Katibu Mwenezi wa Umoja wa Wakazi wenye asili ya Wilaya ya Iramba na Mkalama daktari Alfred Mdima (Kushoto) akimkabidhi jezi Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka huku akishuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mhandisi Godfrey Sanga, Afisa Elimu Msing Bw. Chacha Kehogo na Mwenyekiti wa Umoja huo Bw. Joseph Nsoza (kulia). |
Viongozi na wajumbe wa Umoja wa Wakazi wenye asili ya Wilaya ya Iramba na Mkalama (IDA) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka baada ya kukamilika kwa hafla ya kukabidhi jezi za timu ya Wilaya inayoshiriki michezo ya Umitashumta ngazi ya Mkoa. |
Umoja wa Wakazi wenye asili ya Wilaya ya Iramba na Mkalama
(IDA) umetoa msaada wa jezi pea mbili kwa timu ya Wilaya ya Mkalama
inayotarajia kushiriki mashindano ya
Umitashumta katika ngazi ya Mkoa.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya
Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka
ambaye pia ndo alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo fupi, aliwashukuru
wajumbe wa umoja huo kwa uzalendo waliouonesha kwa timu hiyo na kuongeza kuwa
si rahisi kwa watu walioondoka katika maeneo yao ya asili kukumbuka kupeleka
misaada katika maeneo yao.
“Binafsi kwa kuteuliwa tu kuwa Mkuu wa Wilaya tayari
nimeshakuwa mwanachama wa Umoja huu ndio maana nahakikisha Wilaya ya Mkalama
inasonga mbele katika Nyanja zote” Alisema Masaka.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi
Godfrey Sanga ametoa rai kwa watu wengine kuiga mfano uliooneshwa na Umoja huo
na kuongeza kuwa wamefanya jambo la kizalendo sana na linalopaswa kuenziwa.
“ Tunaomba msiishie hapa tu bali tuendelee kushirikiana
katika kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Mkalama” Aliongeza Sanga.
Naye Mwenyekiti wa Umoja huo Bw. Joseph Nsoza alisema kuwa
amefarijika sana kwa jinsi Wilaya ya Mkalama ilivyopiga hatua hali ambayo ni
tofauti kabisa na kipindi walipokuwa wanaondoka na kuupongeza uongozi wote wa
Wilaya kwa kazi ngumu ya kuhakikisha Mkalama inazidi kuwa bora kila siku.
“ Wakati tunaondoka hapa nyumbani palikuwa nyuma sana
kimaendeleo lakini leo hii tumekuja na kuikuta Mkalama yetu mpya kabisa na
inayozidi kuendelea, tumefarijika sana kwa hili” Alisema Nsoza.
Nsoza alimaliza kwa kuahidi kuutumia umoja huo kushirikiana
na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika kutatua changamoto mbalimbali
zinazowakabili wananchi wa Wilaya hiyo na kwamba malengo ya Umoja huo na ya
Wilaya yanalingana.
No comments:
Post a Comment