Wednesday, 8 August 2018

Mkalama yang'ara Nanenane Kanda ya kati

Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde (kulia) akimkabidhi cheti cha Ushindi Afisa Mifugo wa Wilaya ya Mkalama Bw. Elias Mbwambo baada ya Wilaya hiyo kuibuka mshindi wa kwanza kwa halmashauri za wilaya zilizopo Mkoani Singida kwenye kilele cha maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji (NANENANE)  Nzuguni jijini Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akimpongeza Afisa Mifugo wa Wilaya ya Mkalama Bw. Elias Mbwambo baada ya Wilaya hiyo kuibuka mshindi wa kwanza kwa halmashauri za wilaya zilizopo Mkoani Singida kwenye kilele cha maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji (NANENANE) hapa Nzuguni jijini Dodoma.

Wawakilishi wa wakulima wa Wilaya ya Mkalama wakijumuika na viongozi wa Idara za Kilimo na Mifugo za Wilaya hiyo kufurahia ushindi baada ya Wilaya hiyo kuibuka mshindi wa kwanza kwa halmashauri za wilaya zilizopo Mkoani Singida kwenye kilele cha maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji (NANENANE) Nzuguni jijini Dodoma.
“RUDI MKALAMA, KUMENOGA!”   Hiyo ndio kauli inayoweza kutumika hivi sasa baada ya Wilaya ya Mkalama kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwa Halmashauri za Mkoa wa Singida kwenye maonesho ya 22 ya sikukuu ya wakulima na Wafugaji (NANENANE)  yaliyohitimishwa leo hii na Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde.

Ushindi huo  unatokana na Wilaya hiyo kujidhatiti kikamilifu katika sekta za Kilimo na Mifugo ambapo waliweza kuonesha kwa vitendo kwa kuotesha mimea mbalimbali inayolimwa Wilayani Mkalama kupitia mashamba yao yaliyopo hapa kwenye viwanja vya Nzuguni.

Mbali na mimea hiyo iliyostawi vizuri, Mkalama pia wameweza kuonesha ustadi wa kufuga samaki na kuku ambapo wataalam wa mifugo na uvuvi waliweza kuonesha namna bora kabisa ya kufuga kuku wa kienyeji na aina mbalimbali za samaki kupitia bwawa lililopo nyuma ya banda lao  la Maonesho.

Katika hali inayoonesha kujipanga zaidi kwa Uongozi wa Wilaya ya Mkalama katika maonesho yajayo, Wilaya hiyo imeshatengeneza mabanda ya kufugia Ng’ombe na Mbuzi hivyo kwa wageni watakaotembelea banda hilo kwenye maonesho ya mwaka 2019  watapata fursa ya kujifunza namna bora ya kufuga ng’ombe na mbuzi.

Mkalama Guntooooooo!Monday, 6 August 2018

Ni lazima taarifa za masoko ziwafikie wakulima- Masaka

PICHA 10 CHINI: Ziara  ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka aliyoifanya leo kwa kutembelea  mabanda mbalimbali ya maonesho ya Nanenane kanda ya kati yanayofanyika jijini Dodoma.Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka leo alikuwa mgeni rasmi katika manesho ya 22 ya sikukuu ya Wakulima na Wafugaji (nanenane) kanda ya kati ambapo alitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika viwanja vya maonesho hayo jijini Dodoma.

Ziara hiyo ya Mhe. Masaka ilianzia katika banda la Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambapo aliishauri wizara hiyo kufanya matumizi mbadala ya jengo lao walilolijenga kwa ajili ya  maonesho ya Nane nane badala ya kuliacha wazi huku likisubiri siku ambayo maadhimisho ya kitaifa yatafanyikia jijini Dodoma.

“Kuna taasisi mbalimbali zinapenda kushiriki maonesho haya lakini zimekosa maeneo ya kuweka bidhaa zao, mnaweza kuwapa jengo hilo au mnaweza hata kufikiria kuweka maonesho ya utamaduni ili wananchi waweze kufahamu kwa kina tamaduni za kitanzania kwa sababu kuliacha bila matumizi yoyote kama mnavyofanya hivi sasa ni kupoteza fedha za serikali ilizowekeza wakati wa kulijenga” Alisisitiza Mhe. Masaka.

Baada ya kutoka katika banda la TAMISEMI Mhe. Masaka alielekea katika banda la wataalam wa ufugaji wa kisasa wa kuku wanaojulikana kama ‘’Silverland’’ ambapo akiwa hapo aliwashauri wataalam hao kuhakikisha elimu inayohusu ufugaji wa kuku ifike mpaka kwa wafugaji wadogo badala ya kuishia kwenye maonesho ya Nanenane.

Mhe. Masaka ambaye katika ziara hiyo aliongozana na viongozi wengine waandamizi wa Mkoa wa Dodoma na Wizara ya Kilimo alifika pia  katika banda la Mamlaka ya Maendeleo ya biashara (TANTRADE)  ambapo akiwa hapo aliisisitiza mamlaka hiyo kuhakikisha inatoa matangazo kwa wakulima juu ya masoko ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha.

“Sasa hivi wakulima wanalima lakini wengi hawajui masoko ya mazao wanayolima yako wapi matokeo yake wanajikuta wanalima kilimo kisicho na tija hivyo ninawashauri mtengeneze utaratibu mzuri wa kuwajulisha wakulima kuhusu aina ya mazao yanayohitajika sokoni na mahali yanapohitajika mazao hayo’’ Aliongeza Mhe. Masaka.

Mbali na mabanda hayo Mhe. Masaka pia alitembelea Mamlaka ya Uhamiaji, benki ya CRDB, halmashauri za wilaya za Mkalama na Chamwino, AGRICOM na Polymachinery, Sido na Benki kuu ya Tanzania (BOT).Saturday, 4 August 2018

Miaka minne ijayo Singida na Dodoma tutaongoza korosho- Nchimbi

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akitoa hotuba jioni ya leo wakati akifungua rasmi maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na wafugaji maarufu kama nanenane kanda ya kati  jijini Dodoma.
‘’Nyie wote mlioshiriki katika maadhimisho haya ya Sikukuu ya Wakulima na wafugaji mnatakiwa kuhakikisha yale mliyojifunza yanaonekana kupitia kwa wananchi wenu huko mlipotoka’’

Ni moja ya kauli zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi wakati wa hotuba yake muda mfupi kabla hajafungua rasmi maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji kanda ya kati maarufu kama Nane nane yanayoendelea hapa jijini Dodoma.

Katika hotuba yake Mhe. Nchimbi alibainisha kuwa mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi trilioni 13.8 kwa ajili ya Kilimo na Mifugo hivyo aliwataka wadau wa sekta hizo kutumia fursa hiyo vizuri na kuhakikisha sekta za kilimo na mifugo zinakuwa chachu ya kuhakikisha azma ya Tanzania kuelekea kwenye uchumi wa viwanda inatimia.

“Leo wakati natembea kwenye mabanda mbalimbali nimekutana na mkulima ambaye katika maelezo yake amenieleza kupitia boga moja nililomkuta nalo badala ya kuliuza shilingi elfu 10 ana uwezo wa kulitumia  kuingiza zaidi ya shilingi laki moja kwa kutengeneza juice, maandazi na keki” Alisema Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi alisema kuwa hivi sasa zao la korosho  limekuwa ni zao mkakati katika mikoa ya Dodoma na Singida  ambapo viongozi wa mikoa hiyo wanataka kuhakikisha ndani ya miaka minne ijayo mikoa hiyo itakuwa vinara wa mazao hayo.

“Kwa bahati mbaya katika maeneo yaliyozoeleka kulima mazao hayo tafiti zinaonesha wanavuna mazao hayo mara moja tu kwa msimu lakini huku kwetu hasa mkoani Singida imeshathibitika zao la korosho kuweza kuvunwa mara mbili kwa mwaka” Aliongezea Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi amewataka Wakulima kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuendelea kuongeza kipato kupitia sekta hiyo kwa mwaka mzima badala ya hivi sasa ambapo wakulima wengi baada ya kuuza mavuno yao hushinda vijiweni huku wakisubiri msimu wa masika.


Thursday, 12 July 2018

Uwanja wa kisasa kujengwa Mkalama

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa katika sehemu ya watu mashuhuri ''VIP''

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa kwa muonekano wa juu

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa kwa muonekano wa mbele

Jinsi Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Wilaya ya Mkalama utakavyokuwa kwa muonekano wa pembeni
Habari Njema na kubwa kwako Mwananchi wa Wilaya ya Mkalama na Tanzania kwa ujumla  ni kwamba Wilaya ya Mkalama imeanza mchakato wa Ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu utakapokuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 45,000.

Uwanja huo bora kabisa na wa kisasa unaotarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.6 unajengwa katika kijiji cha Maziliga na tayari eneo hilo limeshasafishwa huku hatua ya kulisawazisha au kufanya ‘’levelling’’ kama inayojulikana kitaalam ikitarajiwa kufanyika Wiki ijayo.

Mbali na Mpira wa Miguu, uwanja huo utakuwa na viwanja vya ndani vya michezo ya Mpira wa Kikapu, Mpira wa ikono, Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu na sehemu ya Mashindano ya riadha.

