Wednesday 5 October 2016

WATUMISHI MKALAMA WAPATA ELIMU YA "UKIMWI MAHALA PA KAZI"

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Injinia Jackson Masaka akifungua mafunzo yaliyopewa jina la "Ukimwi mahala pa kazi" mbele ya watumishi wa makao makuu ya halmashauri ya Wilaya ya mkalama (hawapo pichani) jana.

Kamanda wa Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa kanda ya Iramba na Mkalama Zacharia Mwandumbya akiwasilisha somo kuhusiana na Vitendo vya Rushwa ya Ngono inavyoweza kusababisha maambukizi ya virusi vya ukimwi mahala pa kazi.

Mratibu wa Ukimwi kutoka Manispaa ya Singida Dokta George Mwakahesya akiwasilisha somo zima linalohusiana na maambukizi, dalili na kinga dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.


PICHA TATU CHINI:  WATUMISHI WALIOPO MAKAO MAKUU YA HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA WAKIPATA MAFUNZO YALIYOPEWA JINA LA "UKIMWI MAHALA PA KAZI" MAPEMA JANA.







Mafunzo yanayojulikana kama “Ukimwi mahala pa kazi” yamefanyika jana katika halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambapo watumishi wote wa halmashauri walihudhuria na kupatiwa mafunzo hayo.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Injinia Jackson Masaka aliwataka watumishi wote kuwa makini  na kujiepusha na mazingira  ambayo yanaweza kuwasababishia maambukizi ya virusi vya ukimwi.

“Bahati mbaya watumishi wengi hapa hamuishi na wake zenu au waume zenu hivyo ni vyema muwe na tahadhari kubwa sana kutokana na mazingira mliyonayo”. Alisema Masaka.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Kamanda wa  Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kanda ya Iramba na Mkalama Zacharia Mwandumbya alisema ni vizuri wiongozi, wakuu wa idara na watumishi wote kwa ujumla kutotumia nafasi zao kuomba rushwa ya ngono kutoka kwa watu wanaohitaji huduma kwenye ofisi zao.

“Unakuta bosi ni wa kiume afu kuna msichana anahitaji huduma fulani katika ofisi yake lakini atazungushwa au kukataliwa kisa hajampa rushwa ya ngono, hilo ni kosa na Takukuru tukikubaini tutakukamata na kukukabidhi katika mamlaka nyingine zikuchukulie hatua Zaidi” Alisema Mwandumbya.

Aliongeza kuwa ni lazima watumishi wawe makini sana kwa sababu wanaweza kujikuta wanaomba rushwa ya ngono kwa watu ambao tayari wana maambukizi ya virusi vya ukimwi au wao wenyewe wanaweza kuwa tayari wana maambukizi hivyo kufanya hivyo ni sawa na kueneza zaidi ugonjwa huo.

Naye mratibu wa Ukimwi wa Manispaa ya Singida ambaye pia alikuwa ni muwasilishaji katika mafunzo hayo, Dokta George Mwakahesya alisema ni vyema kila mtu kupima na kujua afya yake ili kuepusha kufanyishwa kazi ambazo zitazidi kupunguza kinga ya mwili.

“Ukishajua una virusi vya ukimwi usiogope wala kusita kwenda kwa Afisa utumishi wako ili iwe rahisi kwake kutokukupa majukumu mazito sana lakini pia kukujibu kwa haraka pindi unapohitaji kwenda kufanya matibabu” Alisema Dokta Mwakayesya.


Alimalizia kwa kuwataka watumishi kutumia kinga kila wanapotaka kufanya tendo la ndoa ili kuepusha maambukizi ya virusi vya ukimwi maeneo yao ya kazi na pindi wakirejea nyumbani.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA