|
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka akitoa maelekezo juu ya ufungashaji sahihi wa vitunguu ambao utamtendea haki Mkulima. |
|
Afisa Kilimo na Ushirika wa Wilaya ya Mkalama Bw. Cuthbert Mwinuka (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa dereva wa lori aina ya Fuso ambalo lilipakia Vitunguu katika ufungashaji usiokubalika. |
|
Meneja wa Wakala wa vipimo wa Mkoa wa Singida, Bw. Albogast Kajungu akiwaonesha wakulima na wafanyabiashara mfano wa gunia linalotakiwa kutumika kwa ajili ya kufungashia mazao. |
PICHA MBILI CHINI NI JINSI VITUNGUU VILIVYOKUWA VIMEFUNGASHWA KATIKA KIJIJI CHA DOMONIKI.
|
Kiasi cha Vitunguu vilivyobaki baada ya kupima ujazo unaotakiwa kwa mujibu wa sheria kwa ujazo wa gunia moja.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe: Mhandisi Jackson Masaka leo amefanya ziara ya
kushtukiza katika kijiji cha Dominic kwa
ajili ya kukagua ujenzi wa soko la Vitunguu na kuchunguza ufungashaji wa
vitunguu hivyo kwenye mifuko kabla ya kupelekwa sokoni ambapo amebaini
udanganyifu mkubwa unaofanywa na wafanyabiashara wanapofika mashambani.
Akiwa katika shamba la Mkulima mmoja aliyejulikana kwa
majina ya Richard isaya, Mhe: Masaka ameshuhudia mfanyabiashara mmoja akiwa
anapakia vitunguu ambavyo ameviweka kwenye ujazo wa zaidi ya Kilo 130 kwa gunia
kinyume kabisa na sheria na taratibu za ufungashaji wa mazao ya Vitunguu ambapo
mnunuzi anapaswa kufungasha ujazo wa Kilo 100 hadi 105 kama vitunguu hivyo
vitakuwa havijakauka vizuri.
“Sitaki kuingilia makubaliano ya bei mliyokubaliana lakini
sipo tayari kuona Mkulima akikandamizwa kiasi hiki kwa sababu ametumia nguvu,
fedha na muda mwingi mpaka kufikia hatua
ya kuvuna na pia utaratibu huu unaifanya halmashauri kupoteza mapato kwa kiasi
kikubwa sana” Amesema Masaka.
Mhe: Masaka ameongeza kuwa kila mfanyabiashara anayeingia
katika Wilaya ya Mkalama ni lazima afuate sheria ndogondogo na taratibu
zilizowekwa katika Wilaya hiyo na kamwe asilinganishe taratibu za Mkalama na
maeneo mengine kwa sababu kila Wilaya ina Mkuu wake wa Wilaya na ana utaratibu
wake wa kuongoza.
Kufutia tukio hilo, Mhe: Masaka aliagiza vitunguu hivyo
vitolewe kwenye mifuko hiyo na kupimwa upya katika ujazo unaokubalika
kisheria na mfanyabiashara huyo alipe
ushuru hapo hapo shambani kabla hajasafirisha mazao yake.
Naye Meneja wa wakala wa Vipimo Mkoa wa Singida, Bw. Albogast Kajungu amesema
kuwa ufungashaji wa mazao kwa kutumia mifuko ya aina yoyote tofauti na gunia la
katani ni kinyume na sheria na kutokana na mabadiliko ya sheria yaliyofanyika
hivi karibuni kutenda kosa hilo hakumuweki hatiani mfanyabiashara pekee bali
mpaka dereva anayesafirisha mazao hayo.
“ Lakini pia wakulima waepuke kupima mazao yao kwa kutumia
vifaa vya plastiki kama vile ndoo na visado kwa sababu vyombo hivyo vikipata
joto hutanuka na kuongeza ujazo wa mazao jambo ambalo ni udanganyifu na kinyume
na sheria ya ufungashaji mazao” Alimalizia Kajungu.
Ni kwa muda mrefu hivi sasa wakulima wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama wamekuwa wakiwaruhusu wafanyabiashara kufungasha mazao
shambani kwa kutumia nyavu huku wafanyabiashara hao wakidai kutumia chombo
kingine kinyume na hapo kunawakosesha soko hasa wanaposafirisha mazao hayo
katika nchi za jirani kama Kenya na Uganda.
|
No comments:
Post a Comment