Monday, 27 June 2016

KILA LA KHERI NGUBIAGAI

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Mteule wa Kilwa Mhe: Christopher Ngubiagai akizungumza na Madiwani na wakuu wa Idara muda mfupi uliopita katika kikao cha baraza la madiwani ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaaga rasmi.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na Wakuu wa Idara wa Halmashauri hiyo wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Mkalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Mteule wa Kilwa muda mfupi uliopita wakati akiwaaga rasmi.
Baada ya kuiongoza Wilaya ya Mkalama kwa kipindi kisichozidi miezi nane, Mkuu wa Wilaya hiyo  Mhe: Christopher Ngubiagai ametumia kikao cha baraza la madiwani kilichomalizika muda mfupi uliopita kuwaaga viongozi na wananchi wote wa Wilaya hiyo.

Kitendo hicho kinafuatia mabadiliko na uteuzi wa wakuu wa Wilaya uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: Dokta John Pombe Magufuli ambaye amemhamishia Mhe: Ngubiagai katika Wilaya ya Kilwa.

“Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru sana kwa ushirikiano na upendo mlionionesha tangu niteuliwe kushika wadhifa huu tar 5 mwezi Oktoba mwaka jana, Mwenyezi Mungu awajaalie sana” Amesema Ngubiagai.

Mhe: Ngubiagai ameshukuru kwa uzoefu mkubwa alioupata katika Wilaya ya Mkalama na kuomba viongozi na wananchi wote wa Wilaya hiyo kumpa ushirikiano wa kutosha mbadala wake pindi atakapoanza kazi yake.

Pia ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa uongozi wa Wilaya ya Mkalama pamoja na mbadala wake kutilia mkazo kwenye suala la Elimu ambapo amesisitiza kuwa itakuwa ni jambo linalopendeza kwa Wilaya hiyo yenye watu Zaidi ya laki mbili kuwa na shule ya Elimu ya juu ya sekondari.


“Lakini pia nitumie fursa hii kuwaomba mtumie fursa nzuri na kubwa ya kiuchumi iliyopo Wilayani Mkalama kuongeza kipato cha Wilaya na kuinua hali ya uchumi wa mwananchi mmoja mmoja hasa kupitia sekta ya madini ambayo hivi sasa ni wageni tu ndio wanaonufaika” Alimalizia Ngubiagai.


No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA