Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari John Pombe Magufuli akiwaongoza viongozi mbalimbali zoezi la uwekaji jiwe la msingi la daraja la mto Sibiti mapema leo. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari John Pombe Magufuli akiwaaga wananchi waliojitokeza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi daraja la Sibiti mapema leo. |
Sehemu ya umati wa watu uliojitokeza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la daraja la mto Sibiti iliyofanyika mapema leo darajani hapo. |
“Haiwezekani ujenzi
wa daraja uchukue zaidi ya miaka sita wakati mkandarasi analipwa stahiki zake
zote kwa wakati tena kwa kutumia kodi za Watanzania hivyo daraja hili ni lazima
likamilike ifikapo mwezi machi mwakani, Wizara mjipange kweli kweli kwa sababu
tutafukuzana hapa hapa na kuanzia sasa hivi nalifanya kuwa kipaumbele changu namba
moja kwa kulifuatilia hivyo ntapiga simu usiku na mchana ili kujua limefikia
wapi”
Ni kauli iliyotolewa mapema leo na Rais wa jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari John
Pombe Magufuli wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi la Mto Sibiti baada
ya kutofurahishwa na kasi ya mkandarasi
anayejenga daraja la mto huo huku pia
akizikataa sababu mbalimbali za uchelewaji huo zilizotolewa na Mkurugenzi Mtendaji
wa wakala wa barabara wa Taifa (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale na Waziri wa
Miundombinu na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwelwe.
“Waziri kama unaona mkandarasi huyu hana uwezo wa
kumaliza kazi hii kwa wakati ni bora utafute mkandarasi mwingine kwa sababu
sina uhakika hata kama mkandarasi huyu ana vifaa vya kutosha kumaliza kazi hii
na huenda hata hivi navyoviona hapa vimeletwa jana usiku baada ya kusikia
ninakuja leo” Aliongeza Mhe. Magufuli.
Mhe. Magufuli aliwaagiza wenyeviti wa bodi ya wakandarasi
na washauri wa wakandarasi kuwasimamia ipasavyo mkandarasi na mshauri wa
mkandarasi wa daraja hilo na kama
wataonekana kufanya kazi chini ya kiwango wachukuliwe hatua kwa mujibu wa
taratibu za bosi hizo.
“Nyie ‘consultants’
mnapaswa kujua mpo hapo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na najua nyie
ni wafanyabiashara but this is not a good business for you so watch out’’ Alionya Mhe. Magufuli.
Katika hotuba yake Mhe. Magufuli aliieleza halaiki ya
wananchi waliojitokeza katika tukio hilo kuwa baada ya kukamilika kwa daraja
hilo uchumi wa Mikoa ya Singida na
Simiyu utaimarika zaidi kwa sababu utawapa fursa wananchi wa pande hizo mbili
kufanya biashara ya rasilimali wanazozalisha.
“Waziri wa Madini amesema hapa kuwa Mkoa wa Simiyu una
chumvi nyingi sana kwa hiyo nategemea kukamilika kwa daraja hili kutachochea
uchimbaji zaidi wa chumvi hiyo ambapo kiwango kikiridhisha tunaweza hata
kuongeza kodi ya uingizaji wa chumvi ya nje ili kuongeza matumizi ya chumvi
tunayozalisha wenyewe hapa ndani” Alisisitiza Mhe. Magufuli.
Mhe. Rais alihitimisha hotuba yake kwa kumpongeza Mbunge
wa Mkalama Mhe. Allan Kiula kwa ushirikiano mzuri alionao dhidi ya wanasiasa
wenzake ndani ya Wilaya na wataalam wote wa Wilaya hiyo ambapo alimtaka
kuendeleza ushirikiano huo ili kuzidi kuongeza maendeleo ya Wilaya hiyo.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa
Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi alimshukuru Mhe. Magufuli kwa ujenzi wa
daraja hilo ambapo alimhakikishia kuwa tayari Mkoa wa Singida umejipanga kuhusu
matumizi sahihi ya daraja hilo na mkakati wa utunzaji wa mazingira yanazunguka
daraja hilo umeshakamilika.
“Mhe. Rais ninakushukuru kwa sababu hivi sasa maji ya ziwa
Victoria yatakayopita Simiyu yatafika mpaka Singida kupitia Mkalama” Alisema
Mhe. Nchimbi.
Mpaka sasa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imetumia zaidi ya shilingi bilioni 2002 za mapato yake ya ndani katika
kuboresha na kutengeneza miundombinu ya barabara huku daraja la Sibiti
likigharimu jumla ya shilingi bilioni 16 mpaka kukamilika kwake ambapo kwa sasa
limefikia asilimia 70 na kugharimu shingi bilioni 15.
No comments:
Post a Comment