Friday 26 January 2018

Ni marufuku walimu kukusanya michango ya Wanafunzi- Nchimbi

Mkuu wa Mkoa wa Singida (kushoto) akitoa maelekezo kwa viongozi wa mamlaka ya Bonde  na viongozi wa Wilaya ya Mkalama juu ya namna bora ya utunzaji wa mazingira.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akimuelezea jambo Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi katika kituo cha upimaji wa wingi wa maji kijiji cha Iambi.


Mkuu wa Mkoa wa Singida na Viongozi waandamizi wa Wilaya ya Mkalama wakishiriki Ufunguzi wa Darasa la kisasa lililojengwa na Shirika la 'Norwegian Church Aid' katika  kijiji cha Munguli jana

Afisa Miradi wa mashirika ya 'Norwegian Church Aid' (NCA) na 4 Corners Cultural Program (4CCP) Nelson Faustine akielezea mchakato mzima wa ujenzi wa darasa la kisasa uliofanywa na mashirika hayo katika kijiji cha Munguli mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi jana.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akiwa kwenye picha ya pamoja na Mshauri Mkuu wa masuala ya Maji kutoka Shirika la 'Norwegian Church Aid' NCA Manford Hart wakati wa ziara yake jana katika kijiji cha Munguli.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Lameck Itungi wakati wa ziara yake jana katika kijiji cha Munguli.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi (Kushoto mbele) akiwa ndani ya darasa lililojengwa na Shirika la 'Norwegian Church Aid' mara baada ya kulifungua jana katika kijiji cha Munguli.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akiwaasa wananchi wa kijiji cha Munguli  juu ya umuhimu wa kutumia vyema fursa wanazozipata.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akizungumza machache muda mfupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida katika kijiji cha Munguli Jana.

Viongozi waandamizi wa Kanisa la Hydorm na wawakilishi wa shirika la 'Norwegian Church Aid' wakipokea cheti kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida. Cheti hicho kimetolewa na Uongozi wa Wilaya ya Mkalama kama ishara ya kushukuru kwa mchango uliotolewa na Shirika hilo  Wilayani hapa.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama pamoja wawakilishi wa Shirika la 'Norwegian Church Aid' kutoka Nchini Norway jana katika kijiji cha Munguli. Nyuma yao ni paneli za Sola zinazohakikisha upatikanaji wa maji kijijini hapo Muda wote.


“Kuanzia sasa jukumu la kukusanya na kusimamia michango ya aina yoyote ile shuleni lifanywe na wazazi wa wanafunzi hao kupitia bodi za shule badala ya walimu na kuanzia sasa mwalimu haruhusiwi kumrudisha nyumbani mwanafunzi mwenye upungufu wa mahitaji ya shule na badala yake amshirikishe mzazi juu ya umuhimu wa mahitaji hayo ili mzazi kwa hiyari yake aweze kutimiza majukumu yake ya msingi kwa mwanae akiwa shuleni”

Hayo ni maneno yaliyozungumzwa na  Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi alipokuwa katika ziara yake Kijiji cha Munguli mapema jana ambapo alifika kwa ajili ya kukagua mradi mkubwa wa Maji na kuzindua darasa la kisasa la shule ya Msingi Munguli na Ofisi ya Walimu miradi yote ikiwa imewezeshwa na Mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka nchini Norway yanayojulikana kama ‘Norwegian Church Aid’ (NCA) na ‘4 corners Cultural Program’ (4CCP).

Mhe. Nchimbi ameyapongeza mashirika hayo kwa kuwezesha ujenzi wa miradi mikubwa katika kijiji cha Munguli ambapo aliongeza kuwa undugu huo kati ya Wilaya ya Mkalama na mashirika hayo unapaswa kuenziwa kwa njia ya utunzaji bora wa miradi hiyo ili kuwapa nguvu wafadhili hao kuendelea kuboresha miundombinu mingine iliyopo Wilayani hapa.

“Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwenu na mimi huwa napenda kusema kuwa kushukuru ni kuomba tena hivyo ninawaomba kama ilivyowapendeza kwa upande wa Munguli Magharibi, muiangalie Munguli Mashariki kwa jicho hilo hilo kwani nao wanahitaji sana miradi mliyoiweka hapa kwa wenzao” Aliongeza Mhe. Nchimbi.

Suala la upandaji wa Miti ya Korosho na matumizi mazuri ya Fedha zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ni moja ya mambo yaliyosisitizwa na Mhe. Nchimbi katika hotuba yake kijijini hapo ambapo aliagiza wakuu wa shule zote za Msingi na Sekondari kuhakikisha wanapanda korosho katika mashamba ya shule zao na walengwa wote wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii wanatumia fedha hizo kujikwamua kiuchumi badala ya kuzitumia kwenye ulevi na anasa nyingine.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka  aliyashukuru Mashirika ya NCA na 4CCP kwa kuwezesha miradi hiyo mikubwa Wilayani kwake ambapo aliwaagiza wananchi wa Kijiji hicho kuhakikisha hawafanyi shughuli za kiuchumi katika maeneo yaliyo karibu na mradi wa Maji ili kuweza kuulinda mradi huo.

Kwa upande wake Afisa Miradi wa Mashirika ya NCA na 4CCP Nelson Faustineamewashukuru viongozi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa ushirikiano Mkubwa waliouonesha katika kipindi chote cha Ujenzi wa Miradi hiyo jambo ambalo alikiri kutolipata kwa kiwango hicho  katika maeneo mengine yote waliyotekeleza miradi yao.

“Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wametuonesha ushirikiano mkubwa sana na ilifikia hatua tulikuwa tunawapigia simu muda wowote tunaaohitaji msaada wao na wao hawakusita kutusaidia” Alisisitiza Faustine.
Mashirika ya NCA na 4CCP yametekeleza miradi hiyo  kwa kushirikiana na Kanisa la Kilutheri la Hydom lililopo Wilayani Mbulu Mkoani Manyara.




No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA