Tuesday, 30 October 2018

Ujenzi hospitali ya Wilaya uanze wiki ijayo- Ndugulile

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Daktari Faustine Ndugulile akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kinyambuli mapema leo alipotembelea kituo cha Afya cha Kinyambuli.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Daktari Faustine Ndugulile (katikati)  akitoa agizo la kuanza kwa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Mkalama wakat wa ziara yake aliyoifanya wilayani hapa leo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Daktari Faustine Ndugulile akihitaji ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya ujenzi kutoka kwa Mhandisi wa ujenzi wa wilaya ya Mkalama  Bi. Paskazia Tibalinda (wa pili kutoka kulia) wakati wa ziara yake leo wilayani hapa.

Viongozi mbalimbali wa serikali wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameendelea na ziara za kikazi ndani ya wilaya ya Mkalama ambapo leo ilikuwa ni zamu ya Naibu waziri wa Wizara ya Afya , Maendeleo ya jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Daktari Faustine Ndugulile.

Mhe. Ndugulile aliipongeza wilaya ya Mkalama kwa jitihada za dhati za kuhakikisha wanapanda katika vigezo vya ubora wa utoaji wa huduma za afya au  “Star rating”  kama inavyojulikana kitaalam ambapo mwaka 2016  vituo vyote vilikuwa chini ya nyota 3 hali iliyoashiria hakuna kituo kilichokuwa kimekidhi viwango vya utoaji wa huduma bora.

“Lakini mwaka 2018 asilimia 33.5 ya vituo vilivyopo hapa Mkalama vimepata  nyota 3 au zaidi huku aslimia 66.5 ya vituo vikiwa na nyota 2 na hakuna hata kituo kimoja kisicho na nyota hivyo jambo lililoifanya Wilaya ya Mkalama kuwa ya tatu kwa mkoa wa Singida kwa upande wa utoaji wa huduma bora za Afya, hongereni sana” Alisisitiza Mhe. Ndugulile.

Akiwa katika eneo lililoandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya, Mhe. Ndugulile aliwapongeza wananchi wa kata ya Nduguti kwa kujitolea eneo kwa ajili ya kujenga hospitali ya Wilaya bila fidia yoyote ambapo aliwataka wananchi wa maeneo mengine nchini kuiga mfano huo.

“Kwa sababu tayari mmeshaletewa fedha za awamu ya kwanza na michoro mnayo ninaagiza ujenzi wa hospitali hii ya Wilaya uanze mapema wiki ijayo na kama kuna mtu atasema msubiri michoro mwambieni michoro hiyo aniletee mimi “ntadeal” naye lakini nyinyi anzeni kazi” aliongeza Mhe. Ndugulile.

Mhe. Ndugulile alimalizia ziara yake kwa kutembelea kituo cha afya cha Kinyambuli ambapo alizipongeza kamati zote zilizoshiriki katika ujenzi wa kituo hicho na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kuhakikisha anatumia fedha za mapato ya ndani kumalizia kazi zote zilizobaki za ujenzi wa kituo kufikia mwisho wa mwaka huu ili kuanzia mapema mwakani wananchi waanze kupatiwa huduma katika majengo hayo mapya.

“Lakini pia niwatangazie wananchi wa Kinyambuli na Watanzania wote kuwa hivi sasa tumeanza kudhibiti dawa tunazosambaza kwa kuziwekea alama inayosomeka “MSD GOT” ambayo mbali na kuiweka nje ya maboksi ya dawa pia tumeiweka mpaka ndani kwenye tembe na kwenye bomba za sindano hivyo yoyote atakayeona vifaa tiba na dawa zenye alama hiyo zinauzwa kwenye maduka binafsi ya dawa tafadhali atoe taarifa kwenye mamlaka za Ulinzi na usalama” Aliongeza Mhe. Ndugulile.

Kwa mwaka 2018 serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia zaidi ya shilingi bilioni 5.3 kwa ajili ya ukarabati na uwekaji wa miundombinu ya Afya mkoani Singida ambapo pia imeuongezea Mkoa huo bajeti ya Afya kutoka shilingi bilioni 4 ya mwaka 2017/2018 hadi shilingi bilioni 7.5 kwa mwaka 2018/2019.No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA