Friday, 7 September 2018

Pikipiki hizi zisitumike kwenye michepuko-DC

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akizungumza na maafisa elimu kata wa Wilaya hiyo (hawapo pichani) muda mfupi kabla ya kuwakabidhi pikipiki zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la EQUIP-T.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga (kulia) akitoa maelezo ya awali muda mfupi kabla ya kumkaribisha mkuu wa Wilaya ya Mkalama (katikati) aweze kukabidhi pikipiki zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la EQUIP-T.

Maafisa elimu kata wa Wilaya ya Mkalama wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka (hayupo pichani) muda mfupi kabla hawajakabidhiwa  pikipiki zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la EQUIP-T.

Hizi ndio pikipiki walizokabidhiwa maafisa elimu kata leo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka amekabidhi jumla ya pikipiki 17 zilizotolewana shirika lilisilo la kiserikali linalojulikana kama “EQUIP-T”  ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na shirika hilo kama sehemu ya kuwapa hamasa maafisa elimu kata wilayani hapa.


Hafla hiyo fupi ilifanyika mapema leo asubuhi kwenye viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambapo Mhe. Masaka aliwataka maafisa elimu hao kuhakikisha wanatumia vyombo hivyo vya usafiri kuinua kiwango cha elimu wilayani Mkalama.

“Pikipiki hizi sio za matumizi binafsi na msizitumie kwenda kwenye michepuko yenu kwa sababu tunahitaji kuona pikipiki hizi zinapunguza idadi ya mimba shuleni na zinaongeza kiwango cha ufaulu” Alisisitiza Mhe. Masaka.

Kwa upande wake mwakilishi wa maafisa  elimu kata hao ambaye pia ni Afisa elimu kata wa kata ya Msingi, Bw. Elisante Mbazi aliishukuru serikali na shirika la EQUIP-T kwa vitendea kazi hivyo ambapo kwa niaba ya maafisa elimu kata wenzake, aliahidi kutumia pikipiki hizo kuongeza kiwango cha ufaulu na kuboresha elimu kwa ujumla wilayani Mkalama.

“Tulikuwa tunapata changamoto ya kuzifikia baadhi ya shule kwa ajili ya ufuatiliaji lakini sasa kupitia pikipiki hizi za kisasa, changamoto hiyo imeisha” Alimalizia Mbazi.
Pikipiki hizo zilizokabidhiwa leo zilikuwa na viambatanishi vyake vyote vya msingi ikiwemo kofia ngumu na  ‘’gloves’’ za kuvaa mikononi wakati wa kuendesha.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA