Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida Mhe. Asha-Rose Matembe akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya Wanawake iliyoadhimishwa leo katika kijiji cha Mwando Wilayani Mkalama |
|
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya Wanawake iliyoadhimishwa leo katika kijiji cha Mwando Wilayani hapa. |
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida Mhe. Asha-Rose Matembe akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mkalama na Viongozi wengine wa Wilaya hiyo Mifuko 30 ya Saruji ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya Mifuko 50 ya Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mwando, Zoezi hilo limefanyika leo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya wanawake iliyoadhimishwa Kiwilaya Kijijini hapo. |
Wilaya ya Mkalama leo imeungana na maeneo mengine yote kusherehekea
siku ya kimataifa ya wanawake iliyofanyika katika kijiji cha Mwando yakiwa ni maadhimisho ya tano ya sikukuu hiyo tangu
kuanzishwa kwa Wilaya hii.
Katika maadhimisho hayo ambayo mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu ya kitaifa isemayo “Kuelekea
Uchumi wa Viwanda tuimarishe usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa Wanawake” viongozi
mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama na Mkoa wa Singida kwa ujumla walitumia fursa
hiyo kuhamasisha wanawake kujitokeza katika fursa mbalimbali na kupiga vita
hali ya utegemezi dhidi ya wanaume.
Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Singida Mhe. Asha-Rose
Matembe aliwaasa wanawake wote Wilayani Mkalama kujunga kwenye Vikundi ili
waweze kukidhi vigezo vya kupatiwa mikopo ya Serikali na taasisi mbalimbali za
fedha.
“Niwaombe Sido na taasisi mbalimbali za fedha watembelee
vikundi vya wanawake na kutoa elimu ya Ujasiriamali ili fedha wanazokopeshwa
ziweze kuwa na tija” Alisisitiza Mhe. Matembe.
Mhe. Matembe pia amepongeza jitihada za wazi zilizooneshwa
na wananchi wa Kijiji cha Mwando kwa Kujenga Zahanati ambapo aliunga mkono jitihada
hizo kwa kuwaahidi kuchangia mifuko 50 ya Saruji huku 30 akiikabidhi hapo hapo
na mingine 20 kuahidi kuitoa ndani ya siku chache zijazo.
Awali kabla ya Kumkaribisha Mgeni Rasmi wa maadhimisho
hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey
Sanga aliainisha jitihada mbalimbali ambazo serikali imezifanya ndani ya Wilaya
ya Mkalama katika kuinua Ustawi wa wanawake ambapo mbali na Asilimia 5
inayokwenda kwenye vikundi vya wanawake vilivyosajiliwa kila Mwezi, Serikali
pia inatarajia kukamilisha wodi ya wanawake iliyopo katika Zahanati ya Nduguti ndani ya Siku 60
kuanzia sasa.
“Pia ndani ya Miezi miwili ijayo tunatarajia kukamilisha
Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinyambuli ambacho ndani yake kuna Chumba kikubwa
cha Upasuaji kwa wanawake wajawazito jambo ambalo litazidi kuhakikisha usalama
wa afya za wanawake waliopo Wilayani Mkalama” Alisisitiza Sanga.
Sanga aliongeza kuwa Bweni la Wanafunzi wa kike katika Shule
ya Sekondari Nduguti linatarajiwa kukamilika muda wowote kuanzia hivi sasa
hivyo kuanzia Muhula ujao wanafunzi wa Kike wote waliopo shuleni hapo watakuwa
wakiishi bwenini jambo litakaloongeza usalama wa watoto wa kike pindi wakiwa
shule.
Katika hotuba yake, Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo ambaye
pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka ameainisha aina
mbalimbali za Unyanyasaji wa wanawake unaoendelea katika jamii likiwemo suala
la ndugu wa Marehemu kuchukua Mali pindi mwanamke anapofiwa na mumewe.
“Jambo hili katika Wilaya ya Mkalama sitaki kulisikia na
naagiza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya watakaobainika kufanya
hivyo” Aliongeza Mhe.Masaka.
Mhe. Masaka aliongeza kuwa kumekuwa na tabia isiyopendeza
kwa baadhi ya wanaume ambapo wamekuwa wakiwalaumu wake zao pindi watoto
wanapoharibikiwa kimaadili huku wakisahau kuwa jukumu la malezi ya watoto ni la
baba na mama kwa pamoja na si mama peke yake.
“Lakini bado kuna baadhi ya kaya ambazo mpaka leo hazimpi
mwanamke haki ya kupanga uzazi na bado jamii imekuwa ikifumbia macho badala ya
kutoa ushauri unaofaa jambo ambalo linasababisha wanawake kuchoka sana kwa
kuzaa mfululizo bila kufuata uzazi wa mpango” Alisema Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka wanawake
wote Wilayani Mkalama kutoona ni jambo la kawaida kwa watoto wao wa kike kupata
ujauzito wakiwa shuleni kwa sababu takwimu zinaonesha kiwango cha watoto wa
kike wanaopata ujauzito wakiwa Shuleni ni asilimia moja tu hivyo ni lazima
wazazi wa watoto hao waungane na hiyo asilimia 99 ili kutokomeza kabisa hali
hiyo.
“Mpaka sasa Jumla ya Kesi tatu za ubakaji zimeshafikishwa
Mahakamani Wilayani hapa na wahusika wote waliokutwa na hatia wamehukumiwa
vifungo” Alimalizia Mhe. Masaka.
No comments:
Post a Comment