Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akikagua ubora wa matofali yanayotumika kujengea Miundombinu ya Kituo cha Afya cha Kinyambuli mapema leo |
“Jana Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imepokea fedha kwa
ajili ya kumalizia miundombinu yote ya Zahanati za Kidarafa, Milade na Nduguti
hivyo muda si mrefu tutafungua Zahanati hizo na Wananchi wa maeneo hayo wataanza kupata huduma
zote stahiki za kiafya”
Hiyo ni kauli iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga alipokuwa katika kijiji
cha Kinyambuli kukagua ujenzi wa Kituo bora na cha Kisasa cha Afya Unaoendelea
kijijini hapo.
Mradi huo unaogharimu kiasi cha Shilingi milioni 700 unatarajiwa
kukamilika ifikapo Mwezi Aprili Mwaka huu ambapo jumla ya Shilingi milioni 400
zilipokelewa na Halmashauri ya Wilaya na
Kuhamishiwa katika akaunti ya Serikali
ya Kijiji hicho ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo kwa wakati.
“Shilingi Milioni 300 zilizobaki zitatumika kwa ajili ya
ununuzi wa vifaa tiba na dawa ambapo tayari tumeshazielekeza Bohari Kuu ya Dawa
(MSD) ili pindi tu Kituo kitakapokamilika huduma ianze mara moja” Alisisitiza
Sanga.
Sanga alibainisha faida kadhaa ambazo wananchi wa Wilaya ya
Mkalama kwa ujumla watanufaika nazo baada ya kukamilika kwa kituo hicho ikiwa
ni pamoja na kusogezewa karibu huduma muhimu na za lazima ikiwemo ile ya
Kuhifadhi Maiti na Kufanya Upasuaji ambapo Wananchi wa Mkalama wanalazimika kwenda
mpaka hospitali ya Hydorm kwa ajili ya kupata huduma hizo.
“Lakini pia ninapenda kuwajulisha kuwa katika mwaka ujao wa Fedha Halmashauri inakusudia kuanza
ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambapo tayari eneo la kujenga hospitali hiyo
limeshatengwa na kinachosubiriwa ni Fedha tu kwa ajili ya kuanza Utekelezaji wa
Ujenzi wa Hospitali hiyo” Aliongezea
Sanga.
Mpaka kufika mwezi Juni mwaka huu Halmashauri ya Wilaya ya
Mkalama inatarajiwa kupiga hatua kubwa katika sekta ya Afya baada ya kukamilika
kwa wodi ya wazazi ya Zahanati ya Nduguti, Vifaa tiba na miundombinu yote
katika zahanati ya Milade na Kidarafa na Ujenzi wa Majengo ya Chumba cha
Upasuaji, wodi ya Wazazi, Maabara ya Kisasa, Chumba cha Kuhifadhia Maiti na
Nyumba bora ya Watumishi wa kituo hicho.
No comments:
Post a Comment