Friday, 18 March 2016

SERIKALI: WACHEZA POOL KULIPA FAINI YA SHILINGI 300000Siku mbili tu baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama kutoa agizo kwa watendaji kutekeleza kwa vitendo amri ya Rais wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli ya Vijana kutocheza mchezo wa Pool muda wa asubuhi na kabla ya saa 10 jioni, hatimaye serikali kupitia Mkurugenzi wa bodi ya michezo ya kubahatisha, Abbas Tarimba (pichani juu) imetaja adhabu ya faini kwa wale watakaokiuka amri hiyo.

Akizungumza mchana wa leo, Tarimba amesema kuwa wachezaji wa mchezo huo hasa vijana sasa watalazimika kusubiri hadi saa 10 kamili jioni ndipo wacheze mchezo huo au wakubali kulipa faini ya shilingi laki tatu  (300,000) kama wakikiuka amri hiyo.

“Tumetayarisha barua ambazo zitatumwa kwa wakuu wa mikoa ili kuelekeza wananchi kanuni, sheria na taratibu za mchezo huo”.

Amesema kuwa barua hizo pamoja na matangazo yatakayotoka kwenye vyombo vya habari, yatatoa muongozo kwa wachezaji wa mchezo huo ambapo kwa siku za kazi utaanza saa 10:00 jioni mpaka saa 5:00 usiku na siku za mapumziko utaanza saa 8:00 mchana mpaka saa 6:00 usiku.

Tarimba amesema kuwa faini hiyo inatokana na sheria ya michezo ya kubahatisha (Gaming Act) kifungu cha 52 katika kifungu kidogo cha kwanza sura ya 42 inayosema asiye na kibali cha kuchezesha au atakayekiuka kanuni za mchezo huo atashtakiwa na akikutwa na hatia atalazimika kulipa faini ya shilingi 300000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote viwili.


No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA