Hatimaye awamu ya sita ya ugawaji wa ruzuku kwa Mwaka wa
fedha 2015/2016 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) kwa Wilaya ya Mkalama
imefikia kikomo ambapo jumla ya Shilingi 200,408,000 zimegawiwa kwa walengwa.
Mratibu wa TASAF Wilaya ya Mkalama, Athuman Dule
amewashukuru viongozi wa vijiji na walengwa wote kwa ushirikiano waliouonesha
katika zoezi hilo ambapo aliainisha changamoto mbalimbali zilizojitokeza huku
kubwa ikiwa ni baadhi ya walengwa kutojitokeza kuchukua ruzuku zao.
Dule amesema kuwa changamoto hiyo imetokana na taarifa
kutofika kwa walengwa wote kwa wakati ingawa taarifa za maandishi
zilifika kwa watendaji wa vijiji mapema kabla ya zoezi la awamu hii kuanza.
“ Mpaka sasa jumla ya shilingi 1484000 imerejea ofisini
kutokana na changamoto hiyo hivyo ninawasisitiza kamati ya TASAF ngazi ya
vijiji (CMC) wawajazie walengwa fomu ya madai kama utaratibu unavyoelezwa kisha
fedha hizi watapewa pamoja na zile za awamu ijayo ya mwezi Julai/ Agosti”
Aliongeza Dule.
Akisisitiza juu ya mkakati wa kuhakikisha changamoto
hiyo haijitokezi tena katika awamu ijayo, Dule amesema kuwa ofisi yake itafanya
mikutano na walengwa katika kila kijiji na kuwasisitiza juu ya umuhimu wa
kupeana taarifa baina yao ili hata wale ambao hawatapata taarifa kutoka kwa uongozi
wa kijiji wapate taarifa kutoka kwa walengwa wenzao.
No comments:
Post a Comment