Kaimu Afisa Elimu wa Wilaya ya Mkalama Bi. Rose Kibakaya (katikati) akifafanua jambo wakati wa ziara ya kamati ya Fedha, Mipango na Utawala katika shule ya Msingi Kibololo juzi. |
Wajumbe wa kamati ya Fedha, Mipango na Utawala wakikagua jengo la bweni la wanafunzi wa shule ya sekondari Iguguno linaloendelea kujengwa na mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). |
Kamati ya Fedha, mipango na Utawala kutoka Halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama imefanya ziara yake juzi na jana ambapo ilitembelea miradi
mbalimbali ya Maendeleo hususani inayohusu sekta ya Elimu na Maji.
Ziara hiyo ilihusu vijiji vya Nduguti Makao Makuu ya Halmashauri
unapoendelea mradi wa Ujenzi wa Ukumbi
bora na wa kisasa wa Mikutano, kijiji cha Ishenga inapopatikana shule ya watoto
wenye mahitaji maalum, Kijiji cha Kinyangiri ulipofanyika ujenzi wa Bweni la
kisasa la wasichana katika shule ya sekondari ya Kinyangiri, Kitongoji cha
Kibololo yanapojengwa madarasa ya kisasa na vyoo vya Shule ya Msingi Kibololo,
Kijiji cha Iguguno linapojengwa bweni la wanafunzi wa Shule ya Sekondari
Iguguno, Kijiji cha Senene yanapojengwa madarasa na vyoo vya Kisasa katika shule
ya Msingi Senene, Kijiji cha Tumuli yanapojengwa madarasa ya kisasa ya Shule ya
Sekondari ya Tumuli,Kijiji cha Kitumbili yanapojengwa madarasa katika shule ya
Msingi Kitumbili, Kijiji cha Mgolombyo yanapojengwa madarasa ya Shule shikizi
ya Mgolombyo na Kijiji cha Nyahaa unapojengwa mradi wa Maji wa Kijiji hicho.
Katika vijiji vyote ambavyo Kamati imepita pamoja na mambo
mengine, wajumbe wa kamati wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Mkalama Mhe. James Mkwega waliagiza Kamati za Shule zijikite zaidi katika
kuinua taaluma badala ya kushughulika na matumizi ya fedha za shule pekee.
Pia kamati ilitoa onyo kwa walimu wote wanaokunywa pombe
muda ambao wanapaswa kuwa darasani ambapo iliwaagiza viongozi wa vijiji
kuwakamata walimu hao na wale wote wanaokunywa nao na kuwafikisha katika vituo
vya polisi ili iwe fundisho kwa walimu wengine wenye tabia kama hiyo.
Mbali na walimu wanaokunywa pombe muda wa kazi, Kamati
hiyo pia imepiga marufuku wanafunzi wote katika Wilaya ya Mkalama kutoonekana
katika kumbi za starehe, kukesha katika kumbi za televisheni wakiangalia mpira
na kutumia simu za Mkononi wakati wote
wakiwa shuleni au nyumbani ambapo Mwanafunzi atakayebainika kupuuza agizo hilo
atachukuliwa hatua yeye pamoja na Mzazi wake.
Wakihitimisha ziara yao katika kijiji cha Nyahaa, wajumbe
wa kamati walioneshwa kusikitishwa na kasi ya Mkandarasi katika utekelezaji wa
mradi wa maji wa kijiji hicho jambo lililolalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu
ambapo walitoa agizo kwa Mkandarasi huyo kukamilisha mradi huo ifikapo Mwisho
wa Mwezi huu vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Ziara za kamati mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya
Mkalama hufanyika mara kwa mara huku lengo kuu likiwa ni kufika na kukagua
maeneo yote yenye miradi iliyogharamiwa na serikali na wadau mbalimbali wa
maendeleo.
No comments:
Post a Comment