyota 3 hali iliyoashiria hakuna kituo kilichokuwa kimekidhi viwango vya utoaji wa huduma bora.

“Lakini mwaka 2018 asilimia 33.5 ya vituo vilivyopo hapa Mkalama vimepata  nyota 3 au zaidi huku aslimia 66.5 ya vituo vikiwa na nyota 2 na hakuna hata kituo kimoja kisicho na nyota hivyo jambo lililoifanya Wilaya ya Mkalama kuwa ya tatu kwa mkoa wa Singida kwa upande wa utoaji wa huduma bora za Afya, hongereni sana” Alisisitiza Mhe. Ndugulile.

Akiwa katika eneo lililoandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya, Mhe. Ndugulile aliwapongeza wananchi wa kata ya Nduguti kwa kujitolea eneo kwa ajili ya kujenga hospitali ya Wilaya bila fidia yoyote ambapo aliwataka wananchi wa maeneo mengine nchini kuiga mfano huo.

“Kwa sababu tayari mmeshaletewa fedha za awamu ya kwanza na michoro mnayo ninaagiza ujenzi wa hospitali hii ya Wilaya uanze mapema wiki ijayo na kama kuna mtu atasema msubiri michoro mwambieni michoro hiyo aniletee mimi “ntadeal” naye lakini nyinyi anzeni kazi” aliongeza Mhe. Ndugulile.

Mhe. Ndugulile alimalizia ziara yake kwa kutembelea kituo cha afya cha Kinyambuli ambapo alizipongeza kamati zote zilizoshiriki katika ujenzi wa kituo hicho na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kuhakikisha anatumia fedha za mapato ya ndani kumalizia kazi zote zilizobaki za ujenzi wa kituo kufikia mwisho wa mwaka huu ili kuanzia mapema mwakani wananchi waanze kupatiwa huduma katika majengo hayo mapya.

“Lakini pia niwatangazie wananchi wa Kinyambuli na Watanzania wote kuwa hivi sasa tumeanza kudhibiti dawa tunazosambaza kwa kuziwekea alama inayosomeka “MSD GOT” ambayo mbali na kuiweka nje ya maboksi ya dawa pia tumeiweka mpaka ndani kwenye tembe na kwenye bomba za sindano hivyo yoyote atakayeona vifaa tiba na dawa zenye alama hiyo zinauzwa kwenye maduka binafsi ya dawa tafadhali atoe taarifa kwenye mamlaka za Ulinzi na usalama” Aliongeza Mhe. Ndugulile.

Kwa mwaka 2018 serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia zaidi ya shilingi bilioni 5.3 kwa ajili ya ukarabati na uwekaji wa miundombinu ya Afya mkoani Singida ambapo pia imeuongezea Mkoa huo bajeti ya Afya kutoka shilingi bilioni 4 ya mwaka 2017/2018 hadi shilingi bilioni 7.5 kwa mwaka 2018/2019.







Saturday 27 October 2018

Mkalama inapiga hatua-Tulia

Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari Tulia Ackson akizungumza wakati wa harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa wilaya ya Mkalama iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Singida Mhe. Martha Mlata (kushoto) akimkabidhi zawadi ya mboga aina ya ''mnafu'' naibu spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dakatri Tulia Ackson wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu iliyofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri wilaya ya Mkalama.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega (kushoto)  akimkabidhi zawadi maalum spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari Tulia Ackson wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Uwanja wa mpira wa miguu iliyofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama

Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (kulia) Mhe. Daktari Tulia Ackson akipokea jumla ya mifuko 100 ya saruji kutoka kwa Mbunge wa viti maalum Mhe. Martha Mlata (kushoto) huku tukio hilo likishuhudiwa na Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Mhe. Lameck Itungi.




Naibu spika wa Bunge la  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari Tulia Ackson leo aliongoza viongozi na  mamia ya wananchi wa wilaya ya Mkalama katika harambee ya kuchangia ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Wilaya hiyo.

