![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akihutubia umati wa watu waliojitokeza kwenye sherehe za uzinduzi wa kampeni ya Furaha yangu zilizofanyika katika kijiji cha Nkalakala leo. |
![]() |
Kikundi cha Ngoma kutoka kijiji cha Nkalakala kikitumbuiza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya "Furaha yangu" leo katika kijiji cha Nkalakala. |
“Ninaagiza kampeni hii ifanyike katika kata nyingine zote
16 zilizobakia za Wilaya yaMkalama”
Hilo ni agizo lililotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama
Mhe. Mhandisi Jackson Masaka wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upimaji wa hiyari
wa virusi vya ukimwi iliyopewa jina la
“Furaha Yangu” uliofanyika leo katika kijiji cha Nkalakala ambapo zaidi ya watu
250 walijitokeza kupima.
Katika hotuba yake Mhe. Masaka alimshukuru Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwa kuzindua kampeni hiyo
kitaifa yenye lengo la kuhamasisha wananchi hasa wanaume kujitokeza kwa wingi
katika vituo vya afya kupima kwa hiyari virusi vya ukimwi.
“Kwa Wilaya ya Mkalama suala la kupima afya sio jipya
kwetu kwa sababu nimeshuhudia watu wengi sana wakijitokeza kupima afya zao
kipindi cha mkesha wa Mwenge na sherehe nyingine huku vipimo mbalimbali
vikifanyika ikiwemo shinikizo la damu, Malaria na HIV/VVU” aliongeza Mhe.
Masaka.
Mhe. Masaka aliwasisitiza wananchi wote wa Mkalama
kuchukua tahadhari kwa kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya
Ukimwi ili kuweza kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo ambayo kwa mkoa
wa Singida imeonekana kukua kwa asilimia 0.3 kutoka asilimia 3.3 ya mwaka
2011/2012 hadi asilimia 3.6 ya mwaka 2016/2017.
“Lakini pia ninaomba wananchi msipuuze pindi mnapobanwa na
vikohozi visivyoisha kwa sababu huenda ikawa ni dalili ya ugonjwa wa Kifua
kikuu kwa hiyo usijikaushe ewe dada na kaka nendeni mkapime na bahati nzuri
Wilaya yetu imepata wahisani wa kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi
na TB na kampeni hizi ni msaada mkubwa
kwa afya zetu” Aliongeza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka alihitimisha hotuba yake kwa kuwahimiza
wananchi wote kuwashawishi vijana na watoto wao wasome kwa bidii masomo ya
sayansi ili waweze kupata nafasi za kusomea uuguzi, ukunga, maabara, udaktari
na kozi nyingine za afya kwa sababu wasipofanya hivyo watakuwa na majengo
mazuri ya zahanati, vituo vya afya na hospitali lakini hakutakuwa na wataalam
wa kuendesha vituo hivyo.
Kampeni ya “Furaha Yangu” ilizinduliwa kitaifa na Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa mnamo tarehe 16
mwezi juni mwaka huu makao makuu ya nchi jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment