Mkuu wa Wilaya
ya Mkalama mheshimiwa Christopher Ngubiagai amefurahishwa na kumpongeza Mkuu wa
Shule ya Sekondari Jorma iliyopo katika
kata ya Gumanga Wilayani hapa Mwalimu
Mwanga H.B Mangi kwa kuonesha moyo wa kizalendo na kujenga bweni la
kisasa kabisa kwa wanafunzi wa kike shuleni hapo.
Akizungumza
wakati wa ziara ya ukaguzi wa shule hiyo, Ngubiagai alisema kuwa mwalimu huyo
anastahili kupongezwa na kupewa motisha kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa sababu
kuna baadhi ya watu wakipewa pesa na serikali huzitumia kwa matumizi yao
binafsi na kutekeleza miradi ya serikali chini ya kiwango au kutotekeleza
kabisa.
“Kule Iramba kuna
watumishi nimewasimamisha kazi na wameshafunguliwa kesi mahakamani kwa sababu
walipewa milioni 133 kwa ajili ya ujenzi wa bweni tangu mwaka 2011 lakini mpaka
leo bweni lile halijakamilika lakini huyu alipewa milioni 40 na amejenga bweni
la kisasa kabisa tena kwa muda mfupi na bado pesa ya choo katoa kwenye bajeti
yake” Alisisitiza Ngubiagai.
Aliongeza kuwa
watumishi wa aina hiyo atahakikisha wanapata kila nyenzo watakazohitaji katika
kutekeleza majukumu yao kwa sababu wameonesha nia ya dhati ya kuwatumikia
wananchi na kulinda rasilimali za serikali.
Kwa upande
wake Mwalimu Mangi alisema kuwa baada ya
kukabidhiwa pesa hiyo, waliwasiliana na mhandisi wa Wilaya ambaye B.O.Q yake
ilionesha pesa hiyo inatosha kujenga bweni la wanafunzi 48 tu ambao ni wachache
ukilinganisha na uhitaji uliopo.
“Nilikaa na
timu yangu tukaamua kumtafuta fundi wa hapa hapa kijijini akakiri kuwa pesa
hiyo inaweza kujenga bweni zuri lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 56 ambayo ni
zaidi ya idadi ya awali” Alisema Mwalimu Mangi.
Aliongeza kuwa
baada ya kupata taswira hiyo, aliwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama Bravo Lyapembile na mhandisi wa Wilaya ambaye alisema kwa
mchakato walioufanya suala hilo linawezekana hivyo wanaweza kuendelea nao na
kama wakikwama wawasiliane na ofisi ya Mkurugenzi mara moja.
“Tulianza
rasmi ujenzi na mafundi wetu wa hapa hapa kijijini na hatimaye jengo
limekamilika na bado kuna vifaa vimebaki lakini katika pesa ile hakukuwa na bajeti ya choo hivyo niliamua
kutumia bajeti yangu ya shule kujenga vyoo na ndo vipo kwenye hatua ya mwisho
kukamilika”. Alimalizia mwalimu Mangi.
Katika hatua
nyingine Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mheshimiwa Christopher Ngubiagai alisema
atafanya kila jitihada kuhakikisha bweni jingine ambalo ujenzi wake
umesimama kutokana na kukosa fedha
linakamilika na linaanza kutumiwa na wanafunzi kama ilivyokusudiwa.
“Nikifika
ofisini nitaanza kufanya mchakato ili fedha zinazotakiwa kwa ajili ya kumalizia
ujenzi wa bweni hili zipatikane na likamilike kabla ya mwezi julai mwaka huu
ili hawa watoto wetu hasa wanafunzi wa kike waondokane na changamoto ya
kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.” Alimalizia Ngubiagai.
Huu ndio muonekano kwa ndani wa bweni lililojengwa kwa pesa ya serikali na kusimamiwa na Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Jorma. |
Na huu ndo muonekano wa bweni hilo kwa nje. |
Huu ndio muonekano kwa kila chumba cha bweni hilo ambapo kila chumba kina uwezo wa kuweka vitanda vinne. |
No comments:
Post a Comment