Mgeni rasmi wa ufunguzi wa Maonesho ya NaneNane kwa kanda ya kati Mhe: Daktari Rehema Nchimbi akifuatilia burudani muda mfupi baada ya kufika katika eneo la Sherehe. |
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe: Jordan Rugimbana akizungumza machache muda mfupi kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi wa Ufunguzi wa Maonesho ya 21 ya NaneNane kwa kanda ya kati Dodoma. |
Maadhimisho ya 21 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji
maarufu kama NANENANE yamefunguliwa rasmi leo kwa kanda ya kati inayojumuisha
mikoa ya Singida na Dodoma.
Mgeni rasmi katika Ufunguzi huo alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa
Singida Mhe: Daktari Rehema Nchimbi ambaye alitumia muda usipungua dakika 45
kusisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kilimo na ufugaji wenye tija ili kuendana na falsafa ya serikali ya
awamu ya Tano nayohimiza zaidi Uchumi wa Viwanda.
Mhe: Nchimbi amesema kuwa ni vizuri maadhimisho ya Mwaka
huu yakaonesha mabadiliko chanya kwa washiriki waliojitokeza katika kuonesha
bidhaa mbalimbali na wale waliofika kwa ajili ya kununua au kupata maelezo ya
matumizi ya bidhaa hizo.
“ Nimepita kwenye banda la Jeshi la Magereza na kuona
bidhaa nyingi sana zilizotengenezwa na Ngozi na wamenihakikishia kuwa kiwanda
chao kina uwezo wa kununua ngozi yote inayopatikana katika Mikoa ya Singida na
Dodoma hivyo ni vizuri tutumie hiyo kama fursa” Aliongeza Mhe: Nchimbi.
Mhe: Nchimbi ameliomba Jeshi la Magereza na wawekezaji
wote wa ndani nan je ya Nchi wafike kuwekeza katika mikoa ya Singida na Dodoma na
kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma watahakikisha wanatengeneza
mazingira rafiki kwa kila atakayekuwa tayari kuwekeza katika Mikoa hiyo.
“Kila siku huwa nasisitiza Mikoa ya Singida na Dodoma
haina ukame na ndio maana hivi sasa tunataka kuanzisha mpango maalum wa kilimo
cha umwagiliaji kwa sababu watafiti wameshatuhakikishia mikoa hii ina kiwango
kikubwa sana cha maji ardhini tena yapo karibu sana na uso wa ardhi”
Alisisitiza Mhe: Nchimbi.
Katika hatua nyingine Mhe: Nchimbi amewataka wananchi wa
Mikoa ya Singida na Dodoma kuacha kabisa kukata miti kwa kisingizio cha
kujikwamua kiuchumi kwa sababu kuna njia nyingi sana za kuondokana na hilo
badala ya kuharibu misitu.
“Kule Singida nimeanzisha kampeni inayojulikana kama ‘ACHIA
SHOKA, KAMATA MZINGA’ ambayo inampa mwananchi nafasi ya kuamua kuacha kukata
mti na badala yake anafuga nyuki jambo linalomsaidia kujikwamua kiuchumi kwa
muda mrefu zaidi kwa sababu unaweza kuukata mara moja tu lakini mzinga unaweza
kuutundika mara nyingi kadri uwezavyo” Alisema Mhe: Nchimbi
Mhe: Nchimbi alimalizia hotuba yake kwa kuwasisitiza
maafisa kilimo kupeleka kalenda za kilimo katika ngazi zote kuanzia ngazi ya
kijiji ili iwe rahisi kwa Mkulima kujua aina ya mazao anayoweza kulima kwa
Mwaka husika badala ya kumsubiri Mkulima apate madhara kwanza ndipo aje apewe elimu ya mazao aliyotakiwa
kulima kwa mwaka husika.
No comments:
Post a Comment