Hivi ndivo ng'ombe walivyokuwa wakipigwa chapa kama inavyoonekana pichani wakati wa zoezi hilo katika kijiji cha Mwando siku chache zilizopita |
Zoezi la kupiga chapa ng’ombe kwa Wilaya ya Mkalama
limehitimishwa mapema leo katika kijijicha Gumanga ambapo jumla ya Ng’ombe
192,900 ikiwa ni zaidi ya lengo la awali lililolenga kupiga chapa jumla ya
ngombe 127,849.
Akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa zoezi, Afisa Mifugo
wa Wilaya ya Mkalama Elias Mbwambo amesema utekelezaji wa zoezi hilo unatokana
na sheria namba 12 ya Mwaka 2010 ya usajili, ufuatiliaji na utambuzi wa mifugo
ikichagizwa na takwa la soko la kimataifa ambapo ili mifugo iingie katika soko
hilo ni lazima ijulikane mahali ilipotoka.
Mbwambo amesema kuwa katika zoezi hili kila mfugaji
alitakiwa kulipia shilingi 500 kama gharama ya chapa ambapo fedha hizo zilikuwa
zikitumika kwa ajili ya kuratibu zoezi zima mpaka kukamilika kwake.
“Usajili huu umefanyika kwa kutumia code zilizotolewa na
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambazo ni T MKL na code za vijiji
zilizotolewa na Wilaya ambapo vijiji vilipangwa kwa mpangilio wa herufi kuanzia
kijiji namba moja hadi 70 na chapa hiyo iliwekwa mguu wa nyuma kulia katikati
ya goti na paja” Alisema Mbwambo.
Aidha Mbwambo ameongeza kuwa wafugaji wanaruhusiwa kuwa na
alama zao za utambuzi ambapo zitatakiwa kusajiliwa kwanza ndipo wazitumie bila
kuathiri zile za serikali na alama hizo zitawekwa mkono wa mbele upande wa
Kulia.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kufunga rasmi zoezi hilo
kwa awamu hii, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka
amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kuhakikisha
anatenga maeneo ya kulisha mifugo hiyo ili kuondokana na migogoro baina ya
wafugaji na wakulima.
“Kumekuwa na mazoea ukifika msimu wa masika maeneo yote huwa yanalimwa na kusababisha
mifugo kukosa maeneo ya chakula jambo ambalo huweza kusababisha mgogoro baina
ya mkulima na mfugaji” Alisema Masaka.
Mhe. Masaka ametoa agizo kwa serikali za vijiji kuwa endapo ng’ombe
asiye na chapa atachinjwa, kuuzwa au kusafirishwa nje ya Wilaya hatua za
kisheria zichukuliwe dhidi ya mwenye ng’ombe, mchinjaji na mnunuzi wa ng’ombe
huyo.
“Wananchi watumie mifugo yao kwa kujiendeleza na kuboresha
hali za maisha kwa kufanya shughuli za maendeleo” Alimalizia Mhe. Masaka.
No comments:
Post a Comment