Harambee hiyo ambayo mpaka kukamilika kwake ilifanikisha kupatikana jumla ya shilingi milioni 61 ilihusisha viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa vyama vya siasa, wataalam mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama na wananchi kwa ujumla.

Wakati wa harambee hiyo Mhe. Tulia aliwasifu viongozi wote na watendaji wa wilaya ya Mkalama kwa jitihada mbalimbali wanazofanya katika kuhakikisha wilaya hiyo inapiga hatua kadri muda unavyokwenda.

“Najua Mkalama ni moja ya wilaya ambazo hazina muda mrefu sana tangu kuanzishwa kwake lakini nina uhakika kiwango chake cha maendeleo hivi sasa ni kikubwa kuliko baadhi ya Wilaya kongwe zilizoanzishwa muda mrefu hivyo niwapongeze sana kwa hilo” Alisisitiza Mhe. Tulia.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria harambee hiyo na kutoa michango yao ni pamoja na Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula ambaye alichangia shilingi milioni 4, Mbunge wa viti maalum Mhe. Martha Mlata ambaye alichangia mifuko 150 ya saruji yenye thamani ya shilingi 2,250,000/= na Mbunge wa viti maalum Mhe. Asha-Rose Matembe ambaye alichangia mifuko 50 ya saruji.

Wengine waliochangia katika harambee hiyo ni pamoja na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Mohamedi Mpinga ambaye alichangia mifuko 230 ya saruji, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ambayo ilitoa kiasi cha shilingi 550,000/=, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambaye alichangia bati 98  na shilingi 500,000/=.

Mbali na viongozi hao wengine waliotoa au kuahidi michango yao kwenye harambee hiyo ni pamoja na wakuu wa idara wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama, waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo, wafanyabiashara mbalimbali waliopo ndani ya wilaya hiyo na wananchi mbalimbali waliopo ndani na nje ya wilaya hiyo.

Katika hafla hiyo, Mhe. Tulia alipewa rasmi jina la “Nzitu” ambalo asili yake ni kabila la wanyiramba likimaanisha mtoto ambapo mara baada ya kulipokea alimtangaza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Mkalama Mhe. Lameck Itungi kuwa baba yake rasmi wa kabila hilo.

  

Tuesday 23 October 2018

Sunday 7 October 2018

Ni wajibu wa kila Mtanzania kutunza utamaduni wetu-Mlawi

Kikundi cha Ngoma za asili ya kabila la Wambulu kikionesha umahiri wa kucheza ngoma hiyo wakati wa tamasha la Utamaduni wa makabila ya wilaya za Mkalama na Mbulu lililofanyika jana katika kijiji cha Hydorm.

Kikundi cha maonesho ya sarakasi kutoka Mbulu vijijini kikionesha umahiri wa mchezo huo wakati wa tamasha la Utamaduni wa makabila ya wilaya za Mkalama na Mbulu lililofanyika jana katika kijiji cha Hydorm.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Bi. Suzan Mlawi akimkabidhi cheti mwakilishi wa kikundi cha kabila la wahadzabe ikiwa ni ishara ya kukishukuru kikundi hicho kwa kushiriki kwenye tamasha la utamaduni wa makabila ya wilaya za Mkalama na Mbulu lililofanyika jana katika kijiji cha Hydorm. 

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akimshukuru na kumuaga Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Bi. Suzan Mlawi ambaye alikuwa mgeni rasmi wa tamasha la utamaduni wa makabila ya wilaya za Mkalama na Mbulu lililofanyika jana katika kijiji cha Hydorm. 


Mkoa wa Singida kupitia Wilaya ya Mkalama na mkoa wa Manyara kupitia wilaya ya Mbulu leo wameadhimisha tamasha la pamoja la utamaduni wa makabila makuu yaliyopo kwenye mikoa hiyo tukio lililofanyika katika kijiji cha Hydorm.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa utamaduni na Michezo Bi. Suzan Mlawi ambaye alizipongeza wilaya hizo kwa kufanikisha maadhimisho ya tamasha hilo huku akisisitiza kuwa suala la kudumisha mila na utamaduni wa watanzania ni jukumu la kila mwananchi.

