Monday 6 August 2018

Ni lazima taarifa za masoko ziwafikie wakulima- Masaka

PICHA 10 CHINI: Ziara  ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka aliyoifanya leo kwa kutembelea  mabanda mbalimbali ya maonesho ya Nanenane kanda ya kati yanayofanyika jijini Dodoma.











Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka leo alikuwa mgeni rasmi katika manesho ya 22 ya sikukuu ya Wakulima na Wafugaji (nanenane) kanda ya kati ambapo alitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika viwanja vya maonesho hayo jijini Dodoma.

Ziara hiyo ya Mhe. Masaka ilianzia katika banda la Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambapo aliishauri wizara hiyo kufanya matumizi mbadala ya jengo lao walilolijenga kwa ajili ya  maonesho ya Nane nane badala ya kuliacha wazi huku likisubiri siku ambayo maadhimisho ya kitaifa yatafanyikia jijini Dodoma.

“Kuna taasisi mbalimbali zinapenda kushiriki maonesho haya lakini zimekosa maeneo ya kuweka bidhaa zao, mnaweza kuwapa jengo hilo au mnaweza hata kufikiria kuweka maonesho ya utamaduni ili wananchi waweze kufahamu kwa kina tamaduni za kitanzania kwa sababu kuliacha bila matumizi yoyote kama mnavyofanya hivi sasa ni kupoteza fedha za serikali ilizowekeza wakati wa kulijenga” Alisisitiza Mhe. Masaka.

Baada ya kutoka katika banda la TAMISEMI Mhe. Masaka alielekea katika banda la wataalam wa ufugaji wa kisasa wa kuku wanaojulikana kama ‘’Silverland’’ ambapo akiwa hapo aliwashauri wataalam hao kuhakikisha elimu inayohusu ufugaji wa kuku ifike mpaka kwa wafugaji wadogo badala ya kuishia kwenye maonesho ya Nanenane.

Mhe. Masaka ambaye katika ziara hiyo aliongozana na viongozi wengine waandamizi wa Mkoa wa Dodoma na Wizara ya Kilimo alifika pia  katika banda la Mamlaka ya Maendeleo ya biashara (TANTRADE)  ambapo akiwa hapo aliisisitiza mamlaka hiyo kuhakikisha inatoa matangazo kwa wakulima juu ya masoko ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha.

“Sasa hivi wakulima wanalima lakini wengi hawajui masoko ya mazao wanayolima yako wapi matokeo yake wanajikuta wanalima kilimo kisicho na tija hivyo ninawashauri mtengeneze utaratibu mzuri wa kuwajulisha wakulima kuhusu aina ya mazao yanayohitajika sokoni na mahali yanapohitajika mazao hayo’’ Aliongeza Mhe. Masaka.

Mbali na mabanda hayo Mhe. Masaka pia alitembelea Mamlaka ya Uhamiaji, benki ya CRDB, halmashauri za wilaya za Mkalama na Chamwino, AGRICOM na Polymachinery, Sido na Benki kuu ya Tanzania (BOT).



No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA