Saturday, 4 August 2018

Miaka minne ijayo Singida na Dodoma tutaongoza korosho- Nchimbi

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akitoa hotuba jioni ya leo wakati akifungua rasmi maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na wafugaji maarufu kama nanenane kanda ya kati  jijini Dodoma.
‘’Nyie wote mlioshiriki katika maadhimisho haya ya Sikukuu ya Wakulima na wafugaji mnatakiwa kuhakikisha yale mliyojifunza yanaonekana kupitia kwa wananchi wenu huko mlipotoka’’

Ni moja ya kauli zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi wakati wa hotuba yake muda mfupi kabla hajafungua rasmi maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji kanda ya kati maarufu kama Nane nane yanayoendelea hapa jijini Dodoma.

Katika hotuba yake Mhe. Nchimbi alibainisha kuwa mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi trilioni 13.8 kwa ajili ya Kilimo na Mifugo hivyo aliwataka wadau wa sekta hizo kutumia fursa hiyo vizuri na kuhakikisha sekta za kilimo na mifugo zinakuwa chachu ya kuhakikisha azma ya Tanzania kuelekea kwenye uchumi wa viwanda inatimia.

“Leo wakati natembea kwenye mabanda mbalimbali nimekutana na mkulima ambaye katika maelezo yake amenieleza kupitia boga moja nililomkuta nalo badala ya kuliuza shilingi elfu 10 ana uwezo wa kulitumia  kuingiza zaidi ya shilingi laki moja kwa kutengeneza juice, maandazi na keki” Alisema Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi alisema kuwa hivi sasa zao la korosho  limekuwa ni zao mkakati katika mikoa ya Dodoma na Singida  ambapo viongozi wa mikoa hiyo wanataka kuhakikisha ndani ya miaka minne ijayo mikoa hiyo itakuwa vinara wa mazao hayo.

“Kwa bahati mbaya katika maeneo yaliyozoeleka kulima mazao hayo tafiti zinaonesha wanavuna mazao hayo mara moja tu kwa msimu lakini huku kwetu hasa mkoani Singida imeshathibitika zao la korosho kuweza kuvunwa mara mbili kwa mwaka” Aliongezea Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi amewataka Wakulima kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuendelea kuongeza kipato kupitia sekta hiyo kwa mwaka mzima badala ya hivi sasa ambapo wakulima wengi baada ya kuuza mavuno yao hushinda vijiweni huku wakisubiri msimu wa masika.


No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA