‘’Nyie wote mlioshiriki katika maadhimisho haya ya Sikukuu
ya Wakulima na wafugaji mnatakiwa kuhakikisha yale mliyojifunza yanaonekana
kupitia kwa wananchi wenu huko mlipotoka’’
Ni moja ya kauli zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida
Mhe. Daktari Rehema Nchimbi wakati wa hotuba yake muda mfupi kabla hajafungua
rasmi maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji kanda ya kati
maarufu kama Nane nane yanayoendelea hapa jijini Dodoma.
Katika hotuba yake Mhe. Nchimbi alibainisha kuwa mwaka huu
wa fedha Serikali imetenga shilingi trilioni 13.8 kwa ajili ya Kilimo na Mifugo
hivyo aliwataka wadau wa sekta hizo kutumia fursa hiyo vizuri na kuhakikisha
sekta za kilimo na mifugo zinakuwa chachu ya kuhakikisha azma ya Tanzania
kuelekea kwenye uchumi wa viwanda inatimia.
“Leo wakati natembea kwenye mabanda mbalimbali nimekutana
na mkulima ambaye katika maelezo yake amenieleza kupitia boga moja nililomkuta
nalo badala ya kuliuza shilingi elfu 10 ana uwezo wa kulitumia kuingiza zaidi ya shilingi laki moja kwa kutengeneza
juice, maandazi na keki” Alisema Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi alisema kuwa hivi sasa zao la korosho limekuwa ni zao mkakati katika mikoa ya
Dodoma na Singida ambapo viongozi wa
mikoa hiyo wanataka kuhakikisha ndani ya miaka minne ijayo mikoa hiyo itakuwa
vinara wa mazao hayo.
“Kwa bahati mbaya katika maeneo yaliyozoeleka kulima mazao
hayo tafiti zinaonesha wanavuna mazao hayo mara moja tu kwa msimu lakini huku
kwetu hasa mkoani Singida imeshathibitika zao la korosho kuweza kuvunwa mara
mbili kwa mwaka” Aliongezea Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi amewataka Wakulima kujikita kwenye kilimo cha
umwagiliaji ili kuendelea kuongeza kipato kupitia sekta hiyo kwa mwaka mzima
badala ya hivi sasa ambapo wakulima wengi baada ya kuuza mavuno yao hushinda
vijiweni huku wakisubiri msimu wa masika.
No comments:
Post a Comment