Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe: Selemani Jafo, akielekea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni. |
Mkandarasi kutoka kampuni ya Mzinga akitoa maelekezo juu ya namna ukamilishaji wa ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Wilaya utakavyofanyika. |
Haya ndio madawati aliyokabidhiwa Mheshimiwa Waziri leo na Mbunge wa jimbo la Mkalama, Mhe: Allan Kiula. |
Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe: Allan Kiula akimkabidhi madawati 100 yaliyotokana na mfuko wa jimbo, Mhe: Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemai Jafo. |
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe: Selemani Jafo akikabidhi madawati kwa mmoja waWAkuu wa Shule za sekondari mara baada ya kukabidhiwa na Mhe: Mbunge mapema leo asubuhi. |
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe: Selemani Jafo akimpongeza mtengenezaji mkuu wa madawati hayo Lameck mara baada ya kukabidhi kwa wakuu wa Shule. |
Sehemu ya Wananchi wa Wilaya ya Mkalama waliojitokeza kumsikiliza Naibu waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe: Selemani Jafo katika eneo la Stendi mapema leo. |
Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe: Allan Kiula akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mkalama muda mfupi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mh: Selemani Jafo. |
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe: Selemani Jafo akihutubia wananchi wa Wilaya ya Mkalama waliojitokeza kumsikiliza mapema leo asubuhi. |
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ambaye pia
ni Mbunge wa jimbo la Kisarawe leo amefanya ziara fupi katika halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama ambapo amewataka watendaji wa serikali kufanya kazi zao kwa
weledi na kuhakikisha ofisi zao zinamaliza kero zote za wananchi.
Huku akizungumza mbele ya umati wa watu waliojitokeza
kumsikiliza mara baada ya kukabidhi madawati, Mhe: Jafo amesema ni jambo la
kushangaza kwa halmashauri kuendelea kuwa na madai ya watumishi kutopandishwa
madaraja wakati ofisi ya Utumishi ipo.
“Kuanzia sasa, akitokea mtu yoyote kulalamika
kutopandishwa daraja, Afisa Utumishi tutakuondoa kwenye nafasi yako”
Alisisitiza Jafo.
Kwa upande wa Idara ya Maendeleo ya jamii, Mhe: Jafo
amemtaka Afisa Maendeleo ya jamii kupitia ofisi yake, ahakikishe wametoa elimu
ya kutosha kwa vikundi vya vijana na wanawake juu ya namna watakavyotumia mkopo
wa Milioni 50 alizoahidi Mhe: Rais ambazo zitatoka muda wowote kuanzia sasa.
“Afisa Maendeleo ya jamii ndio injini ya kuchochea
maendeleo ya vijana na jamii inayokuzunguka hapa Wilayani lakini cha kushangaza wengi wenu mmekuwa mkionekana zaidi pindi pesa za Tasaf na Mradi wa Ukimwi zinapotoka na huenda hata hii jamii iliyopo mbele yangu hapa haikutambui, Naomba mbadilike” Aliongeza Jafo.
Kabla ya kuzungumza na wananchi hao Mhe: Jafo
alikabidhiwa madawati 100 yaliyotolewa na Mfuko wa Mbunge wa jimbo hilo ambapo
aliwapongeza viongozi, watendaji na wananchi wote wa Mkalama kwa kumaliza
kabisa tatizo la madawati Wilayani hapa.
“ Madawati ndio kipimo kikubwa kwa wakurugenzi na wakuu
wa Wilaya wote nchini hivyo ukiona hujakamilisha suala hili ujue nafasi hiyo haikutoshi
tena lakini nawapongeza Mkalama mmeshavuka mtego huo hivyo mpo salama”
Ameongeza Jafo.
Mara baada ya kufika Wilayani hapa mapema leo, Mhe: Jafo
alifanya ziara ya kukagua Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na pamoja na jengo
la halmashauri ya Wilaya ambalo limefikia hatua ya Lenta mpaka hivi sasa na
awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika muda wowote kuanzia hivi sasa.
Baada ya kuona namna ujenzi wa jengo hilo unavyoendelea
kwa kasi, Mhe: Jafo alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama,
Bravo Kizito Lyapembile kwa kazi nzuri ya kujenga jengo lenye ubora tena kwa
kutumia mkandarasi wa ndani.
“Niliwahi kwenda Halmashauri ya Mwanga nikakuta jengo la
serikali limeshatoa nyufa zaidi ya 20 tena kabla hata halijaanza kutumika, Lakini
ukiuliza Mkandarasi anasema “Consultant” hajasema chochote ndio maana naye
ameacha hali iwe hivyo, Lakini Mkalama mmemtumia Mkandarasi wa Wilaya kusimama
kama “consultant” tena kwa mshahara huo huo anaolipwa na serikali, Hongereni
sana” Alipongeza Jafo.
Kufuatia suala hilo Mhe: Jafo Aliagiza Wilaya nyingine
zifike Mkalama kujifunza namna ya kusimamia kazi za serikali bila kufuja fedha
za umma ambazo zinatokana na kodi za wananchi.
Kabla ya kuondoka katika eneo hilo, Mhe: Jafo aliagiza
majengo yote ya serikali nchini
kuhakikisha yanakuwa na hati miliki ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima siku
za usoni.
No comments:
Post a Comment