“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na taifa lililokufa hivyo ni lazima kila mmoja wetu aenzi na kudumisha mila na desturi zetu kwani ndio kitambulisho chetu hata tunapokuwa nje ya nchi yetu” Alisisitiza Bi. Mlawi.

Bi Mlawi aliongeza kuwa maadhimisho hayo ni ishara kubwa inayoonesha ushirikiano wa dhati uliopo baina ya Wilaya ya Mkalama na Mbulu ambapo aliwasihi viongozi wa pande hizo mbili kuendeleza na kudumisha umoja huo huku wakiendelea kuenzi mila na desturi za Mtanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka aliipongeza kamati ya maandalizi ya tamasha hilo na kuwataka wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama kuhakikisha wanajitokeza kwenye tamasha hilo ambalo litafanyika kila mwaka.

“Kuhudhuria tamasha hili ni utalii tosha kabisa na mtu anaweza kuja na familia yake kwa ajili ya mapumziko hivyo nawasihi wananchi wa Mkalama na maeneo mengine ya jirani wafike kushuhudia tukio hili la asili kabisa” Alisisitiza Mhe. Masaka.

Tamasha hilo lilipambwa na burudani mbalimbali za asili kutoka makabila ya Wagogo, Wasukuma, Wangoni, Wahadzabe, Wanyiramba, Wanyisanzu,  Wairaqi, Wamasai na Wadatoga huku kivutio kikubwa kikiwa ni vipaji vilivyooneshwa na mbunge wa jimbo la Mbulu vijijini  Mhe. Flatei Massay na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka ambao walionesha ustadi mkubwa katika kucheza ngoma na nyimbo za asili.

Mbali na ngoma na nyimbo za asili kutoka katika makabila tofauti, tamasha hilo lilijumuisha pia maonesho ya vitu mbalimbali vya asili, wanyamapori kama vile Simba, Chui, Mamba na kobe mwenye umri wa miaka 200 na utamaduni wa kabila la Wadatoga.

Kijiji cha Hydorm kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Mkalama na Mbulu kwa sasa kinatambulika kama kitovu cha Afrika kutokana na kujumuisha makundi makuu manne ya jamii za bara la Afrika ambao ni Wanyiramba na Wanyisanzu (Wabantu), Wadatoga (Wanailo), Wahadzabe (Wakwesa) na Wairaqi (Wakushi).

Makundi hayo pamoja na kuishi pamoja kama ndugu katika kijijichi hicho wanatofautiana katika lugha, historia, utamaduni na mgao wa utumiaji wa rasilimali.


Miongoni mwa wadhamini wakubwa wa tamasha hilo kwa mwaka huu  ni pamoja na serikali ya Norway chini ya kitengo cha Utamaduni kinachojulikana kama 4CCP (4 Corners Cultural Programs), Mbuga ya wanyama ya Ngorongoro, Kampuni ya Yara, Shirika la bima ya afya la MHI na  benki ya CRDB.

Monday 10 September 2018

Nataka daraja likamilike mwezi machi-Magufuli



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari John Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria tukio la uwekaji wa jiwe la msingi la daraja la mto Sibiti mapema leo huku akishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa serikali.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari John Pombe Magufuli akiwaongoza viongozi mbalimbali zoezi la uwekaji jiwe la msingi  la daraja la mto Sibiti mapema leo. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari John Pombe Magufuli akiwaaga wananchi waliojitokeza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi daraja la Sibiti mapema leo.

Baadhi ya waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakiwa kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la daraja la Mto Sibiti mapema leo tukio lililofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari John Pombe Magufuli.

Sehemu ya umati wa watu uliojitokeza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la daraja la mto Sibiti  iliyofanyika mapema leo darajani hapo.


