Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ambaye pia ni Kaimu mkuu wa
Wilaya ya Iramba Mheshimiwa Christopher Ngubiagai amesema kuwa kasi yake ya
kuwasimamisha watendaji wazembe itaendelea mpaka pale watumishi katika Wilaya
hizo watakapofuata maadili ya kazi zao.
Ngubiagai ameyasema hayo kufuatia baadhi ya watumishi wa
Wilaya ya Iramba kutamka wazi kuwa hivi sasa hali katika halmashauri hiyo
imebadilika kabisa na kila mtu amekuwa akifanya kazi kwa kuogopa kusimamishwa
kazi pindi akikosea.
“Kama unafanya kazi zako vizuri na unatimiza wajibu wako
vizuri sitokuwa na tatizo na wewe kabisa lakini wale wazembe na wabadhirifu
wote nitaendelea kuwasimamisha na kama wakipatikana na hatia nitawakabidhi
kwenye mkono wa sheria”.
Alisisitiza wale wote wanaowafahamu watu wanaokiuka
maadili ya kazi kwa kushiriki vitendo vya kifisadi wawapo ofisini, wasisite
kutoa taarifa ili kuepuka kuwaonea watu wasio na hatia.
“Kuna hili suala la ubadhirifu wa zaidi ya milioni mia
tano za lile jengo la Zahanati pale ambalo bado halijakamilika, Nitakuja kwa
ajili ya kufuatilia na kushughulika na wale wote ambao wamehusika katika
ufisadi wa ujenzi ule”
Katika kuunga mkono jitihada zinazooneshwa na Watendaji wa
serikali yake, Jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwajibu wale wote
wanaobeza staili yake ya kutumbua majipu na kusema kuwa mtu aliyeiba hadharani anapaswa
kufukuzwa hadharani pia.
No comments:
Post a Comment