PICHA MBALIMBALI ZIKIMUONESHA MKUU WA MKOA WA SINGIDA MHE: REHEMA NCHIMBI AKIWA AMEAMBATANA NA VIONGOZI MBALIMBALI WA MKOA NA WILAYA KATIKA ZIARA YAKE WILAYANI MKALAMA JANA.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe: Rehema Nchimbi jana
alifanya ziara Wilayani Mkalama ambapo alitembelea na kukagua miradi mbalimbali
na kuzindua zoezi la madaktari bingwa linaloendelea katika hospitali ya Iambi.
Mara baada ya kufika katika hospitali ya Iambi, Mganga
Mkuu wa Mkoa Dokta John Mwombeki alimsomea Mhe: Nchimbi taarifa fupi ya zoezi hilo na jinsi
lilivyofanyika katika Mkoa wa Singida ambapo taarifa hiyo ilieleza namna zoezi
hilo lilivyofanyika kwa mafanikio huku likitarajiwa kuhitimishwa katika Wilaya
ya Mkalama.
“Mpaka sasa jumla ya watu 675 wameonwa na madaktari
bingwa na 71 kati yao wamefanyiwa upasuaji” Alisema Mwombeki.
Akizungumza mara baada ya kusomewa taarifa, Mhe: Nchimbi
alimpongeza Mganga Mkuu wa Mkoa na timu yake kwa kufanikisha kufanyika kwa
zoezi hilo ambapo alizitaka Halmashauri zote Mkoani Singida kuangalia namna ya
kupata shilingi Milioni 18 kila Mwaka kwa ajili ya huduma za madaktari bingwa.
“Halmashauri zisisubiri kufuatwa na Mkoa kwa ajili ya
zoezi hili bali ziandae ratiba na kuziwasilisha Mkoani ili zoezi hili liwe
endelevu” Alisema Mhe: Nchimbi.
Aliongeza kuwa utengenezwe mfuko maalum kwa ajili ya
zoezi hilo ili pesa inayopatikana katika mazoezi ya madaktari bingwa iwekwe
humo kwa ajili ya kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu.
Kabla ya kuzindua zoezi la Madaktari bingwa, Mhe:
Nchimbi alitembelea Chuo cha Maendeleo ya Jamii kilichopo katika kata ya
Gumanga ambapo aliiagiza halmashauri ya Wilaya ya Mkalama iandae taarifa ya
miaka mitano ya chuo hicho.
“Halmashauri ni lazima ikichukue chuo hiki na ihakikishe
kinapata wanafunzi wa kutosha na viongozi wa Chuo ni lazima wabadilike na kutoa
mapendekezo mazuri ya uendelezaji wa Chuo hiki”. Alisema Mhe: Nchimbi.
Alisema kuwa Mkoa na Halmashauri watumie chuo hicho kama
sehemu ya mafunzo kwa watendaji wa kada zote na kisigeuzwe shule ya kidato cha tano kama ilivyopendekezwa bali halmashauri itafute mahali pengine na
kuhakikisha inakuwa na shule ya ngazi ya kidato cha tano mwaka huu.
Alihitimisha kwa kuziagiza halmashauri zote Mkoani
Singida kununua camera na vifaa vingine vya kisasa vitakavyowawezesha maafisa
habari kufanya kazi zao kwa ufanisi badala ya kuwaacha wataalam hao kuendelea
kutumia vyombo binafsi.
“Haiwezekani hawa wataalam wa serikali kuendelea kutumia
vyombo binafsi, vyombo vina “filosofia” zao , tuwe na matukio yetu tuyaandae na
kuyatangaza kwa sababu moja ya vitu vikubwa vinavyochagiza maendeleo ni kupata
taarifa au habari” Alimalizia Mhe” Nchimbi.
No comments:
Post a Comment