Mkuu wa Mkoa wa Singida (kushoto) akitoa maelekezo kwa viongozi wa mamlaka ya Bonde na viongozi wa Wilaya ya Mkalama juu ya namna bora ya utunzaji wa mazingira. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akimuelezea jambo Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi katika kituo cha upimaji wa wingi wa maji kijiji cha Iambi. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida na Viongozi waandamizi wa Wilaya ya Mkalama wakishiriki Ufunguzi wa Darasa la kisasa lililojengwa na Shirika la 'Norwegian Church Aid' katika kijiji cha Munguli jana |
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi (Kushoto mbele) akiwa ndani ya darasa lililojengwa na Shirika la 'Norwegian Church Aid' mara baada ya kulifungua jana katika kijiji cha Munguli. |
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akiwaasa wananchi wa kijiji cha Munguli juu ya umuhimu wa kutumia vyema fursa wanazozipata. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akizungumza machache muda mfupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida katika kijiji cha Munguli Jana. |
Viongozi waandamizi wa Kanisa la Hydorm na wawakilishi wa shirika la 'Norwegian Church Aid' wakipokea cheti kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida. Cheti hicho kimetolewa na Uongozi wa Wilaya ya Mkalama kama ishara ya kushukuru kwa mchango uliotolewa na Shirika hilo Wilayani hapa. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama pamoja wawakilishi wa Shirika la 'Norwegian Church Aid' kutoka Nchini Norway jana katika kijiji cha Munguli. Nyuma yao ni paneli za Sola zinazohakikisha upatikanaji wa maji kijijini hapo Muda wote. |
“Kuanzia sasa jukumu la kukusanya na kusimamia michango ya
aina yoyote ile shuleni lifanywe na wazazi wa wanafunzi hao kupitia bodi za
shule badala ya walimu na kuanzia sasa mwalimu haruhusiwi kumrudisha nyumbani
mwanafunzi mwenye upungufu wa mahitaji ya shule na badala yake amshirikishe
mzazi juu ya umuhimu wa mahitaji hayo ili mzazi kwa hiyari yake aweze kutimiza
majukumu yake ya msingi kwa mwanae akiwa shuleni”
Hayo ni maneno yaliyozungumzwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema
Nchimbi alipokuwa katika ziara yake Kijiji cha Munguli mapema jana ambapo
alifika kwa ajili ya kukagua mradi mkubwa wa Maji na kuzindua darasa la kisasa
la shule ya Msingi Munguli na Ofisi ya Walimu miradi yote ikiwa imewezeshwa na Mashirika
yasiyo ya kiserikali kutoka nchini Norway yanayojulikana kama ‘Norwegian Church
Aid’ (NCA) na ‘4 corners Cultural Program’ (4CCP).
Mhe. Nchimbi ameyapongeza mashirika hayo kwa kuwezesha
ujenzi wa miradi mikubwa katika kijiji cha Munguli ambapo aliongeza kuwa undugu
huo kati ya Wilaya ya Mkalama na mashirika hayo unapaswa kuenziwa kwa njia ya
utunzaji bora wa miradi hiyo ili kuwapa nguvu wafadhili hao kuendelea kuboresha
miundombinu mingine iliyopo Wilayani hapa.
“Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwenu na mimi
huwa napenda kusema kuwa kushukuru ni kuomba tena hivyo ninawaomba kama
ilivyowapendeza kwa upande wa Munguli Magharibi, muiangalie Munguli Mashariki
kwa jicho hilo hilo kwani nao wanahitaji sana miradi mliyoiweka hapa kwa
wenzao” Aliongeza Mhe. Nchimbi.
Suala la upandaji wa Miti ya Korosho na matumizi mazuri ya
Fedha zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ni moja ya mambo
yaliyosisitizwa na Mhe. Nchimbi katika hotuba yake kijijini hapo ambapo
aliagiza wakuu wa shule zote za Msingi na Sekondari kuhakikisha wanapanda korosho
katika mashamba ya shule zao na walengwa wote wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
wanatumia fedha hizo kujikwamua kiuchumi badala ya kuzitumia kwenye ulevi na
anasa nyingine.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya
Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka
aliyashukuru Mashirika ya NCA na 4CCP kwa kuwezesha miradi hiyo mikubwa
Wilayani kwake ambapo aliwaagiza wananchi wa Kijiji hicho kuhakikisha hawafanyi
shughuli za kiuchumi katika maeneo yaliyo karibu na mradi wa Maji ili kuweza
kuulinda mradi huo.
Kwa upande wake Afisa Miradi wa Mashirika ya NCA na 4CCP
Nelson Faustineamewashukuru viongozi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
kwa ushirikiano Mkubwa waliouonesha katika kipindi chote cha Ujenzi wa Miradi
hiyo jambo ambalo alikiri kutolipata kwa kiwango hicho katika maeneo mengine yote waliyotekeleza
miradi yao.
“Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mkalama wametuonesha ushirikiano mkubwa sana na ilifikia hatua tulikuwa
tunawapigia simu muda wowote tunaaohitaji msaada wao na wao hawakusita
kutusaidia” Alisisitiza Faustine.
Mashirika ya NCA na 4CCP yametekeleza miradi hiyo kwa kushirikiana na Kanisa la Kilutheri la
Hydom lililopo Wilayani Mbulu Mkoani Manyara.
No comments:
Post a Comment