Mwenyekiti wa kijiji cha Mgolombyo George Nkango akizungumza machache kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya aweze kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho. |
Kaimu afisa ardhi wa Wilaya ya Mkalama, Imikigwe Mwanitu akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa Kijiji cha Mgolombyo juu ya suala la shamba lao lililochukuliwa na kijiji cha Kinyambuli. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mgolombyo alipowatembelea jana. |
Diwani wa kata ya Miganga Mhe: Omary Mtinga maarufu kama "Kulwa" akimpongeza na kutoa shukrani zake kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mara baada ya kiongozi huyo kumaliza hotuba yake. |
Kufuatia kushamiri kwa
matukio ya hivi karibuni ya mauai ya watu kwa kuchinjana, Mkuu wa Wilaya
ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai ametoa angalizo kwa wakazi wote wa
Mkalama kuwa makini na wageni wote wanaoingia na kutoka Wilayani hapa.
Mhe: Ngubiagai ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya
Ulinzi na Usalama amesema kuwa Vikosi vya Ulinzi na Usalama Wilayani hapa
vimejipanga kukabiliana na aina yoyote ya uhalifu lakini vinahitai ushirikiano
wa kutosha kutoka kwa wananchi ili viweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.
“Mtu anakuja, anaulizia chumba lakini cha ajabu kila bei
unayomtajia hashtuki wala habishi anakuwa tayari kutoa, Jiulize amekuja kufanya
nini cha thamani ya pesa anayolipia pango kwa gharama kubwa?” Alisema
Ngubiagai.
Ngubiagai aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na
wananchi wa kijiji cha Mgolombyo kilichopo katika kata ya Miganga Wilayani hapa
ambapo alitoa wito kwa watendaji wa kata
na vijiji kuhakikisha wanajiridhisha na kila mtu anayeingia wilayani hapa ikiwa
ni pamoja na kufanya utambuzi wa kina juu ya madhumuni ya safari yake.
“Hivi sasa binadamu amekuwa na roho mbaya kuliko hata
mnyama kwa sababu wanyama huwa wanaua wanyama wenzao kwa ajili ya kupata
kitoweo lakini binadamu anamuua mwenzake tena kwa kumchinja bila kutegemea
chochote kutoka kwake”, Aliongeza Ngubiagai.
Kwa upande mwingine, Mhe: Ngubiagai aliwaomba wananchi
wa kijiji cha Mgolombyo kuweka akiba ya kutosha ya chakula kutokana na mazao
mengi waliyoyapata msimu huu ili kuhakikisha hakuna uhaba wa chakula
utakaojitokeza kwa wakazi hao msimu huu.
“Ni aibu kubwa kwa mwananchi ambaye alilima mazao na
yakastawi vizuri kisha akayauza na baadaye akaja ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuomba
chakula kwa sababu sio tu unajiabisha wewe bali unaniabisha hata mimi kama Mkuu
wa Wilaya” Alisema Ngubiagai.
Katika hatua nyingine Mhe: Ngubiagai aliwahakikishia
wananchi wa kijiji cha Mgolombyo kuwa atapambana mpaka dakika ya mwisho
kuhakikisha kuwa wanapata haki yao ya kurejeshewa shamba lao la kijiji ambalo
limeporwa na watu wa kijiji cha Kinyambuli.
“Kwa sasa kesi hii ipo mahakamani hivyo siwezi kuingilia
shughuli za mahakama lakini nawahakikishia ntahakikisha haki juu ya suala hili
inatendeka kwa sababu mazingira ya uchukuaji wa shamba hili yanazua maswali
mengi sana na kwa kuanzia nitaikabidhi Takukuru na Maafisa usalama wa Wilaya
majina ya waliokuwa wajumbe wa baraza la ardhi la kata ili kufanya uchunguzi wa
kina dhidi ya baraza hilo lililoridhia shamba hilo wapewe watu hao” Alimalizia
Ngubiagai.
MSIKILIZE HAPA MHE: NGUBIAGAI AKIZUNGUMZIA SUALA LA ULINZI NA USALAMA WA WILAYA.
Great dude.... Great job
ReplyDelete