Mafunzo yanayojulikana kama “Ukimwi mahala pa kazi”
yamefanyika jana katika halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambapo watumishi wote
wa halmashauri walihudhuria na kupatiwa mafunzo hayo.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe:
Injinia Jackson Masaka aliwataka watumishi wote kuwa makini na kujiepusha na mazingira ambayo yanaweza kuwasababishia maambukizi ya
virusi vya ukimwi.
“Bahati mbaya watumishi wengi hapa hamuishi na wake zenu
au waume zenu hivyo ni vyema muwe na tahadhari kubwa sana kutokana na mazingira
mliyonayo”. Alisema Masaka.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Kamanda wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) kanda ya Iramba na Mkalama Zacharia Mwandumbya alisema ni vizuri
wiongozi, wakuu wa idara na watumishi wote kwa ujumla kutotumia nafasi zao
kuomba rushwa ya ngono kutoka kwa watu wanaohitaji huduma kwenye ofisi zao.
“Unakuta bosi ni wa kiume afu kuna msichana anahitaji
huduma fulani katika ofisi yake lakini atazungushwa au kukataliwa kisa hajampa
rushwa ya ngono, hilo ni kosa na Takukuru tukikubaini tutakukamata na
kukukabidhi katika mamlaka nyingine zikuchukulie hatua Zaidi” Alisema
Mwandumbya.
Aliongeza kuwa ni lazima watumishi wawe makini sana kwa
sababu wanaweza kujikuta wanaomba rushwa ya ngono kwa watu ambao tayari wana
maambukizi ya virusi vya ukimwi au wao wenyewe wanaweza kuwa tayari wana
maambukizi hivyo kufanya hivyo ni sawa na kueneza zaidi ugonjwa huo.
Naye mratibu wa Ukimwi wa Manispaa ya Singida ambaye pia
alikuwa ni muwasilishaji katika mafunzo hayo, Dokta George Mwakahesya alisema
ni vyema kila mtu kupima na kujua afya yake ili kuepusha kufanyishwa kazi
ambazo zitazidi kupunguza kinga ya mwili.
“Ukishajua una virusi vya ukimwi usiogope wala kusita
kwenda kwa Afisa utumishi wako ili iwe rahisi kwake kutokukupa majukumu mazito
sana lakini pia kukujibu kwa haraka pindi unapohitaji kwenda kufanya matibabu”
Alisema Dokta Mwakayesya.
Alimalizia kwa kuwataka watumishi kutumia kinga kila
wanapotaka kufanya tendo la ndoa ili kuepusha maambukizi ya virusi vya ukimwi
maeneo yao ya kazi na pindi wakirejea nyumbani.
No comments:
Post a Comment