Ujenzi huo unaoratibiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Mkalama chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Mhandisi Lameck Itungi  unatarajiwa kukamilika Julai 2019 ambapo zaidi ya matofali 5000 kati ya 27,000 yanayohitajika kwa ajili ya ujenzi wa Ukuta wa Uwanja huo yameshafyatuliwa.

Kwa Mujibu wa Mhe. Itungi jumla ya mali zinazokadiriwa kuwa na  thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 800 zimeahidiwa kutolewa  na  wadau mbalimbali ambapo kiasi kingine cha Fedha kinatarajiwa kukusanywa katika Harambee itakayofanyika septemba 9 mwaka huu.

“Mgeni rasmi katika harambee hiyo anatarajiwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson hivyo nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama na Watanzania kwa ujumla mjitokeze kuunga Mkono jitihada hizi za dhati kwa ajili ya kuendeleza sekta ya Michezo Mkalama na Tanzania kwa ujumla” Alisihi Mhe. Itungi.

Tuesday, 5 June 2018

Wajasiriamali Mkalama wanufaika

PICHA 10 CHINI:  WAWAKILISHI WA VIKUNDI 10 VYA UJASIRIAMALI  WILAYANI MKALAMA WAKIPOKEA HUNDI ZA MIKOPO YA RIBA NAFUU  KUTOKA KWA MKUU WA WILAYA YA MKALAMA MHE. MHANDISI JACKSON MASAKA JIONI YA LEO.Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka jioni la leo amevikabidhi vikundi 10 vya ujasiriamali hundi zenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 37.8  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo wa bajeti wa Serikali unayoitaka kila Halmashauri kutoa asilimia 10 ya fedha zake kuviwezesha vikundi vya wanawake na vijana mikopo ya riba nafuu.

Fedha hizo zimekabidhiwa kwenye vikundi 10, saba vya vijana na vitatu vya wanawake ambapo baada ya kukabidhi hundi hizo Mhe. Masaka alivitaka vikundi hivyo kuhakikisha vinatumia fedha hizo kufanyia shughuli za maendeleo ili viweze kupata faida na kurejesha fedha walizopewa ili watoe fursa ya vikundi vingine kukopeshwa kwa haraka.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga alisema kuwa fedha Halmashauri hiyo itaendelea kutoa fedha zaidi  kwa vikundi kulingana na ongezeko la mapato yake ya ndani.

MKALAMA yafanya DCC ya kwanza leo

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akihutubia wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akizungumza machache kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi  wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Wajumbe mbalimbali waliojitokeza akihutubia wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka leo ameongoza kikao cha kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC)  ambapo katika hotuba yake ametoa maelekezo mbalimbali kwa wadau na idara mbalimbali zilizopo Wilayani Mkalama.

Kikao hicho mbali na kuhusisha baraza lote la Madiwani, pia kilihusisha taasisi mbalimbali zinazoendesha shughuli zake Wilayni Mkalama, Watendaji wote wa kata, wawakilishi wa taasisi za dini na wawakilishi wa vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.

Mhe. Masaka aliwataka wananchi na viongozi kutambua umuhimu wa wingi wa fedha zinazotolewa na serikali katika kuhudumia Eimu nchini kwa kuhimiza watoto kwenda shule, walimu kufanya kazi pindi wawapo shuleni na wazazi kuonesha mwamko wakati wa kuchangia huduma mbalimbali za uboreshaji wa Elimu za watoto wao.

“Jambo la pili nitumie fursa hii kuhimiza wakulima wote walime mazao ya mkakati ambapo kwa Wilaya yetu mazao hayo ni pamba, korosho, alizeti na Vitunguu” Aliongeza Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka alisisitiza kuwa ili kilimo cha Mkakati kiweze kuwa na tija ni lazima wakulima watumie mbegu bora, wapande mazao yao kwa vipimo sahihi na watumie vipimo stahili katika uwekaji wa dawa za kuua wadudu wanaoathiri mazao hayo.

“Mawakala wa huduma za Misitu nchini (TFS) na idara ya Maliasili ni lazima waonekane wapo badala ya kuziachia serikali za vijiji  kesi za uvamizi wa maeneo ya misitu ingawa pia vijiji vyote vinapaswa kulinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya misitu” Aliongeza Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka alitumia fursa hiyo kusisitiza wananchi wajenge viwanda vidogo kama viwanda vya kukamua mafuta ya Alizeti na kuagiza kila mtu awaunge mkono wenye viwanda hivyo ili wafanikiwe na hatimaye waweze kufungua viwanda vikubwa.

