Baada ya
jitihada mbalimbali za Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na wananchi wa Mkalama kuhakikisha wanafunzi wote wa Wilaya ya
Mkalama wanakaa kwenye madawati, hatimaye lengo la jitihada hizo limeanza
kutimia baada ya madawati mia moja kukabidhiwa na kuanza kutumika katika shule
ya msingi Gumanga iliyopo Wilayani hapa.
Akizungumza
wakati wa kukagua madarasa ili kuhakikisha kama wanafunzi wote wamekaa kwenye
madawati hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mheshimiwa Christopher Ngubiagai
alisema kuwa amefarijika sana kuona tatizo la wanafunzi kukaa chini au juu ya
mawe likiisha katika Wilaya yake.
“Nawapongeza
sana wananchi wa Gumanga kwa kazi nzuri mliyoifanya ya kutengeneza madawati 150
ikiwa ni Zaidi ya mahitaji halisi ambayo ni 104” Alisema Ngubiagai.
Ngubiagai aliongeza
kuwa mpaka kufika mwisho wa mwezi huu, atahakikisha tatizo la ukosefu wa
madawati linabaki kuwa historia katika Wilaya ya Mkalama ikiwa ni miezi miwili
nyuma ya tarehe ya mwisho aliyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
“Nafurahi kwa tatizo la madawati kuelekea
ukingoni kabisa katika Wilaya ya Mkalama, nataka sasa tuhamishe juhudi zetu
katika kuboresha mazingira ya shule zote zilizopo wilayani kwetu”. Alisema
Ngubiagai.
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Ngubiagai alitumia fursa hiyo ya ukaguzi wa madawati
kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa kata ya Gumanga ambapo baadhi
alizitolea majibu yeye mwenyewe na nyingine
zilijibiwa na kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Ndugu
Chacha James Kihego.
Huu ndio muonekano wa darasa la pili katika shule ya msingi Gumanga baada ya wanafunzi kuanza kukalia madawati. |
Wanafunzi wakikaa kwenye madawati hata nafasi ya mwalimu kupita kukagua kazi zao inapatikana kama unavyoona wanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Gumanga baada ya kuanza kukalia madawati. |
Huu ndio muonekano wa darasa la nne katika shule ya msingi Gumanga baada ya wanafunzi wake kuanza kukalia madawati. |
Wananchi wa kata ya Gumanga wakimsubiri Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mheshimiwa Christopher Ngubiagai azungumze nao machache na kusikiliza kero zao. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mheshimiwa Christopher Ngubiagai (katikati) akijiandaa kuzungumza na wananchi wa kata ya Gumanga. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mheshimiwa Christopher Ngubiagai akizungumza na wananchi wa kata ya Gumanga mambo mbalimbali yanayohusu kata yao |
No comments:
Post a Comment