“Haiwezekani  ujenzi wa daraja uchukue zaidi ya miaka sita wakati mkandarasi analipwa stahiki zake zote kwa wakati tena kwa kutumia kodi za Watanzania hivyo daraja hili ni lazima likamilike ifikapo mwezi machi mwakani, Wizara mjipange kweli kweli kwa sababu tutafukuzana hapa hapa na kuanzia sasa hivi nalifanya kuwa kipaumbele changu namba moja kwa kulifuatilia hivyo ntapiga simu usiku na mchana ili kujua limefikia wapi”

Ni kauli iliyotolewa mapema leo na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari John Pombe Magufuli wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi la Mto Sibiti baada ya kutofurahishwa na kasi ya mkandarasi anayejenga daraja la mto huo  huku pia akizikataa sababu mbalimbali za uchelewaji huo zilizotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa wakala wa barabara wa Taifa (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale na Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwelwe.

“Waziri kama unaona mkandarasi huyu hana uwezo wa kumaliza kazi hii kwa wakati ni bora utafute mkandarasi mwingine kwa sababu sina uhakika hata kama mkandarasi huyu ana vifaa vya kutosha kumaliza kazi hii na huenda hata hivi navyoviona hapa vimeletwa jana usiku baada ya kusikia ninakuja leo” Aliongeza Mhe. Magufuli.
Mhe. Magufuli aliwaagiza wenyeviti wa bodi ya wakandarasi na washauri wa wakandarasi kuwasimamia ipasavyo mkandarasi na mshauri wa mkandarasi  wa daraja hilo na kama wataonekana kufanya kazi chini ya kiwango wachukuliwe hatua kwa mujibu wa taratibu za bosi hizo.

“Nyie ‘consultants’  mnapaswa kujua mpo hapo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na najua nyie ni wafanyabiashara but this is not a good business for you  so watch out’’ Alionya Mhe. Magufuli.

Katika hotuba yake Mhe. Magufuli aliieleza halaiki ya wananchi waliojitokeza katika tukio hilo kuwa baada ya kukamilika kwa daraja hilo  uchumi wa Mikoa ya Singida na Simiyu utaimarika zaidi kwa sababu utawapa fursa wananchi wa pande hizo mbili kufanya biashara ya rasilimali wanazozalisha.

“Waziri wa Madini amesema hapa kuwa Mkoa wa Simiyu una chumvi nyingi sana kwa hiyo nategemea kukamilika kwa daraja hili kutachochea uchimbaji zaidi wa chumvi hiyo ambapo kiwango kikiridhisha tunaweza hata kuongeza kodi ya uingizaji wa chumvi ya nje ili kuongeza matumizi ya chumvi tunayozalisha wenyewe hapa ndani” Alisisitiza Mhe. Magufuli.

Mhe. Rais alihitimisha hotuba yake kwa kumpongeza Mbunge wa Mkalama Mhe. Allan Kiula kwa ushirikiano mzuri alionao dhidi ya wanasiasa wenzake ndani ya Wilaya na wataalam wote wa Wilaya hiyo ambapo alimtaka kuendeleza ushirikiano huo ili kuzidi kuongeza maendeleo ya Wilaya hiyo.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi alimshukuru Mhe. Magufuli kwa ujenzi wa daraja hilo ambapo alimhakikishia kuwa tayari Mkoa wa Singida umejipanga kuhusu matumizi sahihi ya daraja hilo na mkakati wa utunzaji wa mazingira yanazunguka daraja hilo umeshakamilika.

“Mhe. Rais ninakushukuru kwa sababu hivi sasa maji ya ziwa Victoria yatakayopita Simiyu yatafika mpaka Singida kupitia Mkalama” Alisema Mhe. Nchimbi.

Mpaka sasa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia zaidi ya shilingi bilioni 2002 za mapato yake ya ndani katika kuboresha na kutengeneza miundombinu ya barabara huku daraja la Sibiti likigharimu jumla ya shilingi bilioni 16 mpaka kukamilika kwake ambapo kwa sasa limefikia asilimia 70 na kugharimu shingi bilioni 15.








HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA