Friday 29 September 2017

Tatizo la Maji Mkalama litakuwa historia-Kamwelwe

Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe  (Kulia) akisalimiana na Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula mara baada ya kuwasili katika Mradi wa Maji wa Iguguno jana.

Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. Loth Kambi  mara baada ya kuwasili katika Mradi wa Maji wa Iguguno jana.

Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe akisalimiana na Diwani Viti Maalum  wa Kata ya Iguguno Mhe. Mariam Kahola  mara baada ya kuwasili katika Mradi wa Maji wa Iguguno jana.

Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe akisalimiana na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Lilian Kasanga  mara baada ya kuwasili katika Mradi wa Maji wa Iguguno jana.

Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe akifungua bomba ya maji kama ishara ya ufunguzi wa huduma ya maji katika kata ya Iguguno mapema jana

Wanafunzi wa shule ya sekondari Kikonda wakitoa ujumbe unaohusu utunzaji wa Mazingira na Vyanzo vya Maji mbele ya Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe mara wakati wa ukaguzi wa mradi wa maji uliopo katika kata ya Kikonda.

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe ameuhakikishia uongozi wa Wilaya ya Mkalama kuwa kufikia mwaka 2020 tatizo la Maji litakuwa historia katika Wilaya hiyo.

Mhe. Kamwelwe ameyasema hayo mapema jana wakati wa ziara yake ya Kikazi Wilayani Mkalama ambapo pamoja na mambo mengine amefurahishwa na kasi ya maendeleo ya Wilaya hiyo huku akiwapongeza Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mbunge wa jimbo la Mkalama kwa ushirikiano mkubwa walionao katika kuhakikisha Mkalama inapiga hatua siku zote.

“Mbunge wenu amekuwa akiniomba sana nifike huku ili nijionee changamoto ya Maji  na nilimhakikishia kuwa ntakuja tena nashukuru nimekuja kipindi cha kiangazi ili nijionee hali ya upatikanaji wa huduma ya maji wakati huu ambao maeneo mengi huwa ni makavu” Alisema Mhe. Kamwelwe.

Akiunga mkono wazo la Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambaye alimuomba fedha zinazotumika kuwekea miradi ya maji zitumike kuchimbia visima virefu badala ya kuendelea na miradi hiyo ambayo mbali na kuwa na gharama kubwa huchukua muda mrefu kukamilika na hutoa huduma kwa watu wachache, Mhe. Kamwelewe amesema kuwa kuanzia sasa fedha hiyo ambayo ni zaidi ya shilingi milioni 500 kwa mwaka zitatumika  kuchimba visima hivyo ili kufikia mwaka 2020 tatizo la maji katika Wilaya hiyo libaki kuwa historia.

“Katika kutekeleza hilo leo ntaacha visima virefu kumi ili tuwe tumeingia kwenye vitendo moja kwa moja huku kila awamu  tutakuwa tukitenga fedha ya kutosha kwa ajili ya kumaliza tatizo la Maji Mkalama” Alisema Kamwelwe.

Akiwa katika kijiji cha Kidarafa kilichopo kata ya Mwanga Mhe. Kamwelwe alivutiwa na maendeleo na mchango unaotolewa na kata hiyo katika uzalishaji wa chakula  na uingizaji wa pato la Wilaya ambapo alisema kuwa mfuko wa maji wa kijiji hicho ni mdogo sana ukilinganisha na gharama ya mafuta ya shilingi laki moja kwa siku jambo ambalo litasababisha jumuiya ya watumia maji wa kijiji hicho kushindwa kumudu gharama za uendeshaji wa mradi huo hivyo alimuagiza  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ampelekee gharama za kuunga umeme wa jua  ili wananchi hao waendelee kupata huduma hiyo ya maji.

“Ninataka baada ya kuweka mitambo ya sola gharama ya maji ishuke kutoka shilingi 50 kwa ndoo mpaka shilingi 20” Aliagiza Mhe. Kamwelwe.

Akimkaribisha  Mhe. Naibu waziri na kuwasilisha  taarifa ya hali ya huduma ya maji kwa Wilaya ya Mkalama Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka amesema kuwa mpaka sasa ni asilimia 43 pekee ya wananchi wa Wilaya hiyo wanaopata huduma  hiyo huku vyanzo vinavyotoa huduma hiyo vikiwa ni 186 kati ya 264 huku vyanzo 78 vikiwa havitoi huduma kutokana na sababu mbalimbali.

“Mhe. Naibu Waziri, Utekelezaji wa miradi mbalimbali Wilayani Mkalama unahusisha wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Serikali kuu pamoja na  Benki ya Dunia” Aliongeza Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka alihitimisha taarifa yake kwa kutaja changamoto mbalimbali zinazoathiri ufanisi wa utoaji wa huduma ya maji Wilayani Mkalama ambazo ni pamoja na Ukosefu wa Vitendea kazi, ufinyu wa bajeti na uchache wa watumishi wa idara ya maji.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula alimshukuru Mhe. Waziri kwa kukubali ombi lake na kufika Mkalama ambapo alimhakikishia kuwa ataendelea kushirikina na Wizara yake bega kwa bega ili kuhakikisha malengo ambayo Wizara imeweka juu ya Wilaya ya Mkalama yanatimia.


“Mimi ni Mwakilishi wa wananchi hivyo kila changamoto nayopewa ni lazima niifikishe kwa watendaji na matokeo yake ndio haya na ntajitahidi kuhakikisha  kila Waziri anayehusika na changamoto zilizopo Mkalama anafika hapa ili kujionea mwenyewe hali halisi” Alimalizia Mhe. Kiula.

Muone Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega wakati akizungumza katika kata ya Kikonda jana kwa kubonyeza hapa

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA