Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akihutubia leo katika sherehe za Siku ya Mkulima zilizofanyika katika kijiji cha Kidarafa. |
Wilaya ya Mkalama leo imefanya sherehe za siku ya Mkulima iliyofanyika
katika kijiji cha Kidarafa kwa kuwajengea uwezo wakulima kutambua umuhimu wa
kutumia pembejeo bora na za kisasa.
Sherehe hizo zilizofanyika kwa mtindo wa Warsha fupi kwa
wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbegu na mbolea iliwezeshwa na wasambazaji maarufu
wa pembejeo za kilimo wanaojulikana kama “BAYDA AGROVET” wakishirikiana na Kampuni ya kizalendo ya uuzaji
wa mbegu bora na za kisasa, viautilifu na madawa mbalimbali ya mimea inayojulikana
kama “Meru Agro tours” yenye makao yake makuu Mkoani Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka ambaye
pia alikuwa Mgeni rasmi katika sherehe hizo, alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kuwasisitiza
wakulima kutumia vyema elimu waliyopewa
katika warsha hiyo kuhakikisha wanafanya kilimo bora na cha kisasa.
Mbali na msisitizo huo, Mhe. Masaka pia alitumia fursa
hiyo kuwatahadharisha wakulima wote Wilayani hapa wahakikishe wanapata pembejeo
kwenye maduka rasmi na waombe risiti ya kuthibitisha manunuzi yao.
“Epukeni kununua pembejeo kwenye minada au maduka yasiyo
rasmi kwa sababu tutashindwa kumpata muuzaji pindi ikigundulika kuwa bidhaa
uliyonunua ni feki” Alisisitiza Mhe. Masaka.
Mpaka sasa kampuni ya “Meru Agro tours” imefanikiwa kutoa elimu kwa wakulima kutoka katika kata
tano za Mwanga, Nduguti,Ilunda, Nkalankala na Kinampundu.
Mafunzo hayo ambayo yalijumuisha wakulima mmoja mmoja 42
na vikundi 25 vyenye jumla ya wakulima 625 yalienda sambamba na ugawaji wa kilo
133 za mbegu bora za mahindi zenye thamani ya shilingi 798,000, kilo 300 za
mbolea aina ya DAP, kilo 300 za mbolea aina ya Urea na kilo 50 za mbolea aina
ya Kyno vyote vikigharimu shilingi 648,000 na hivyo kufanya jumla ya mchango
uliotolewa na kampuni hiyo Wilayani Mkalama mpaka sasa kufikia kiasi cha shilingi milioni
1,446,000.
Siku ya Mkulima Wilayani Mkalama huadhimishwa kila mwaka
muda mfupi kabla ya kuanza kwa msimu wa mavuno ya mazao mbalimbali.
“
No comments:
Post a Comment