Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika daraja la Mto Sibiti mapema leo wakati wa ziara yake aliyoifanya Wilayani Mkalama. |
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika eneo la Mto Sibiti mapema leo wakati wa ziara yake Wilayani Mkalama. |
Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mkalama wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya leo Wilayani hapo. |
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakati akihitimisha ziara yake Wilayani hapo leo. |
Wanafunzi wa kidato cha tano wa Shule ya sekondari Iguguno wakionesha picha za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli (kushoto) na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan muda mfupi baada ya Makamu huyo wa Rais kuwasili katika viwanja vya Shule hiyo mapema leo. |
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na mwanafunzi Laylat Ramadhani (19) muda mfupi kabla hajamkabidhi kiasi cha fedha kitakachomsaidia katika masomo yake ikiwa ni ishara ya kutambua juhudi zilizooneshwa na mwanafunzi huyo licha ya kukabiliwa na changamoto ya kuwa na umbile dogo kuliko wanafunzi wote shuleni hapo. |
Muda mfupi uliopita Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewahutubia wananchi wa Wilaya ya Mkalama
katika Mkutano uliofanyika kwenye moja ya viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama.
Mhe. Samia ambaye aliambatana katika ziara yake
aliambatana na mawaziri watatu, alianza
ziara hiyo kwa kukagua miundombinu ya shule ya sekondari Iguguno kabla ya
kwenda kuangalia hatua ya ujenzi wa daraja la mto Sibiti na alihitimisha ziara
hiyo muda mfupi uliopita kwa kuzindua Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
na kuzungumza na wananchi.
Akizungumza kabla ya hotuba ya Mhe. Makamu wa Rais, Naibu
Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa alisema kuwa dhamira ya serikali kwa sasa
ni kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Mkalama hawapati changamoto yoyote
kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara na ndio maana kwa kushirikiana na
Wakala wa barabara wa Taifa (TANROADS) itahakikisha kila upande unaunganishwa
kwa kiwango cha lami.
“Hivi karibuni tutaenda kujenga daraja la chuma pale
kijiji cha Msingi na wakati wowote fedha ikipatikana kipaumbele chetu kitakuwa
ni kuweka lami barabara inayotoka Iguguno hadi daraja la Sibiti huku
tukiunganisha pia barabara ya lami kutoka kijiji cha Gumanga hadi Msingi”
Alisisitiza Mhe. Kwandikwa.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso
alisema kuwa mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 10 zimeshatumika kwa miradi
ya maji ya Wilaya ya Mkalama ikiwa ni pamoja na mradi wa maji wa Kikhonda,
Ipuli, Iguguno, Nyahaa na Nduguti ambapo alisisitiza kuwa fedha za miradi hiyo
yote zilishalipwa na wananchi wameanza kupata huduma ya maji kwa miradi
iliyokamilika.
“Lakini Mhe. Makamu wa Rais ni lazima niseme ukweli kuwa
mradi wa maji wa Nyahaa umejaa ufisadi mkubwa sana kwa sababu serikali imelipa
zaidi ya shilingi milioni 900 lakini mradi huo haujakamilika mpaka sasa ingawa
mkandarasi alishalipwa hela zote na cha kusikitisha zaidi mhandisi aliyekuwa
anasimamia mradi huo amehamishiwa Gairo” Alitoa angalizo Mhe. Aweso
Kufuatia hali hiyo Mhe. Aweso alimuomba Makamu wa Rais
kumuagiza katibu Mkuu wa Wizara ya Maji amuandikie barua ya wito mhandisi huyo
ili afike kwenye kikao cha majumuisho ya Ziara keshokutwa na kutoa majibu ya
kina kuhusu suala hilo ombi ambalo Mhe. Makamu wa Rais alilikubali.
Katika hotuba yake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania aliwapongeza viongozi wote wa Wilaya ya Mkalama kwa kukamilisha
ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ambapo aliwataka kuendelea kufanya hivyo katika
ujenzi wa hospitali ya Wilaya na miradi mingine ya serikali.
“Lakini lazima niseme ukweli kuwa kitendo cha kusimamishwa
pale Ibaga kimeonesha wazi kuwa kuna ukosefu wa ushirikiano baina ya wananchi
kwa sababu inaonekana kuna baadhi ya watu wanapangwa kusimama barabarani na
mabango kwenye misafara ya viongozi jambo ambalo si zuri na linachafua taswira
nzuri mliyoijenga wananchi wa Mkalama” Alisisitiza Mhe. Samia.
Mhe. Samia alihitimisha hotuba yake kwa kuwasihi wananchi
wa Mkalama kutunza mazingira hasa katika kipindi hiki cha Masika ili vyanzo vya
maji vilivyopo visikauke na kusababisha ukame wakati wa Kiangazi.
“Mwisho ninawaomba Wananchi wa Mkalama na Mkoa wa Singida
kwa ujumla, tujihadhari sana na ugonjwa wa Ukimwi kwa sababu japo sijapata
takwimu ya Wilaya lakini takwimu ya Mkoa si nzuri hata kidogo hivyo tujilinde
dhidi ya Ugonjwa huu hatari ndugu zangu” Alimalizia Mhe. Samia.