Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa ndugu Amour H. Amour akisoma ujumbe uliowekwa katika mradi wa Ujenzi wa bweni, bwalo la chakula na choo katika shule ya sekondari Iguguno. |
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa ndugu Amour H. Amour akizungumza na wananchi mara baada ya kuanza kwa mbio za Mwenge Wilayani Mkalama. |
Siku ya jumatatu ya wiki hii (Julai 3,2017) Wilaya ya
Mkalama ilikimbiza Mwenge wa Uhuru baada ya kuupokea kutoka Wilaya ya Iramba
ambapo ulikimbizwa katika Miradi 7 iliyopo Wilayani hapa huku minne ikiwa ni ya kuwekwa jiwe la msingi,
miwili ya kuzinduliwa na mmoja wa kukaguliwa/kuonwa.
Miradi hiyo ni pamoja na wa ujenzi wa bweni kubwa la wanafunzi, bwalo
la chakula na vyoo unaoendelea katika shule ya sekondari Iguguno, mradi wa maji
safi uliopo katika kijiji cha Mnolo, Mradi wa Kiwanda cha kukamua mafuta ya
alizeti na ufugaji wa nyuki uliopo katika kijiji cha Kinyangiri, mradi wa
Ujenzi wa Ukumbi mkubwa wa Mikutano na hadhara mbalimbali uliopo katika Ofisi
za Halmashauri ya Wilaya katika kijiji cha Nduguti, mradi wa ujenzi wa barabara
ya Kijiji cha Mwando mpaka kijiji cha Nkalakala na mradi wa soko la Vitunguu uliopo katika
kijiji cha Dominiki.
Jumla ya gharama ya miradi yote hiyo mpaka kukamilika
kwake ni shilingi 5,197,865,111 ambapo
michango iliyotolewa kupitia nguvu za wananchi ni shilingi 35,770,000 huku fedha iliyotolewa na
serikali kuu ikiwa ni shilingi 1,694,878,769 Upande wa Halmashauri ya Wilaya imetoa shilingi 9,580,000 huku wahisani wakitoa
shilingi 467,045,111.
Katika miradi yote
hiyo Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Ndugu Amour H. Amour amesisitiza juu ya
matumizi bora ya fedha za serikali ambapo aliagiza miradi yote ilingane na
thamani ya pesa iliyotumika kuikamilisha.
“Niwapongeze sana kwa kuwa na jengo zuri na kisasa kuliko
yote katika Maeneo ambayo Mwenge umeshapita na naomba nisisitize juu ya utoaji
huduma bora zenye kufuata weledi kwa
wananchi ili thamani na uzuri wa jengo hili uendane na huduma wanazopata
wananchi huku mkizingatia kuwa madaraka mliyonayo yanatokana na uwepo wa
wananchi hawa” Aliongeza Amour.
Akiwa katika mradi
wa ujenzi wa bweni, bwalo na vyoo ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni
400, katika shule ya Iguguno Amour
alisifu jitihada zilizofanywa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya kupitia
uongozi wa Shule hiyo kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo pekee
yenye wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika Wilaya ya Mkalama wanakuwa na
mazingira mazuri kuanzia sehemu ya kula mpaka kulala ambapo aliwataka wanafunzi
hao kusoma kwa bidii.
Mara baada ya
kumaliza mbio zake katika Wilaya ya Mkalama, Mwenge wa Uhuru ulikabidhiwa
katika Mkoa wa Simiyu makabidhiano yaliyofanyika katika kijiji cha Bukundi
wilayani Meatu siku ya Jumanne Julai 4, 2017.
Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2017 umebeba ujumbe unaosema “Shiriki
Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu”
No comments:
Post a Comment