Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Daktari Deogratius Masini akimvalisha miwani ya jua kijana Daudi Daudi muda mfupi baada ya kukabidhiwa vifaa vyake. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Mhandisi Jackson Masaka(Mwenye suti Kulia) akikabidhi msaada wa nguo kwa wahanga wa ugonjwa wa Ukoma katika kijiji cha Nkungi mapema jana. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Mhandisi Jackson Masaka (mwenye suti katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wahanga wa ugonjwa wa Ukoma katika kijiji cha Nkungi. |
Diwani wa Kata ya Ilunda Mhe. Mohamedi Imbele akiwa na baadhi ya wahanga wa ugonjwa wa Ukoma maarufu kama 'wakoma' katika kijiji cha Nkungi mapema jana. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka
jana alitoa msaada wa chakula na mavazi kwa wahanga wa ugonjwa wa ukoma maarufu
kama ‘wakoma’ wanaoishi katika kijiji cha Iambi Wilayani Mkalama.
Msaada huo umetokana na jitihada za dhati za Mhe. Masaka
za kutafuta wadau mbalimbali wa kuwasaidia wahanga hao na unajumuisha magunia 18 ya mahindi na
viroba vitatu vya nguo ambazo hazijachakaa.
“Shukrani zangu za dhati ziende kwa kanisa la EAGT, kanisa
la Maranatha,kanisa la KKKT wanzelya lililopo hapa Nkungi na watu binafsi ambao wametoa na wanaendelea
kutoa michango mbalimbali kwa ajili ya
wahanga hawa” Alisema Mhe. Masaka.
Naye Mwenyekiti wa shirika lisilo la serikali
linalowasimamia wahanga hao (CHADEREREKO) bw. Martin Nakomolwa amemshukuru Mhe. Masaka kwa jitihada zake za
dhati za kuwasaidia wahanga hao na kuongeza kuwa hakuna Mkuu wa Wilaya ambaye
amewahi kusimamia kikamilifu jambo hilo zaidi yake.
“Wote hapa ni mashahidi kuwa wamepita wengi katika Wilaya
hii lakini hakuna aliyewahi kuguswa na suala la wakoma kwa kweli Mungu aendelee
kukudumisha katika Wilaya yetu” Aliongeza Nakomolwa.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Diwani wa kata ya Ilunda
Mhe. Mohamedi Imbele amesema kuwa ni vyema misaada hiyo ikatumiwa na walengwa
ili kuweza kutimiza haja ya wote waliojitolea kuwasaidia wahanga hao.
“Lakini mimi pia ntakuwa mchoyo wa fadhila kama
sitamshukuru Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mkalama kwa kazi nzuri anayoifanya katika
Wilaya yetu hasa kupigania haki za wanyonge jambo ambalo ndio hasa muelekeo wa
serikali ya awamu hii” Alimalizia Mhe. Imbele.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi
Jackson Masaka alitumia nafasi hiyo kugawa vifaa mbalimbali kwa watu wawili
wenye albinism ambapo jumla ya kofia za kujikinga na jua nne, Mafuta maalum ya
ngozi, miwani pea nne iligawiwa kwa watu hao.
Ili kumuona na kumsikia Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka wakati akizungumza jana tafadhali bonyeza hapa
No comments:
Post a Comment