Baada ya kuiongoza Wilaya ya Mkalama kwa kipindi
kisichozidi miezi nane, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe: Christopher Ngubiagai ametumia kikao cha
baraza la madiwani kilichomalizika muda mfupi uliopita kuwaaga viongozi na wananchi wote wa
Wilaya hiyo.
Kitendo hicho kinafuatia mabadiliko na uteuzi wa wakuu
wa Wilaya uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: Dokta John
Pombe Magufuli ambaye amemhamishia Mhe: Ngubiagai katika Wilaya ya Kilwa.
“Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru sana kwa
ushirikiano na upendo mlionionesha tangu niteuliwe kushika wadhifa huu tar 5
mwezi Oktoba mwaka jana, Mwenyezi Mungu awajaalie sana” Amesema Ngubiagai.
Mhe: Ngubiagai ameshukuru kwa uzoefu mkubwa alioupata
katika Wilaya ya Mkalama na kuomba viongozi na wananchi wote wa Wilaya hiyo
kumpa ushirikiano wa kutosha mbadala wake pindi atakapoanza kazi yake.
Pia ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa uongozi wa Wilaya
ya Mkalama pamoja na mbadala wake kutilia mkazo kwenye suala la Elimu ambapo
amesisitiza kuwa itakuwa ni jambo linalopendeza kwa Wilaya hiyo yenye watu Zaidi
ya laki mbili kuwa na shule ya Elimu ya juu ya sekondari.
“Lakini pia nitumie fursa hii kuwaomba mtumie fursa
nzuri na kubwa ya kiuchumi iliyopo Wilayani Mkalama kuongeza kipato cha Wilaya
na kuinua hali ya uchumi wa mwananchi mmoja mmoja hasa kupitia sekta ya madini
ambayo hivi sasa ni wageni tu ndio wanaonufaika” Alimalizia Ngubiagai.
No comments:
Post a Comment