Thursday, 22 June 2017

Mkalama imeadhimisha Siku ya Mtoto Afrika

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka akimpa chanjo ya vitamin A mmoja wa watoto wa kijji cha Ishenga ikiwa ni ishara ya kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Kimkoa kijijini hapo

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe:Mhandisi Jackson Masaka ( aliyevaa suti) akiongoza maandamano ya watoto ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa kijijini Ishenga. 

Watoto wakionesha mabango yenye jumbe mbalimbali kwenye maadhimisho ya Siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Ishenga.






Tarehe 16, juni 1976, Dunia ilishuhudia ukatili mkubwa sana pengine kuliko wowote uliowahi kufanywa dhidi ya watoto pale ambapo serikali ya Makaburu ya Afrika Kusini ilipopokea kwa kuwapiga risasi watoto waliokuwa wakiandamana kupinga utaratibu wa Elimu ya kibaguzi  iliyokuwa ikitolewa wakai huo.

Ni kutokana na tukio hilo la kinyama ambalo mpaka leo bado idadi kamili ya waliouawa haijawahi kuwekwa wazi ndipo Dunia iliamua kuitumia tarehe hiyo kila Mwaka kuadhimisha sikukuu ya Mtoto wa Afrika ambapo kwa Mkoa wa Singida na Wilaya ya Mkalama maadhimisho hayo mwaka huu yamefanyika katika kijiji cha Ishenga kilichopo kata ya Kinyangiri.

Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo mwaka huu alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe: Daktari Rehema Nchimbi ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka.

Katika hotuba yake, Mhe: Masaka amesema kuwa watoto ni hazina kubwa sana ya taifa, bara na dunia kwa ujumla hivyo hawana budi kutimiziwa haki zao zote za msingi.

“Haki kubwa kuliko zote ambayo kila mtoto ni lazima aipate ni Elimu na bahati nzuri Serikali yetu imeamua kuwalipia gharama za shule watoto wote kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne hivyo ni kosa kisheria kwa mzazi kumnyima mtoto haki hii ya msingi” Amesema Masaka.

Mhe: Masaka pia ametoa agizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa kuwa halmashauri zote za Wilaya za Mkoa wa Singida zihakikishe zinatenga maeneo ya viwanja vya michezo vya watoto ili kuwaepusha watoto hao kujitengea maeneo hatarishi kama vile kwenye barabara, reli na karibu na mitambo ya umeme.

“Ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha anamtunza mtoto aliyemzaa na sio kumtelekeza kwa sababu kwa mujibu wa sheria za nchi yetu kuzaa ni tendo la hiyari lakini kumtunza mtoto ni lazima” Ameongeza Masaka.

Amesema kuwa ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha anampatia mtoto Lishe bora ili kumtengenezea mazingira mazuri ya ustawi wa akili na Mwili ambapo pia alitumia fursa hii kupiga marufuku kwa mtu yoyote kuuza mazao ya chakula katika Wilaya ya Mkalama bila kupewa kibali maalum na katibu Tawala wa Wilaya.

“Katibu Tawala wa Wilaya ndio mratibu mkuu wa suala la Ulinzi wa chakula hapa Wilayani hivyo ni lazima ajiridhishe kiasi cha akiba ya chakula uliyonayo ndipo akupe kibali cha kuuza ziada inayobakia” Amesisitiza Masaka.

Maadhimisho hayo kimkoa yalipambwa na matukio mbalimbali huku lile lililovutia hisia za watu wengi likiwa ni bunge la watoto ambapo watoto walionesha uhodari katika kuchambua kanuni mbalimbali za bunge kupitia kipindi cha maswali na majibu.

Kauli mbiu ya Siku ya Mtoto Afrika mwaka huu ni “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa sawa kwa watoto”  ikihimiza uzingatiaji wa jukumu la Ulinzi na Usalama wa Mtoto na utoaji wa haki sawa kwa watoto wote ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA