Naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari
Tulia Ackson leo aliongoza viongozi na mamia ya wananchi wa wilaya ya Mkalama katika
harambee ya kuchangia ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Wilaya hiyo.
Harambee hiyo ambayo mpaka kukamilika kwake ilifanikisha
kupatikana jumla ya shilingi milioni 61 ilihusisha viongozi mbalimbali wa
serikali, viongozi wa vyama vya siasa, wataalam mbalimbali wa Halmashauri ya
wilaya ya Mkalama na wananchi kwa ujumla.
Wakati wa harambee hiyo Mhe. Tulia aliwasifu viongozi wote
na watendaji wa wilaya ya Mkalama kwa jitihada mbalimbali wanazofanya katika
kuhakikisha wilaya hiyo inapiga hatua kadri muda unavyokwenda.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria harambee hiyo na kutoa
michango yao ni pamoja na Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula ambaye
alichangia shilingi milioni 4, Mbunge wa viti maalum Mhe. Martha Mlata ambaye
alichangia mifuko 150 ya saruji yenye thamani ya shilingi 2,250,000/= na Mbunge
wa viti maalum Mhe. Asha-Rose Matembe ambaye alichangia mifuko 50 ya saruji.
Wengine waliochangia katika harambee hiyo ni pamoja na
aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Mohamedi Mpinga ambaye alichangia mifuko
230 ya saruji, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ambayo ilitoa kiasi cha
shilingi 550,000/=, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
ambaye alichangia bati 98 na shilingi
500,000/=.
Mbali na viongozi hao wengine waliotoa au kuahidi michango
yao kwenye harambee hiyo ni pamoja na wakuu wa idara wa Halmashauri ya wilaya
ya Mkalama, waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo, wafanyabiashara
mbalimbali waliopo ndani ya wilaya hiyo na wananchi mbalimbali waliopo ndani na
nje ya wilaya hiyo.
Katika hafla hiyo, Mhe. Tulia alipewa rasmi jina la “Nzitu”
ambalo asili yake ni kabila la wanyiramba likimaanisha mtoto ambapo mara baada
ya kulipokea alimtangaza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Mkalama
Mhe. Lameck Itungi kuwa baba yake rasmi wa kabila hilo.
No comments:
Post a Comment