“Sio Afisa afya anaenda kukagua kiwanda na kukuta mazingira yasiyoridhisha lakini badala ya kushauri namna ya kuboresha mazingira hayo anaamua kuchukua uamuzi wa kukifunga kiwanda hicho” Alisisitiza Mhe. Masaka.

Katika  hotuba yake Mhe. Masaka pia  alizitaka taasisi zote zinazofanya shughuli zake Wilayani Mkalama kuwa na mipango yenye mwelekeo mmoja ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za msingi kwa wakati badala ya huduma moja kusubiri uwepo wa huduma nyingine.

“Sio Tarura wanajenga barabara Kinyambuli, Halmashauri inaenda kujenga kituo cha Afya Gumanga, Tanesco wanapeleka umeme Kinyangiri na Idara ya Maji wanapeleka maji Ibaga, hapo mtakuwa hamjamsaidia mwananchi kwa sababu hata mkimpelekea kituo cha Afya kizuri, kama hakuna barabara nzuri kufika kwenye kituo hicho au umeme wa kutumia kituoni hapo itakuwa ni kazi bure” Alisema Mhe. Masaka.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Masaka aliwaomba wananchi na taasisi za dini zilizopo wilayani Mkalama kuisaidia serikali kwa kutoa maeneo ambayo hawayatumii ili yatumike katika shughuli za Maendeleo.

“Msiishie tu kumiliki maeneo hayo bila kuyaendeleza kwa kufanya shughuli za Maendeleo hivyo kama ni kilimo limeni, kama ni viwanda wekeni viwanda na kama mlipanga kuweka taasisi za Elimu wekeni taasisi hizo” Alimalizia Mhe. Masaka.
Friday, 18 May 2018

Elimu Mkalama ibadilike kwa vitendo-Nchimbi

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akisoma hotuba yake wakati wa kufunga maandhimisho ya Juma la Elimu, tukio lililofanyika leo mchana katika Viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama akiwasalimia wananchi wote waliofika kwenye kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu,tukio lililofanyika leo mchana katika Viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama. 

Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida Bi. Nelasi Mulungu akisoma jumla ya mambo mbalimbali yaliyoainishwa na timu ya wataalam wa  Wilaya ya Mkalama kwa kushirikiana na Mtandao wa Elimu Tanzania na wadau wengine mbalimbali wa Elimu kwenye kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu,tukio lililofanyika leo mchana katika Viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama. 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akiwa ameshikana mikono na  wageni waalikwa na wanafunzi wa shule ya Msingi Mbigigi kama ishara ya kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Juma la Elimu duniani isemayo "Uwajibikaji wa pamoja kwa Elimu bora kwa wote"


“Elimu ni moyo wa uhakika na hakikisho la uhai wa maendeleo endelevu ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla”

Hayo ni maneno yaliyotamkwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu tukio lililofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mhe. Nchimbi ambaye alimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wote wa elimu chini ya mwamvuli wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) ambapo aliwataka watumie maadhimisho ya mwaka ujao kutoa majibu ya tathmini ya utekelezaji wa changamoto zote walizoziona katika Wilaya za Nanyumbu na Mkalama.

“Haiwezekani kila mwaka muwe mnazungumzia changamoto za aina moja hivyo ni lazima muweke mpango mzuri wa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa changamoto zote mlizoziainisha” Alisisitiza Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi aliushukuru uongozi na wananchi wa Mkalama kwa ujumla kwa kuahidi kubadilisha matokeo waliyoyapata mwaka jana ambapo aliwasisitiza wajikite zaidi kwenye mabadiliko ya vitendo badala ya maneno.

Kabla ya kutangaza kufunga maadhimisho ya juma la Elimu kwa mwaka huu, Mhe. Nchimbi aliendesha harambee ya kuchangia elimu Wilayani hapa ambapo jumla ya shillingi 600,000 zilipatikana.

Awali akizungumza maneno machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka alisema kuwa TenMet waliamini Mkalama bado ipo hai ndio maana walifika kuisaidia kuainisha sababu mbalimbali zilizosababisha kutokuwa na matokeo mazuri ambapo aliwaahidi kuwa Wilaya yake haitofanya vibaya tena.

Wakati huo huo Mhe. Masaka alitumia fursa hiyo kuwatakia kila la kheri waislam wote wa Wilaya ya Mkalama katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo aliwataka wafanyabiashara wote Wilayani hapa kutopandisha bei za vyakula ambavyo hutumiwa kama futari na daku  katika kipindi hiki.

“Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itafuatilia kwa karibu sana utekelezaji wa agizo hili na atakayekiuka hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake” Aliongeza Mhe. Masaka.
HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA