Hiki ni kisima cha maji ambacho kipo katikati ya jiwe kubwa katika kijiji cha Isanzu . Maji haya hayajawahi kuisha hata yakitumiwa kiasi gani. |
Unyayo wa mtu wa kale kama unavyoonekana pichani ukiwa katikati ya jiwe katika kijiji cha Isanzu. |
Pichani hapo kwenye uwazi ndipo palipokuwa pakitumika kwa ajili ya mikutano mbalimbali na serikali ya wakoloni wa Kijerumani. |
Haya ndo yalikuwa makazi, Ofisi na Mahakama ya Serikali ya wakoloni wa Kijerumani wakati wa Utawala wao yaliyopo katika kijiji cha Mkalama. |
Neno Mkalama linatokana na neno la lugha ya asili ya kabila la wanyiramba ambalo
lilizaliwa baada ya mti mkubwa sana kuliko yote kwenye kijiji hicho kuonekana
kulalia upande mmoja ambapo kitendo hicho ndio huitwa “kukalama”. Baadaye mti
huo maarufu ulipewa jina la “ Mkalama” ambalo lilienea sana na hatimaye kijiji
chote kupewa jina hilo.
Pengine unaweza kudhani uzuri wa Mkalama unaishia hapo La
hasha! Wakati wa uasisi wake, Kijiji cha
Mkalama kilikuwa chini ya Wilaya ya Iramba ambayo ni moja ya Wilaya zilizopo
katika Mkoa wa Singida lakini baada ya kutanuka kwa wigo wa upatikanaji wa
huduma za Msingi, serikali iliamua kuigawa Wilaya ya Iramba na hatimaye
kupatikana Wilaya nyingine ambayo kwa heshima na uzuri wa yanayopatikana katika
kijiji cha Mkalama serikali iliamua kuipa Wilaya hiyo mpya jina la Mkalama.
Labda msomaji yoyote wa Makala hii anaweza kujiuliza ni
mambo gani yaliyonisukuma kuelezea uzuri wa Wilaya hii, naomba nichukue fursa
hii kukudokeza japo kwa uchache yanayopatikana katika Wilaya hii.
Hapo hapo katika kijiji cha Mkalama ndipo yalipokuwa makazi
ya kudumu ya Wajerumani walipofika Tanganyika na kwa Mujibu wa Mzee Mbizi
Kitundu na Wilfred Mulundi ambao walifanya kazi wakati wa Utawala wa wajerumani
hao, Wajerumi walikuwa wakitumia sana usafiri wa farasi ambao waliendeshwa na
wafanyakazi wa kiafrika kwa ajili ya kupokea na kusindikiza wageni hao.
Kivutio kikubwa hapo ni wazee hao ambao mpaka sasa hawajui
wana umri wa miaka mingapi lakini kutokana na ukweli kuwa wajerumani waliondoka
kabisa Tanganyika baada ya Vita kuu ya Kwanza ya Dunia, wazee hao wanakadiriwa kuwa na zaidi ya miaka
120 na hata unapozungumza nao ni lazima ukae kando yao ndipo uweze kusikia
wanachozungumza na hawazungumzi lugha yoyote zaidi ya kijerumani na kinyiramba.
Ushahidi juu ya uwepo wa wajerumani waliofika katika Wilaya
ya Mkalama unapatikana katika kijiji cha Mkalama kupitia magofu makubwa ambayo
waliyatumia kwa makazi, Ofisi na mahakama.
Si mapango ya wajerumani pekee yanayoifanya Mkalama kuwa Mji
uliojaa wingi wa vivutio kwani Uwepo wa mapango makubwa katika kijiji cha
Isanzu ni moja ya mambo ambayo huwezi kukubali kuyakosa.
Ukiacha uzuri wa mapango hayo, mambo ya kuzingatia kabla ya
kuingia kwenye mapango hayo ni moja ya mambo
yanavutia zaidi, Naomba nichukue fursa hii kukujuza mambo hayo.
Kabla ya hujaingia kwenye msitu huo ni lazima uhakikishe
hauna kitu chochote chenye rangi nyekundu kwa sababu rangi hiyo huwa
inachukuliwa kama ni rangi ya kafara na hivyo kumfanya yoyote anayeonekana na
vazi hilo kuwa kama mtu mwenye mkosi.
Ndani ya mapango hayo
kuna mti ambao mnyama yoyote ambaye anaweza kuchinjwa huwa analala tu
bila tatizo taari kwa kuchinjwa bila kushikwa na mtu wala kufungwa Kamba na
jambo hilo linamhusu mnyama yoyote bila kujali umbo alilonalo au aina ya ukali
alionao.
Pia kuna ngoma kubwa zenye urefu usiopungua mita saba ambazo
zilikuwa zinatumiwa na watu walioishi kwenye mapango hayo hali inayoashiria
kuwa Watu wa kale walikuwa warefu sana kiasi cha kumudu kupiga ngoma hizo huku
wakiwa wamesimama.
Huku ukistaajabu hayo unapaswa kujua kuwa Kijiji cha Isanzu
ndipo sehemu ambapo utaziona nyayo za watu wa kale na cha kushangaza zaidi
nyayo hizo zipo juu ya mawe hali inayozua maswali mpaka leo juu ya kipimo cha
uzito waliokuwa nao watu wa kale.
Mkalama imezungukwa na milima ambayo tofauti na milima
inayopatikana sehemu nyingine kwani milima hii ndani yake kuna mapango makubwa
yenye michoro ya aina mbalimbali lakini cha kufurahisha zaidi ni uwepo wa
viumbe ambao mpaka sasa hawajajulikana ni viumbe wa aina gani lakini mara kwa
mara muda wa jioni watu wanaoishi karibu na milima hiyo wamekuwa wakisikia
ngoma na sauti mbalimbali zikiimba nyimbo za asili na mara nyingi
kwa mujibu wa wazee
wakongwe wanaoishi maeneo hayo wanasema hao ni mabaki ya vizazi vya watu wa kale
kabisa ambao mpaka leo wanaishi katika milima hiyo huku chakula chao kikubwa
kikiwa ni matunda ya porini na wanyama pori.
Kwa leo naomba niishie hapa, Mungu akipenda tutaendelea na
Makala haii ili uzidi kuufahamu utamu na uzuri wa Wilaya ya Mkalama.
Maoni au Ushauri:
0655949391.
No comments:
Post a Comment