Wednesday, 5 September 2018

Makamu wa Rais kuinufaisha Mkalama

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa ofisini kwake Ikulu jijini Dar-salaam (picha kwa hisani ya mtandao)Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) na Mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo (IFAD) inatarajia kuipa fursa ya kipekee wilaya ya Mkalama baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza uhakika na Usalama wa Chakula katika maeneo kame ya Tanzania (LDFS).

Mradi huo unaoendelea katika nchi 12 barani Afrika zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara unatarajiwa kutekelezwa katika vijiji vya Mpambala, Nyahaa, Lugongo na Mkiko vilivyopo katika kata ya Mpambala.

Kupitia mradi huo wananchi wa Mpambala watapata fursa ya kushiriki moja kwa moja kupitia kamati za uwakilishi za vijiji zitakazoshirikisha jinsia zote ambapo zitakuwa na kazi ya kupanga na kusimamia maliasili zilizopo kati ya vijiji kwa kukubaliana katika upangaji na matumizi yanayozingatia usawa na kuandaa miongozo.

Mradi huo unaotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao  pia utaipa serikali fursa ya kutambua teknolojia na maeneo yanayofaa kwa uvunaji wa mvua na  maeneo ya vyanzo vya maji ambapo teknolojia hiyo itasaidia kupunguza upotevu wa maji na kuongeza uzalishaji hasa kipindi cha kiangazi kwa wananchi wa kata ya mpambala.

Wananchi wa vijiji vya kata ya Mpambala pia watapatiwa mafunzo ya shamba darasa kuhusu kilimo hifadhi na mbinu bora za kilimo rafiki kwa mazingira, uboreshaji na urutubishaji wa udongo, mbinu za kilimo misitu, kilimo cha makinga maji, kilimo cha mzunguko na usimamizi shirikishi wa kudhibiti wadudu na magonjwa ya mazao.

Mafunzo hayo yataenda sambamba na kuwasaidia wakulima hao upatikanaji wa mbinu bora za kilimo na pembejeo  katika mashamba darasa yatakayoanzishwa.

Mbali na Mkalama wilaya nyingine zinazotekelezwa mradi huu hapa nchini ni Kondoa (Dodoma), Nzega (Tabora), Magu (Mwanza) na Micheweni (Kaskazini Pemba).

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA