Tuesday 28 November 2017

MKALAMA MMETEKELEZA- KAKUNDA



PICHA 10 CHINI: Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Joseph Kakunda akisalimiana na viongozi na wakuu wa idara mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama mara baada ya kuwasili katika eneo la mradi wa Maji wa Iguguno.











Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka (Aliyesimama) akizungumza machache kabla ya kumkaribisha Mhe. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Serikali za Mitaa Mhe Joseph Kakunda (kulia).

Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Joseph Kakunda akizungumza na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama mara baada ya kuwasili katika kata ya Iguguno mapema leo

Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Joseph Kakunda akihakiki kiwango cha saruji kilichowekwa kwenye mchanga wa kujengea darasa katika shule ya Msingi Kibololo alipofanya ziara ya kikazi Wilayani Mkalama mapema leo
Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Joseph Kakunda (katikati) akisisitiza jambo mara baada ya kuona zoezi la uchimbaji wa kisima kikubwa cha maji katika kata ya Nduguti (kama inavyoonekana nyuma yao) Wengine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga.



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akisoma taarifa ya Wilaya mbele ya Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Joseph Kakunda makao Makuu ya Wilaya hiyo yaliyopo kata ya Nduguti.

Mbunge wa Jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula akizungumzia changamoto na mafanikio mbalimbali ya Wilaya ya Mkalama mbele ya Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Joseph Kakunda makao Makuu ya Wilaya hiyo yaliyopo kata ya Nduguti.




“Hongereni kwa kuwa na mradi mkubwa wa maji ambao kwa hakika umewaongezea uwezo mkubwa wa kutoa huduma ya maji katika maeneo yote yanayozunguka kata ya Iguguno”

Hayo ni  maneno yaliyotamkwa na Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Joseph Kakunda mara baada ya kufika katika  kituo cha Kutolea huduma za maji kilichopo katika kata ya Iguguno wakati wa  ziara yake ya  Kikazi ya siku moja  aliyoifanya Wilayani Mkalama mapema leo hii.

Ziara hiyo ya Mhe. Kakunda ilihusu  ufuatiliaji wa utoaji wa huduma mbalimbali za jamii Wilayani hapa huku ikijikita zaidi katika sekta ya maji na Elimu ambapo mbali na kutembelea Kituo hicho Kikubwa cha Maji kilichopo katika kata ya Iguguno, pia alifika katika katika Shule ya sekondari ya Iguguno na kujionea miradi mikubwa iliyojengwa na serikali kupitia mafundi wa kawaida kwa utaratibu unaojulikana kitaalam kama ‘’Force Account’’.

Akiwa shuleni hapo Mhe. Kakunda alisifu ubora wa miradi hiyo inayojumuisha Madarasa 8, Mabweni mawili, Vyoo vyenye matundu 11, bwalo la chakula na Maabara ambapo vyote kwa pamoja vimegharimu kiasi cha shilingi milioni 416 tu ikiwa ni chini ya robo ya gharama  ambazo zingetumika kupitia  utaratibu wa Wakandarasi na wazabuni.

Kutokana na ubora wa miradi hiyo, Mhe. Kakunda alitumia nafasi hiyo kuziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatumia mafundi wa kawaida (local fundi) katika miradi yote midogo hasa ile inayohusu ujenzi wa madarasa, mabweni, vyoo, daharia  n.k ambapo alisisitiiza matumizi ya wakandarasi yawe ni kwenye miradi mikubwa tu.

Moja ya mambo yaliyoonekana kutomfurahisha Mhe. Kakunda katika ziara hiyo ni idadi kubwa ya wanafunzi wa kike waliokatishwa masomo yao kutokana na kupewa ujauzito ambapo Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bw. Fredi Kimeme  alitaja idadi ya  wanafunzi 12 waliokatishwa masomo yao kutokana na kupewa ujauzito tangu Mwezi Januari Mpaka sasa.

Kuhusiana na hilo, Mhe. Kakunda alitoa rai kwa wazazi na walezi wote nchini kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kukomesha suala hilo huku akiainisha mbinu ambayo inatumiwa na wazazi wengi kwa kufanya makubaliano na wahusika wa mimba hizo ili waepukane na kifungo cha miaka 30 jela jambo ambalo limesababisha kesi nyingi kutoripotiwa na zile zilizoripotiwa kufutwa kutokana na shahidi namba moja (Mjamzito) kukana uhusika wa mtuhumiwa juu ya ujauzito huo.

Hata hivyo Mhe. Kakunda alielezea dhamira ya Wizara yake kupeleka hati ya dharula bungeni ili itungwe sheria itakayofuta dhamana kwa mtu anayetuhumiwa kumpa ujauzito Mwanafunzi ambapo  pia utafanyika ufuatiliaji na uchunguzi kwa kila Mwanafunzi aliyepewa ujauzito mpaka atakapojifungua kisha mtoto huyo atapimwa DNA ili kuthibitisha kama mtuhumiwa ndiye baba wa mtoto au la.

Awali kabla ya kumkaribisha Mhe. Naibu Waziri, Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Alan Kiula alitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili Wilaya hiyo huku suala la ukosefu wa hospitali ya Wilaya na upungufu wa watumishi hasa katika sekta ya Elimu ya Afya likionekana kupewa kipaumbele zaidi ambapo Mhe. Kakunda aliwahakikishia viongozi, Watumishi na wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama kuwa Serikali imeshaweka katika mipango yake suala la ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Wilaya na kwamba halmashauri inapaswa kukamilisha taratibu za awali tu ikiwemo upatikanaji wa eneo la kutosha kwa ajili ya ujenzi huo.

“Hili la upungufu wa watumishi hasa walimu nalichukua na nawaahidi katika mgao huu wa Mwezi Desemba hadi januari tuwaangalia kwa jicho la pekee kabisa” Alihitimisha Mhe. Kakunda.







No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA