Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Mkalama
Mhandisi Godfrey Sanga ametoa msaada wa chakula na vitu mbalimbali vyenye
thamani ya zaidi ya Shilingi laki sita kwa wananchi wa kijiji cha Nkungi ambao
waliathiriwa na ugonjwa wa Ukoma maarufu kama Wakoma.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya
ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka amesema kuwa hivi sasa Wilaya inafanya
utaratibu wa kuanza kuwahudumia wakoma hao badala ya kusubiri misaada kutoka
kwa wahisani mbalimbali.
“Misaada inachukua muda mrefu kufika na ikifika inakuwa ni
michache hali inayozidi kuwapa wakati Mgumu waathirika hawa kwa sababu
wanahitaji uangalizi wa hali ya juu” Alisema Masaka.
Mhe: Masaka amewapongeza wadau wa shirika la African Smile
kwa kujitolea kujenga nyumba za waathirika hao na kutoa rai kwa vijana na
wananchi wa kijiji hicho kuendelea kujitolea kuwasaidia katika kuboresha makazi
ya waathirika hao.
Aliongeza kuwa shirika la FCC liliwasilisha barua ofisini
kwake na kuwaandikia barua ya kupewa msamaha wa kodi ili waweze kupitisha
chakula cha waathirika hao ambacho hutolewa na watu wa Marekani hivyo muda
wowote kuanzia sasa chakula kitakuwa kimeshafika katika kambi hizo za Wakoma.
“Lakini kwa sababu mimi ni kiongozi wa Wilaya ninaagiza
Mkurugenzi uwaandikie watendaji wa kata ili kila kata itoe kiasi cha gunia moja
kwa ajili ya kuzisaidia kambi hizi na naomba nipate taarifa ya utekelezaji juu
ya hili” Aliagiza na kumalizia Masaka.
No comments:
Post a Comment